Habari za Punde

Ajali ya Boti ya Kilimanjaro 2 Ikitokea Pemba na Kukumbwa na Upepo Nungwi.

Na Mwandishi Wetu.
BOTI ya abiria ya  Kilimanjaro II yanusurika kuzama katika mkondo wa Nungwi wakati ikitokea kisiwani Pemba na kuelekea kisiwani Unguja.

Akisimulia chanzo cha ajali hiyo shuhuda mmoja ambae ni miongoni mwa wasafiri waliokuwemo ndani ya boto hiyo,Sleiman Mohammed Said alisema wakati walipofika  maeneo ya Nungwi hali ya hewa ilibadilika na bahari kuwa na mawimbi makubwa.

Alisema boto hiyo ilipingwa na wimbi zito na hatimae kusababisha kuingia maji ndani ya boti hilo na baadhi ya abiria  na mizigo kuburuzwa baharini.

Aidha alisema kutokana na ukali wa mawimbi hayo hivyo mashine ya boto hiyo ilizima moto kwa muda,hali ambayo ilizidisha taharuki na hofu kwa abiria waliokuwemo ndani ya boti hiyo huku wachache kukimbilia ndani.

"Baadhi ya watu waliokuwa wamekaa mbele ya boti hiyo wametumbukia baharini na baadhi ya mizingo mimi nilikuwa na ndugu zangu wawili tumekaa pamoja mpaka sasa sijawaona na hadi  boti imeshusha abiria wao hawamo"alisema Sleiman.

Hata hivyo alisema mara tu ya kuwaka kwa mashine boti iliendelea na safari.

"Ilivyowaka mashine boti ile ilifanya safari na haikurejea nyuma kwa ajili ya kufanya utaratibu kwa wale abiria walioingia baharini lakini walituwahisha sisi"alisema


Naye Ali Pandu mkaazi wa Mtoni  ambae alifika bandarini hapo kwa kutaka kujua hatima ya ndugu zake wawili aliowataja kwa jina moja Nahiri(17) na Ali(19) ambao walikuwa wamesafiria  boti ya Kilimanjaro II, alilieleza gazeti hili kwamba hawaelewi kama wapo hai au wameshafariki kwani inasemekana hawakuwemo ndani ya boti hilo baada ya kutokea tukio hilo.

"Hawa jumla yao walikuwa watatu mwenzao mmoja yupo lakini na yeye anasema baada ya kutokea kwa tokeo hilo hakuwaona wenziwe mpaka sasa na walikuwa wamekaa mbele"alisimulia.

Kwa upande wa mwananchi Abdalla Mohammed ambae watoto wake walikuwemo katika bato hiyo alisema mnamo majira ya saa mbili hadi tatu alipokea simu kutoka kwa mtoto wake Mohammed Abdalla(17) ambapo alimueleza kwamba hali iliyowafika katika safari yao.

Alisema baada ya kupata simu hiyo alijaribu kuwapigia tena simu lakini alikosa mawasiliano yoyote kutoka kwa watoto wake hadi anazungumza na gazeti hili.

"Watoto wangu walinipigia simu wakanambia baba tunazama tunakufa sisi"alisema mzee huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Abdi Omar alikiri kujitokeza kwa msukosuko wa mawimbi baharini na kusababisha kupotea kwa baadhi ya abiria na mizigo.

Alisema bado hawajakuwa na taarifa kamili ya abiria waliopotea lakini hata hivyo wamekatika utaratibu wa kuelekea eneo la tukio kwa ajili ya kusaka abiria pamoja na mizingo.        


2 comments:

  1. Mwenyezi Mungu awape subra wafiwa. Ni kazi yake Mungu haina makosa.

    ReplyDelete
  2. na bakharesa nawe viboti vyako vidogo sana yakhe

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.