Habari za Punde

Dkt.Shein Aitaka Wizara ya Habari Kukabiliana na Harakati na Changamoto Zinazoikabili Suala la Vingamuzi vya ZBC.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                        23 April, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa taasisi za serikali kufanyakazi kwa pamoja katika kupanga na kugawana rasilimali fedha ili kufanikisha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa.
 Amesema utaratibu wa kupanga na kutekeleza kwa pamoja kazi za Wizara na kuweko na uwazi katika ugawanaji na utumiaji wa rasilimali fedha ndio njia pekee zitakazosaidia kufikia malengo yaliyopangwa na Wizara kwa ufanisi.
 Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema jana alipokuwa akizungumza na uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwenye kikao cha kutathmini utekelezaji wa mpango kazi na bajeti ya Wizara hiyo katika kipindi cha miezi tisa  kuanzia Julai 2013 hadi 2014.
Amesema watendaji wa serikali wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa fedha za umma zinazopatikana baada ya kukusanywa kutokana na kodi na malipo mengine mbali mbali zinatumiwa ipasavyo ili kuhakikisha kuwa tija inayotokana na matumizi ya fedha hizo inaonekana na inawanufaisha wananchi wote.
“Lazima tuweke mipango mizuri itakayohakikisha  kuwa fedha zinazokusanywa na wenzetu wa Bodi ya Mapato Zanzibar –ZRB, Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA na  hata taasisi kama yenu zinagawanywa vizuri na zinatumika kwa mambo muhimu ambayo tija yake itaonekana kwa watu wengi”, alisema Dk. Shein.

Ameongeza kuwa ni vyema kwa kila taasisi ya serikali kuwa na muongozo utakaoweka bayana vipaumbele vyake, na kwamba mgawanyo wa fedha hauna budi kufanywa kwa mujibu wa vipaumbele vitakavyobainishwa kwenye muongozo husika.
Akizungumzia suala la kuimarisha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Rais wa Zanzibar ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuchukua hatua za dharura kukabiliana na changamoto zinazolikabili Shirika hilo ili liweze kuendesha shughuli zake kwa mafanikio sambamba na kukabiliana ushindani mkubwa wa kibiashara. 
Amesema serikali tayari imeshaweza fedha nyingi kwenye Shirika hilo na kusisitiza kuwa hakuna sababu ya shirika hilo kushindwa kujiendesha kibiashara.
Dk Shein alisisitiza kuwa Wizara hiyo haina budi kuendelea na jukumu lake la kuhakikisha kuwa ZBC inapiga hatua na inakwenda sambamba na matumizi ya teknologia ya kisasa hasa baada ya hatua ya serikali ya kuwekeza fedha nyingi kwenye matumizi ya mradi wa Zanzibar Digital Network.
Ameagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuzishughulikia kwa haraka changamoto zote zinazokwamisha ufanisi katika suala zima la ving’amuzi na mradi mzima wa kuhama kutoka kwenye analogia kwenda kwenye Digitali.
Aidha, Rais wa Zanzibar ameiagiza Wizara hiyo kufikiria namna gani itaweza kuimarisha Tume ya Utangazaji Zanzibar ili iweze kufanya kazi zake ipasavyo.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.