Na Salum
Vuai, MAELEZO
SERIKALI ya
Mapinduzi Zanzibar, imeshauriwa kuanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya
kushughulikia kesi zinazohusu vitendo vya kuhujumiwa watalii na kuporwa mali zao.
Akizungumza
wakati wa mkutano wa kujadili mafanikio na changamoto za sekta ya utalii hapa Zanzibar ulofanyika hoteli ya Marumaru mjini Zanzibar mwishoni mwa
wiki, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) Bobby
Mackena, amesema wakati umefika wa kurekebisha baadhi ya sheria nchini.
Mackena
alisema wakati umefika kuunda mahakama hiyo kwa ajili ya kuharakisha kesi
za watalii wanaohujumiwa na wahalifu.
Alifahamisha
kuwa jumuiya yake imeandaa mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya kuyawasilisha
serikalini, kutaka baadhi ya sheria zirekebishwe ili ziende na wakati.
Katika
mkutano huo ulioshirikisha wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja
na vile vya sheria, Mackena alisema baadhi ya sheria zilizopo sasa, ni
kandamizi na zinawanyima fursa watalii wanaokumbwa na kadhia za kuvamiwa,
kushambuliwa na kuibiwa.
Alieleza
kwamba kumekuwa na vikwazo vingi vinavyokwamisha au kuchelewesha kesi hizo,
ikizingatiwa kuwa mara baada ya kuhujumiwa, mtalii hatamani tena kuendelea
kuwepo nchini.
Alisema,
sababu hiyo huzifanya mahakama zishindwe kuendelea na kesi hata kama mhalifu amepatikana, kwani sheria humtaka mtu
aliyehujumiwa afike mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi.
“Watalii
huchukizwa na vitendo vinavyotishia usalama wao na mara baada ya kuhujumiwa
hawapendi tena kubaki nchini na huamua kuondoka. Hili huchangia kufutwa kwa
kesi zao mahakamani. Tunaomba sheria ibadilishwe,” alifafanua.
Kwa hivyo,
alisema miongoni mwa mapendekezo ya ZATI ni kuiomba serikali kwa kushirikiana
na Kamisheni ya Utalii kuunda mahakama maalumu itakayoshughulikia kesi hizo na
kuzitolea hukumu kwa haraka zaidi ili kurejesha imani ya watalii juu ya
kulindwa kwa usalama wao.
ZATI
imependekeza mahakama hiyo maalumu iendeshwe kitaalamu na ikibidi kesi iweze
kusikilizwa na kutolewa hukumu ndani ya saa 24 tangu kuwasilishwa hasa ikiwa na
ushahidi uliokamilika.
Aidha
alisema pale inapotokea mtalii aliyekumbwa na kadhia ya kuhujumiwa na kuporwa
ameshaondoka nchini, serikali ifikirie uwezekano wa kuendesha kesi hizo kwa
njia ya mawasiliano ya teknolojia kwa kutumia video ikimuunganisha muhusika na
mahakama popote alipo duniani.
Naye
Mwenyekiti wa ZATI Abdulsamad Said, alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana
katika sekta ya utalii nchini, lakini matukio ya kuhumuiwa wageni kwa silaha za
moto, kudhuriwa na kuporwa, vinachangia kuwatia hofu watalii wanaokusudia
kufika Zanzibar .
Alisema
kutokana na maendeleo ya teknoljia ambapo dunia yote imo viganjani,
taarifa za matukio hayo zikiwemo za wageni na wenyeji kumwagiwa tindikali,
zinasambaa haraka duniani na kusababisha uhaba wa watalii wanaotarajiwa.
Alisema iko
haja ya kupanga mikakati madhubuti na ya uhakika itakayosaidia kupatiwa
ufumbuzi wa haraka kesi hizo ili kuzuia kuporomoka kwa idadi ya watalii, na
hivyo kushusha mapato ya taifa na wananchi wanotegemea sekta hiyo kujiajiri.
Hata hivyo,
pamoja na changamoto nyingi ikiwemo ya ulinzi na usalama, Mwenyekiti huyo
wa zati, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais
Dk. Shein, kwa kufanya kazi karibu na jumuiya yake, kuimarisha miundombinu na
kuweka mazingira mazuri ili kuhakikisha utalii unazidi kuimarika na kuendelea
kuwa muhimili mkuu wa uchumi wa nchi.
Aidha
aliishukuru serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuridhia maombi ya wanachama
wa ZATI kutaka kupunguziwa kodi na ada nyengine zinazotozwa katika sekta hiyo,
ambazo alisema ni kubwa kulinganisha na kupanda na kushuka kwa mapato
yatokanayo na biashara ya utalii.
“Hivi
karibuni tulimualika Waziri wa Fedha Mhe. Omar Yussuf Mzee katika mkutano wetu
mkuu Zanzibar Beach Resort. Tunashukuru alisikia kilio chetu cha kodi na ushuru
mkubwa, na ametutaka tuchague wawakilishi wetu kukaa na wataalamu wa ZRB na TRA
ili kujadili namna ya kulifanyia kazi jambo hilo ,” alifafanua Said.
Alisema
jumuiya yake itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na sekta nyengine
binafsi, ili kuhakikisha kwa pamoja zinaweza kuvutia watali wengi zaidi na
kuinua kipato cha wananchi na taifa kwa jumla.
No comments:
Post a Comment