Habari za Punde

DK SHEIN AZIAMBIA WIZARA NA TAASISI ZAKE: WAELEZENI WANANCHI MNAVYOTEKELEZA MAJUKUMU YENU

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                       15 Aprili, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amerejea wito wake wa kuzitaka Wizara na Taasisi za Serikali kuwaelimisha wananchi juu ya shughuli wanazozifanya ili wananchi waweze kufahamu namna Serikali inavyofanyakazi ikiwemo kushughulikia matatizo yanayowakabili.
Akikamilisha mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2013/2014 leo Dk. Shein alisema Wizara hiyo na taasisi zake inafanya shughuli nyingi ambazo ni muhimu wananchi kuzielewa kwa kuwa zinagusa maisha yao ya kila siku.
Alitolea mfano Mamlaka ya Maji nchini - ZAWA ambayo imepiga hatua nzuri katika kulipatia ufumbuzi suala la uhaba wa maji katika baadhi ya sehemu za mji wa Zanzibar hivyo hivyo ni muhimu kwa shirika hilo kuwaelimisha wananchi juu ya hatua hizo ili waweze kufahamu mwenendo wa utatuzi wa tatizo hilo ikiwemo hali ilivyokuwa, ilivyo sasa na mwelekeo wa baadae kuhusu tatizo hilo.
Halikadhalika ameitaka wizara hiyo kubuni mkakati madhubuti wa kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la kuziba mara kwa mara kwa mfumo wa majitaka wa nyumba za maendeleo za Michenzani, Kilimani na Kikwajuni pamoja na kubuni mpango mpya wa kushughulikia suala la majitaka katika mji wa Zanzibar kwa kuzingatia hifadhi na usafi wa mazingira.
Katika mkutano huo Mhe Rais aliipongeza Wizara hiyo kwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika kupindi husika pamoja na kutambua changamoto zilizowakabili katika kipindi hicho.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ali Khalil Mirza alisema katika kutekeleza malengo ya Wizara mwaka 2013/2014 Wizara imeweza hadi 31 Machi 2014 kukusanya mapato ya Tshs bilioni 2.8 kati ya lengo la kukusanya Tshs bilioni 4.0 ikiwa ni aslimia 70 ya lengo.
Aidha, kwa upande wa mahkama ya Ardhi imeweza kuvuka lengo kwa asilimia 239 kwa kusikiliza na kuzitolea hukumu kesi 251 kutoka lengo la kesi 105 Unguja na Pemba ambapo kati ya hizo kesi hizo 147 kwa upande wa Unguja na 104 huko Pemba.
Kwa upande wa ukaguzi wa maeneo ya uwekezaji Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa jumla ya miradi 303 imefanyiwa ukaguzi Unguja na Pemba kutoka lengo la kukagua miradi 280.
Katika taarifa hiyo Bwana Mirza alibainisha kuwa zoezi la usajili wa ardhi linaendelea vizuri ambapo Wizara hiyo imebuni mpango mpya wa kutoa kadi maalum kwa wamiliki wa ardhi ili kuleta ufanisi katika mfumo mzima wa usajili wa ardhi.   
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.