Na Salum Vuai, MAELEZO
UONGOZI mpya wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), umeanza
kupunguza changamoto za kiofisi zinazokikabili kwa miaka mingi baada ya kufanikiwa kununua gari mbili ili
kurahisisha utendaji wake.
Gari hizo aina ya NOAH zilizonunuliwa nchini Dubai
(U.A.E) zikiwa na thamani ya shilingi 19,900,000, zilikabidhiwa jana kwa
uongozi wa chama hicho na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said
Ali Mbarouk, katika ofisi za ZFA zilizoko uwanja wa Amaan.
Akizungumza katika hafla hiyo kabla kukabidhi funguo za
gari hizo, Waziri huyo alisifu hatua ya chama hicho kwa kuamua kufanya kazi
kisasa, akisema vyombo vya usafiri ni nyenzo muhimu katika utendaji wa taasisi
yoyote.
Aidha alisema kupatikana kwa gari hizo, kutasaidia
kupunguza changamoto zinazokwamisha shughuli za ZFA, lakini akawasisitiza
viongozi wa chama hicho waendeleee kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau
wengine ili kuleta maendeleo ya mpira wa miguu Zanzibar.
Alieleza kufarijika kwake na namna ZFA ilivyoanza
kubadilika na kuondokana na migogoro aliyoirithi wakati akikabidhiwa wizara
yake, na kutaka vyama vyengine vya mnicxezo viige mfano wa chama hicho kwa
kubuni njia za kujitafutia mapato badala ya kupeta miguu na kusubiri ruzuku ya
serikali.
"Hatutaki vyama vinavyojiendesha kwa ofisi za
mifukoni, au kuishi kwa migogoro na malumbano kupitia vyombo vya habari. Vyama
kama hivyo havitufai na nimemuelekeza Mrajis avifutilie mbali," alifafanua
Waziri Mbarouk.
Mapema, Makamu wa Rais wa ZFA Pemba Ali Mohammed, alisema
baada ya kununua gari hizo kwa ajili ya ofisi za chama hicho Unguja na Pemba,
katika miezi michache ijayo, wanakusudia kununua gari nyengine kumi kwa ajili
ya ofisi zote za ZFA wilayani.
No comments:
Post a Comment