TAARIFAA YA SERIKALI KUHUSU
TUKIO LA AJALI YA KUDONDOKA ABIRIA WALIOKUA WAKISAFIRI KUTOKA PEMBA KUJA UNGUJA
LEO TAREHE 05-01-2014 KWA BOTI YA
KILIMANJARO II
Ndugu Wanahabari
Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais, tumewaita muda huu kuwaeleza kwa majonzi makubwa kuhusu tokeo la ajali ya
kudondoka kwa baadhi ya abiria waliokua wakisafiri kutoka Pemba kuja Unguja,
kwa boti ya MV. Kilimanjaro II.
Ndugu Wanahabari
Kunako majira ya saa 3:00 za asubuhi wakati boti hiyo ikiwa
safarini kutoka Pemba kuja Unguja ilipofika katika maeneo ya bahari ya Nungwi ilikumbwa na
mawimbi makali, mawimbi ambayo yalisababisha baadhi ya abiria waliokuwa wamekaa
nje sehemu ya mbele kusombwa na mawimbi na kudondoka baharini.
Ndugu Wanahabari
Baada ya kutokea tukio hilo, vyombo vya Serikali vikisaidiwa
na wananchi wa Nungwi na wa maeneo ya jirani walifika katika eneo la tukio kwa
ajili ya kufanya uokozi. Katika zoezi hilo, vyombo hivyo vimefanikiwa kuokoa
watu watatu (3) wote wanaume watu wazima wakiwa wako hai na hali zao
zinaendelea vizuri katika hospitali ya Mnazi Mmoja. Aidha, jumla ya maiti
watano (5) wamepatikana. Kati ya hao, wanaume watatu (mmoja mtu wazima na
wawili watoto) na wanawake wawili (mmoja mtu mzima na mmoja mtoto).
Maiti tatu tayari zimeshatambuliwa na kukabidhiwa jamaa zao
(wanaume wawili na mwanamke mmoja). Maiti wawili waliokuwa bado hawajatambuliwa
wapo katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.
Tunawaomba wananchi waende kuwatambua ndugu na jamaa zao na kukabidhiwa kwa
ajili ya hatua za mazishi.
Ndugu Wanahabari
Vyombo vyetu bado vinaendelea na kazi za utafutaji wa abiria
wengine na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kwa kadri hali itakavyoendelea.
Ndugu Wanahabari
Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar natoa mkono
wa pole kwa ndugu na jamaa wa waliopoteza maisha yao na tunamuomba Mwenyezi
Mungu awalaze Marehemu mahala pema peponi AMIN. Vilevile tunawaomba Mwenyezi Mungu awajaalie
afya njema majeruhi wote.
Nachukua fursa hii kuwaomba wananchi wenzangu ambao
hawajawaona ndugu na jamaa zao waliosafiri na chombo hicho wapeleke taarifa
hizo kwa Masheha wa Shehia zao, Wakuu wa Wilaya, Vituo vya Polisi, Mamlaka ya
Usafiri Baharini au Idaya ya Kukabiliana na Maafa Unguja na Pemba.
Ndugu Wanahabari
Naomba nichukue nafasi hii kwa mara nyengine tena, kuwaomba
wananchi wote tuwe na subra wakati huu wa msiba na kwa wale tunaotumia bahari
kwa usafiri na shughuli nyengine tuendelee kuchukua hadhari wakati huu wa upepo
mkali na tufuatilie taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kuepukana na madhara
ambayo yanaweza kupatikana.
Ahsanteni
sana
Dkt.
Khalid S. Mohamed
KATIBU
MKUU
OFISI
YA MAKAMU WA PILI RAIS
ZANZIBAR
Katibu mkuu unasema watu wachukue tahadhari. Hivi kwani Serikali nzima hiyo haiwezi kuvizuia vyombo hivi visifanye safari pale ambapo hali ya hewa inaonekana mbaya kiasi hicho. Hasa ukizingatia kwamba Zanzibar hatuna vyombo na utaratibu wa uokozi kwa maafa haya.
ReplyDeleteTeknolojia zilizojaa munashindwa na hata utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa vyombo vya bahari na hali ya hewa.
Baada ya kepteni wa meli hii kuona hali kua mbaya kwanini kusiwe na utaratibu wa kuwazuia watu wote wasikae nje ya boti hilo.
Tutauana kizembe hadi lini.