Na Mwandishi Wetu.
VIWANJA vya Polisi Ziwani mjini Zanzibar, juzi usiku
vilimeremeta na kugeuka kiota cha burudani kutokana na mirindimo maridhawa ya muziki wa taarab asilia
ulioporomoshwa na kikundi cha Taifa katika kusherehekea nusu karne ya Mapinduzi
matukufu ya Januari 12, 1964.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe. Dk, Ali Mohamed Shein, akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Kikwete, waliungana na wananchi mbalimbali
kuwashuhudia magwiji hao wa taarab
wakishusha kibao kimoja baada ya chengine, huku wakipulizwa na upepo mwanana
uwanjani hapo.
Katika staili ya aina yake, kikundi hicho kilikuwa
kikiongozwa na washereheshaji (MC) wawili, Chimbeni Kheri wa klabu ya Culture
pamoja na Ali Masoud wa Nadi Ikhwan Safaa.
Pazia la burudani lilifunguliwa na mwimbaji Hilda
Mohammed aliyeanza kwa wimbo maalum, Miaka 50 ya Mapinduzi, huku bibiye Fauzia
Abdallah akihanikiza kwa kibao chake, Mapenzi yako matamu.
Waimbaji wengine waliotamba na kulitikisa eneo hilo
ambako Mapinduzi ya 1964 ndiko yalikoanzia na nyimbo walizoimba zikiwa kwenye
mabano, ni Khamis Nyange 'Profesa Gogo' (Lulu namba 2), Sihaba Juma (Faida za
Mapinduzi na Mtumwa Mbarouk (Mpewa hapokonyeki, ombi la Rais Shein na
Tunapendana).
Wengine ni Iddi Sued (Tusherehekee Mapinduzi), Khofu yako
iondoe (Rukia Ramadhan) na Bahati (Fatma Issa) ambayo ilighaniwa baada ya
kuombwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis.
Kutokana
na umahiri waliouonesha katika kucharaza vinanda na kuimba, sambamba na ufundi
wa MC Chimbeni katika kulitawala jukwaa, wasanii hao walifanikiwa kumfanya Rais
Kikwete atie mkono mfukoni na kuwadondoshea bahasha
No comments:
Post a Comment