Na Kija
Elias, Mwanga
Rais Jakaya Kikwete, amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa siasa, walioko ndani ya
Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao wamekuwa waking’ang’ania madaraka, hali ambayo
imekuwa ikileta uhasama, chuki na manung’uniko na wingine kukimbilia
kujiunga na vyama vya pinzani.
Alisema hayo
wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wakati akizungumza na wakazi wa Mwanga
katika sherehe za kumuaga Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
“Uongozi ni dhamana lakini wapo
viongozi wamekuwa ving’ang’anizi katika kuachia madaraka, hunung’unika na
pale wanapokosa nafasi za uongozi huamua kukihama chama wakidhani kuwa ni
suluhisho,”alisema.
Alisema wanapoambiwa wawapishe wengine
nao waweze kulisukuma gurudumu hilo, huisema vibaya CCM kuwa haithamini na
wakati mwingine wamekuwa wakisusia hata shughuli za maendeleo pindi
wanapoambiwa kuachia madaraka hayo.
“Nawaomba viongozi wenzangu
tujifunze kutoka kwa Msuya, ameamua kustaafu shughuli za chama ambazo alikuwa
akizifanya na hii ndio heshima kubwa kwa taifa,” alisema.
Katika ziara hiyo, Rais Kikwete aliweka
jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa na maabara ya taasisi ya kituo cha kiislamu
cha Vuchama na kuwataka viongozi hao kuhakikisha kituo hicho kuzitatua
changamoto za vitabu na walimu na ili watoto wanaosoma hapo wapate elimu bora.
Awali akitoa tarifa ya
kustaafu shughuli za chama, Msuya alimpongeza Rais Kikwete na serikali yake kwa
kuanzisha mchakato wa katiba mpya ambayo alisema itasaidia kuiongoza Tanzania kwa
miaka mingi ijayo.
Akitoa pongezi hizo, Msuya alisema
matatizo ambayo yanaendelea katika bunge la katiba yasiwakatishe tamaa Watanzania
na kamwe wasikubali kurudi nyuma.
Katika hatua
nyingine, Msuya aliipongeza serikali ya CCM kwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi
mwaka 1992 jambo ambalo limesaidia kuifanya Tanzania kupiga hatua kubwa katika
utawala wa kidemokrasia.
Alisema
viongozi wa chama hawana budi kuendelea kudumisha demokrasia ndani ya chama
hicho na kuondoa makundi ambayo yameanza kujitokeza.
Msuya
ameamua kustafu shughuli za chama ambazo amezitumikia kwa kipindi cha miaka 33.
No comments:
Post a Comment