Habari za Punde

Dk Shein: Tuko tayari kushirikiana na Italia katika masuala ya hifadhi ya sehemu za kihistoria


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                   21 Januari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema iko tayari kushirikiana na Serikali ya Italia katika nyanja za elimu na hifadhi ya sehemu za historia kama ilivyo katika sekta nyingine.

Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akizungumza na Balozi wa Italia nchini Bwana Luigi Scotto aliyemtembelea Ikulu jana.

Katika mazungumzo hayo Balozi Luigi alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake imeanzisha Mpango wa Ushirikiano Kati ya Italia na Afrika ambao umelenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hiyo na nchi za Afrika.

Alibainisha kuwa chini ya mpango huo Zanzibar inaweza kufaidika katika suala la uhifadhi na ukarabati wa sehemu za historia kama vile Mji Mkongwe pamoja na masuala ya ufundishaji wa lugha ya Kitaliano hapa nchini.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi Luigi kuwa ukarabati na uhifadhi wa mji Mkongwe ni suala linalopewa umuhimu mkubwa na Serikali hivyo fursa ya kushirikiana na Serikali ya Italia katika suala hilo imekuja wakati muafaka.

Aliongeza kuwa mpango wa kufundisha ya lugha ya kitaliano nao ni muhimu na unaweza kutekelezwa kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar-SUZA chini ya Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni katika chuo hicho.

Kwa hiyo Dk. Shein alimwambia Balozi huyo kuwa Zanzibar inaukaribisha mpango huo kwa mikono miwili na kupendekeza kuwekwa kwa utaratibu utakaowezesha utekelezaji wake kwa kuhusisha wizara na mamlaka husika.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliishukuru Serikali na wananchi wa Italia kwa misaada yao kwa Serikali na wananchi wa Zanzibar.

Alitaja baadhi ya misaada hiyo ikiwemo kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (European Development Fund) ambao Italia ni mwanachama pamoja na Taasisi ya Ivo De Carneri ya nchi hiyo inayosaidia maabara ya uchunguzi wa magonjwa ya binadamu huko Pemba.

Kuhusu uhusiano wa kibiashara na Italia Dk. Shein alibainisha kuwa wawekezaji kutoka Italia hususan katika sekta ya utalii wameifanya sekta hiyo kukua haraka na kuweza kuchangia sehemu kubwa ya mapato ya Taifa.

Dk. Shein alimhakikishia Balozi Luigi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufanyakazi na Serikali ya Italia ili kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi mbili hizo.

Balozi Luigi Scotto kwa upande wake alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake inaupa umuhimu mkubwa uhusiano wake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar ikiwemo.

Alifafanua kuwa mbali ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanywa na wananchi wa Italia humu nchini, nchi mbili hizo zina mambo yanayofanana kama vile sehemu nyingi za kihistoria.

Hivyo kwa kuwa Italia ina utaalamu na uzoefu mkubwa katika uhifadhi na ukarabati wa sehemu za historia hivyo alisema Zanzibar inaweza kufaidika na uhusiano wake na nchi hiyo.

Alieleza kuwa amefanya safari nyingi Zanzibar kikazi na binafsi na kutembelea sehemu za historia kama Mji Mkongwe na kugundua kuwa sehemu hizo zinahitaji ukarabati ili kuendelea kuwa kivutio na pia kudumisha kumbukumbu hiyo muhimu ya historia ya Zanzibar na ulimwengu.

Balozi Luigi alisema Serikali ya nchi yake iko tayari kufundisha lugha ya Kitaliano humu nchini kwa kushirikiana na Taasisi za elimu pamoja na kuanzisha kituo cha utamaduni cha Italia.

Alisema kuwa lugha hiyo hivi sasa imepata nafasi kubwa katika kukuza mawasiliano kati ya wananchi wa Italia na watu wa Zanzibar hadi kufikia kuwa miongoni mwa lugha zinazotumiwa sana hivi sasa hapa Zanzibar hasa katika sekta ya utalii.
  
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.