Na Mahmoud Ahmad,Mwanza
MEYA wa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, Nd. Henry Matata, kupitia
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amekiponda vikali chama hicho
akidai kimekuwa kikijiendesha kwa
kutumia mabavu,ukabila na uchu wa madaraka na kwamba kuna viongozi hawaguswi.
Alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa
habari hizi ofisini kwake kuhusiana na mgogoro wa umeya katika manispaa hiyo
baada ya kuwafukuza madiwani wenzake watatu wa Chadema kwa kushindwa kuhudhuria
vikao vitatu mfululizo.
Alisema mfumo wa chama hicho ni batili kwa kuwa umekuwa ukiendesha
mambo yake kimabavu kwa kuangalia sura za watu na kudai kuna watu ndani ya
chama hicho hata wakifanya makosa hawaguswi.
Alisema uendeshaji wa mambo ndani ya chama hicho ni batili kwa kuwa
katiba ya chama hicho inaminywa maksudi bila demokrasia kuchukua mkondo wake.
“Mfumo wa Chadema ni batili unakwenda kinyume na sheria za nchi,chama
kinaendeshwa kimabavu na ukabila, kuna watu wakifanya makosa hawaguswi,”
alisema.
Akizungumzia ugomvi baina yake na Mbunge wa jimbo la Ilemela, Highness
Kiwia, alisema Mbunge huyo hajitambui na wala hatambui nafasi yake huku
akisisitiza kuwa vurugu anazofanya ni kutokana na hofu kwamba huenda yeye
akagombea katika uchaguzi ujao kwa kuwa anakubalika na watu.
Kuhusu hatma yake ndani ya Chadema alisema katika uchaguzi mkuu ujao
ataangalia chama kinachomfaa lakini kwa sasa amebaini kwamba chama kilicho na
demokrasia ni CCM pekee kwa kuwa hakiendeshwi kibabe.
“Nitaangalia chama ambacho kitanifaa lakini kwa sasa nawaona CCM afadhali
kwani hakina ugomvi, ubabe, kufukuzana, uhasama tofauti kabisa na
Chadema,”alisisitiza.
Kuhusu hatma ya madiwani wa Chadema aliowafukuza, alisema suluhisho ni serikali kutangaza uchaguzi
mdogo kwa nafasi hizo vyenginevyo ni sawa na “kutwanga maji kwenye kinu.”
Alisema yeye kama meya wa Chadema ataendelea kuchapa kazi za
kuwatumikia wananchi bila wasiwasi na endapo kama kuna diwani atakiuka sheria
ya kushiriki vikao vya baraza la madiwani mara tatu mfulululizo atachukuliwa
hatua bila kujali chama anachotoka.
Aidha alisema kamwe madiwani hao hawana haki ya kukata rufaa kwa
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda zaidi ya kwenda mahakamani.
No comments:
Post a Comment