Habari za Punde

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, utalii na Michezo





HOTUBA YA BAJETI YA WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, UTALII NA MICHEZO ZANZIBAR, MHESHIMIWA SAID ALI MBAROUK KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
       UTANGULIZI
1.      Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu muumba mbingu na ardhi na mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na uwezo kutukutanisha tena hapa leo hii, ili kujadili mambo muhimu ya maendeleo ya nchi. Tunamuomba atuongoze ili tuweze kutekeleza kazi hii kwa hekima na busara, na atuwezeshe kufanikisha malengo yetu kwa manufaa ya nchi yetu.
2.      Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako lipokee, lijadili na hatimaye likubali kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
3.      Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kuiongoza vyema nchi yetu.  Uongozi wake uliojaa hekima na busara umesaidia sana kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na katika ustawi wa jamii wa Zanzibar.
4.      Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba kuchukuwa fursa hii pia ya kuwapongeza Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa. Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa. Balozi Seif Ali Iddi kwa kutekeleza majukumu yao na kumshauri ipasavyo Mheshimiwa Rais.  Aidha, napenda kuwapongeza kutokana na juhudi wanazofanya katika kuyapatia ufumbuzi matatizo mbali mbali ya wananchi pamoja na kutetea haki zao.
 
5.      Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kukupongeza kwa dhati wewe, kwa umakini wako katika kuliongoza vyema Baraza la Wawakilishi.Pia pongezi hizi ziende kwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza lako kwa namna wanavyokusaidia katika kazi zako. Aidha napenda kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari Mheshimiwa. Mlinde Mabrouk Juma pamoja na wajumbe wote wa kamati hii kwa kutusaidia na kutushauri ipasavyo na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yangu.
6.      Mheshimiwa Spika, naomba pia kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Gando kwa mashirikiano mazuri wanayonipa katika kutekeleza utumishi wangu kwao.
 

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA 2013/2014
   7.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, ilikadiria kupata shilingi 10,215,458,134/= kwa kazi za kawaida na shilingi 510,000,000/= kwa kazi za maendeleo. Aidha Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 1,522,580,000/= zinazokwenda Mfuko Mkuu wa Serikali na shilingi 2,111,250,000/= zinazokusanywa na kutumiwa na taasisi husika.
 8.        Mheshimiwa Spika, jumla ya shilingi 6,841,986,973/= zilipatikana kwa kazi za kawaida sawa na asilimia 67 na shilingi 267,400,207/= kwa kazi za maendeleo sawa na asilimia 52. Aidha, Wizara ilikusanya shilingi 1,487,410,284/= sawa na asilimia 98 zilizoingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na shilingi 1,897,218,111/= sawa na asilimia 90 ambazo zimekusanywa na kutumiwa na taasisi za Wizara, (Tafadhali angalia kiambatisho namba 1a hadi 1d).
 
 
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KWA MWAKA 2013/2014 
Utekelezaji Halisi wa Miradi kwa mwaka 2013/2014
9.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara imetekeleza Miradi minne (4) ifuatayo:-
  (i)       Utengenezaji wa njia za kukimbilia za Uwanja wa Gombani
10.       Mheshimiwa Spika, lengo la mradi ni kuufanya Uwanja wa Gombani kuweza kukidhi viwango vya kimataifa kwa kujenga “base” itakayotumika kuweka mpira wa kukimbilia (tartan).   
            Mradi huu ulipangiwa shilingi 100,000,000/= ambazo zingeweza kuweka msingi “base” utakaotumiwa kuweka mpira wa kukimbilia. Hadi kufikia Mei 2014 jumla ya shilingi 90,000,000/= zimepatikana katika mradi huu sawa na asilimia 90. Kazi zinazoendelea kufanyika ni pamoja na utoaji wa matangazo ya zabuni, tathmini ya kumpata mshauri mwelekezi, utayarishaji wa michoro, kutoa zabuni ya mjenzi wa msingi na kuanza kazi hiyo.
   (ii)     Uhifadhi wa sehemu za kihistoria na mambo ya kale  
11.       Mheshimiwa Spika, lengo la mradi ni kuwa na maeneo ya kihistoria yaliyo endelevu kwa maendeleo ya Utamaduni na Utalii. Hatua mahsusi ni kuweza kuyapima na kuweka mipaka baadhi ya maeneo ya uhifadhi na kuyapatia hati miliki, Kutangaza na kuendeleza maeneno ya kihistoria, kuhifadhi mambo ya kale na sehemu za kihistoria, kukusanya, kusambaza na kuweka mabango ya maelezo katika maeneo ya kihistoria, kushajiisha jamii na kutangaza sehemu za kihistoria, Kuanzisha maeneo mapya ya kihistoria na makumbusho mpya, Kuwepo kwa maeneo bora ya kihistoria na mambo ya kale.
  Mradi huu ulitengewa shilingi 230,000,000/= ambapo hadi kufikia Mei 2014 jumla ya  shilingi 67,400,207/= ziliingizwa sawa na asilimia 29. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa choo katika chemba ya watumwa Mangapwani, utengenezaji wa kisima cha chini kwa chini Mangapwani, uungaji wa umeme katika chemba ya Watumwa Mangapwani, uwekaji wa nguzo za mipaka katika maeneo ya kihistoria ya Pete, Bungi, Unguja Ukuu, Chuini, Dunga na Shakani. Vile vile maeneo saba (7) ya kihistoria ya Mangapwani, Mnarani, Kisima cha Chini kwa Chini, Chemba ya watumwa, Bi Khole, Kuumbi na Mwana Mpambe yamepiwa na kupatiwa hati miliki. Aidha maeneo ya kihistoria ya Mkamandume na Msikiti Chooko yameendelezwa ili kuyaweka katika hali nzuri na kutumika kwa miaka mingi zaidi.
   (iii)    Uimarishaji wa Studio ya kurikodia Filamu na Muziki kwa kuipatia vifaa
  12.     Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kununua vifaa vya kurikodia muziki na filamu kwa ajili ya studio ya Rahaleo. Mradi huu katika hatua ya kwanza ulitengewa jumla ya shilingi 80,000,000/= na hadi kufikia Mei 2014 shilingi 80,000,000/= zimeingizwa sawa na asilimia100. Kazi inayoendelea ni ununuzi wa vifaa vilivyokusudiwa baada ya kufuata taratibu zote za manunuzi, vifaa hivyo ni Sony xdcamex, Camera tripods na Track dolly, Camera cran, Lens fish eye, Digital video mixer, Digital audio mixer na Power amplifier kwa ukamilishaji wa studio. Hata hivyo Wizara imeamua mradi huu kuumaliza kwa hatua zote mbili ndani ya kipindi hiki cha mwaka wa fedha
  (iv)  Mradi wa ujenzi wa vituo vya kutoa taarifa za usalama.
  13.     Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kutoa msaada wa taarifa za utalii na kusimamia masuala ya usalama yanayohusiana na utalii. Hatua mahususi ya mradi ni kujenga kituo kimoja kwa awamu ya kwanza pamoja na kufanya ununuzi wa vifaa kwa kituo hicho. Fedha zilizotengwa kwa hatua ya kwanza ni shilingi 100,000,000/= ambazo hadi kufikia Mei 2014 shilingi 30,000,000/= zimeingizwa sawa na asilimia 30. Kazi iliyofanyika hadi sasa ni uchoraji wa ramani ya kituo pamoja na kuandaa gharama za mradi, kazi inayoendelea ni uandaaji wa “software” itakayounganisha taarifa za kiusalama za utalii.
MAENEO YA VIPAUMBELE VYA KISEKTA KWA MWAKA 2014/2015
14.       Mheshimiwa Spika, Wizara imeweza kujipangia maeneo muhimu ya utekelezaji kisekta na kuwa ni vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2014/2015 vipaumbele hivyo ni kama vifuatavyo:-
SEKTA YA HABARI
15.       Mheshimiwa Spika, mambo muhimu ambayo imejipangia katika Sekta ya Habari kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ni kama yafuatayo;
         i.            Kuanzisha mitandao ya kijamii kwa ajili ya wananchi kupata habari kwa urahisi popote walipo kupitia simu na internet.
       ii.            Kutoa taaluma ya kutumia vifaa vya Teknolojia ya Utangazaji wa dijitali.
      iii.            Kuwapatia wananchi huduma bora za habari na kwa wakati kwa njia ya magazeti, redio na televisheni.
     iv.            Kuimarisha huduma za habari na mawasiliano kwa kuipatia Sekta hii vitendea kazi vikiwemo gari na mapazia ya sinema.
SEKTA YA UTAMADUNI
16.       Mheshimiwa Spika, maeneo muhimu ambayo tumejiwekea kipaumbele katika Sekta ya Utamaduni kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ni kama yafuatayo;
         i.            Kuhifadhi na kuimarisha maeneo ya kihistoria pamoja na kuyatangaza ndani na nje ya nchi.
       ii.            Kutangaza na kuendeleza Lugha ya Kiswahili kwa ufasaha na usahihi wake ndani na nje ya Zanzibar.
      iii.            Kukuza kazi za sanaa pamoja na kuendeleza matamasha na maonesho ya filamu na muziki.
     iv.            Kuwashajiisha wasanii kuitumia studio ya Rahaleo kurekodia kazi zao ili waweze kunufaika na sanaa zao.
SEKTA YA UTALII
17.    Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopewa kipaumbele katika sekta ya Utalii mwaka wa fedha 2014/2015 ni kama yafuatayo:-
         i.            Kubadilisha muelekeo wa sekta ya utalii  Zanzibar  ili iweze kuleta tija zaidi katika uchumi wa nchi.
       ii.            Kukijengea uwezo wa kitaalamu na kitaaluma Chuo cha Maendeleo ya Utalii (ZIToD) ili kutoa rasilimali watu kulingana na mahitaji ya soko la utalii.
      iii.            Kujenga mazingira bora ya Hoteli ya Bwawani ili kukidhi kiwango cha kimataifa na kuwavutia wageni wengi wa ndani na nje ya nchi.
SEKTA YA MICHEZO
18.       Mheshimiwa Spika, maeneo muhimu yaliyopewa kipaumbele katika sekta ya Michezo mwaka wa fedha 2014/2015 ni kama yafuatayo;
         i.            Kuimarisha miundombinu ya michezo iliyopo na kujenga njia ya kukimbilia katika Uwanja wa Gombani - Pemba.
       ii.            Kukamilisha mapitio ya Sera ya Michezo.
      iii.            Kuviimarisha vilabu vya michezo kwa kuvipatia mafunzo na fursa za michezo ya majaribio ili kuviwezesha kushindana katika mashindano ya kimataifa.
MWELEKEO WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
19.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo imetengewa jumla ya shilingi 15,336,575,000/=. Fedha hizo ni pamoja na miradi iliyoibuliwa kwenye maabara ya Utalii (Tourism Laboratory).  Kati ya hizo shilingi 9,371,200,000/= kwa kazi za kawaida (Tafadhali angalia kiambatisho namba 2) na shilingi 400,000,000/= kwa kazi za maendeleo. Katika kukuza Sekta ya Utalii nchini, Serikali imeanzisha Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Utalii (Tourism Development Program) ambayo imetokana na matokeo ya Maabara ya Utalii (Tourism Lab) yenye jumla ya shilingi 5,595,375,000/= inayohusisha Taasisi mbali mbali za Serikali na Sekta binafsi.
20   Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara inakadiria kukusanya mapato ya shilingi 1,718,658,000/= fedha ambazo zitaingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Pia makusanyo ya shilingi 2,236,250,000/= ambazo taasisi za Wizara hukusanya na zimeruhusiwa kutumia kwa ajili ya uendeshaji wa taasisi hizo.
MIRADI YA MAENDELEO YA WIZARA KWA MWAKA 2014/2015
21.       Mheshimiwa Spika, mbali na miradi iiliyoibuliwa na Maabara ya Utalii, ipo miradi mingine itakayotekelezwa na Wizara katika mwaka wa fedha 2014/2015. Miradi hiyo ni kama ifuatayo:
(i)         Mradi wa ujenzi wa vituo vya kutoa taarifa za usalama.  
22.       Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kutoa msaada wa taarifa za utalii na kusimamia masuala ya usalama yanayohusu utalii. Hatua mahsusi ya mradi huu ni kuendelea kujenga vituo vya kutoa taarifa za usalama kwa watalii. Mradi huu umetengewa shilingi 250,000,000/=  
 
(ii)        Uhifadhi wa sehemu za kihistoria na mambo ya kale
23.       Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kuwa na maeneo ya kihistoria yaliyo endelevu kwa vizazi vya leo na vijavyo kwa maendeleo ya nchi. Kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na uhifadhi wa mambo ya kale na sehemu za kihistoria, kukusanya na kusambaza taarifa za kiakiolojia katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba, kuweka mabango yenye taarifa katika maeneo ya kihistoria, kuwepo maeneo bora ya kihistoria na mambo ya kale. Mradi huu unategemewa kuingiziwa jumla ya shilingi 150,000,000/=
TAARIFA YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014 NA MALENGO YA MWAKA 2014/2015 KWA KILA TAASISI
24.       Mheshimiwa Spika, malengo tuliyotekeleza kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na tuliyopanga kutekeleza kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kiidara na taasisi zilizo chini ya Wizara ni kama ifuatavyo:-
IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI
25.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Idara ya Uendeshaji na Utumishi ni kusimamia shughuli zote za utawala, utumishi (rasilimali watu), maendeleo, wajibu na maslahi ya wafanyakazi wa Wizara pamoja na kusimamia udhibiti wa bajeti ya Wizara. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kujenga mazingira bora ya kazi yatakayowezesha Wizara kufanya kazi kwa ufanisi.
       ii.            Kuwaongezea ujuzi na utaalamu watendaji kwa maendeleo ya Wizara.
      iii.            Kuhakikisha kuwepo kwa mashirikiano ya uendeshaji na utawala ya Wizara.
 
 
 UTEKELEZAJI HALISI:
 26.   Mheshimiwa Spika, Idara hii imefanikiwa kutekeleza malengo yake ya mwaka wa fedha 2013/14 kama ifuatavyo.
         i.            Katika kujenga mazingira bora ya kazi Idara imesimamia na kuimarisha upatikanaji wa huduma mbali mbali za ofisi ikiwemo mawasiliano ya internet, fax na simu za ndani za ofisini, ulipaji gharama za maji, umeme, ununuzi wa mafuta na vilainishaji pamoja na vitendea kazi. Vile vile Idara imefanya matengenezo madogo madogo ya gari, kununua samani za ofisi pamoja na kuwapatia wafanyakazi stahiki zao.
      ii.            Katika kuwaongezea wafanyakazi  ujuzi, utaalamu na maarifa, Idara imegharamia masomo kwa wafanyakazi 14, wanawake (8) na wanaume (6) kati ya hao wafanyakazi  watatu (3) ni wa ngazi ya Shahada ya Pili (Master), watano (5) ni wa ngazi ya Shahada ya Kwanza, na wanne  (5) ni ngazi ya  Stashahada (Diploma) na mmoja ngazi ya Astashada. Lengo ni kuwaongezea ujuzi, maarifa na ubunifu ambao utapelekea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Mafunzo pia yametolewa kwa watendaji wa taasisi nyengine zilizomo katika wizara. (Tafadhali angalia kiambatisho namba 3).
      iii.            Katika kujenga mashirikiano ya uendeshaji na utawala, Idara imefanya tathimini ya utendaji kazi kwa Taasisi, Idara na Vitengo vilivyomo kwenye Wizara Unguja na Pemba kwa lengo la kujua mafanikio na changamoto zilizomo na kubuniwa mbinu za kukabiliana nazo ili kuimarisha ufanisi katika kazi.
27.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Idara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,099,322,218/= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 831,219,802/= sawa na asilimia 76.
 
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
28.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015,  Idara ya Uendeshaji na Utumishi imejipangia kutekeleza malengo makuu matatu ambayo ni:- Kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wenye ujuzi na utaalamu kwa kuwapatia wafanyakazi nafasi za masomo ndani na nje ya nchi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Wizara. Kuwa na mazingira bora ya kazi kwa kuipatia Wizara vitendea kazi vyenye ubora vitakayowezesha Wizara kufanya kazi kwa ufanisi. Kuwa na mashirikiano mazuri na endelevu ya Uendeshaji na Utawala kwa kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara, kushiriki katika semina na mikutano ya kitaifa na kimataifa. Katika kutekeleza malengo hayo Idara imepanga shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuendelea kuwalipia masomo yao wafanyakazi sita (6) waliopo vyuoni pamoja na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wengine watano (5) ambao wanatarajiwa kujiunga katika viwango tafauti vya masomo kama ifutavyo:- Shahada ya Kwanza fani ya Ugavi na Ununuzi mmoja (1), Shahada ya Kwanza ya Computer Science mmoja (1), Stashahada ya Material Management (1), Rasilimali Watu mmoja (1) na (1) Cheti katika Utunzaji Kumbukumbu.
       ii.            Kuwawezesha wafanyakazi sita (6) kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi katika nchi za nje.
      iii.            Kuwafanyia semina wafanyakazi wa Idara ili kupata uelewa zaidi juu ya masuala jinsia, njia za kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi, afya na usalama kazini.
     iv.            Kuandaa mafunzo kwa wafanyakazi wa Wizara kuhusiana na matoleo mapya ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Utumishi Serikalini.
      v.            Kuipatia ofisi vitendea kazi bora na vya kutosha.
29.       Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Uendeshaji na Utumishi iweze kutekeleza malengo yake katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, naomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 1,127,035,000/= kwa kazi za kawaida.
IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI
30.                   Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ni kupanga, kutayarisha, kukagua, kuratibu na kutathmini mipango ya maendeleo ya Wizara, kupitia Sera, kufanya tafiti mbali mbali na kusimamia utekelezaji wake. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara hii ilipanga kutekeleza malengo makuu yafuatayo:
         i.            Kuwa na Sera na Mipango bora ya kisekta ya Wizara kwa maendeleo ya Wizara.
       ii.            Kuimarisha maendeleo ya Wizara kupitia matokeo sahihi ya tafiti.
      iii.            Kuimarisha uwezo wa watendaji na utendaji kazi wa pamoja wa kisekta kwa maendeleo ya Wizara.
UTEKELEZAJI HALISI:
31.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Idara hii imetekeleza shughuli zifuatazo:-
      i.            Idara imeweza kuratibu mapitio ya Sera ya Michezo, Utalii na Mambo ya Kale ambazo hivi sasa matayarisho ya kukamilika kwake yanaendelea.
    ii.            Idara imewalipia wafanyakazi wake wawili mafunzo ya muda mrefu mmoja katika Shahada ya Kwanza ya Takwimu na mwengine Shahada ya Pili ya Usimamizi wa Miradi. Vile vile Idara imewalipia wafanyakazi wawili waliohudhuria mafunzo ya muda mfupi nchini China.
   iii.            Idara imefuatilia na kutathmini Mipango na shughuli mbali mbali zinazotekelezwa ndani ya Wizara ikiwa ni pamoja na kuratibu, kutayarisha na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Kamati ya Baraza la Wawakilishi pamoja na taarifa za utekelezaji wa malengo kwenye vikao vya pamoja vya Uongozi wa Wizara na  Mh.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
  iv.            Hatua ya pili ya utafiti wa maeneo ya kihistoria inaendelea kwa uchambuzi wa taarifa zilizokusanywa zinazohusu maeneo maarufu ya kihistoria kama vile Msikiti wa Kizimkazi, Chwaka Tumbe na Kuumbi yanayotembelewa na watalii. Katika kufanya utafiti wa maendeleo ya sanaa takwimu za utafiti zilizokusanywa katika Mikoa miwili ya Unguja zimekusanywa na zimeanza kufanyiwa kufanyiwa uchambuzi
   v.            Idara imeratibu tafiti zilizofanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara kama vile utafiti wa utamaduni usioshikika na tayari umekamilika na kitabu kimeshachapishwa. Vile Idara imeratibu utafiti wa majina ya viumbe vya baharini na mazingira yao na kazi hii bado inaendelea.
32.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Idara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 157,800,000/= kwa matumizi Mengineyoyo na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 30,479,600/= sawa na asilimia 19.
 
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
33.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imepanga kutekeleza malengo makuu matatu nayo ni:- Kuwa na  Mipango bora ya kisekta na Sera kwa kutayarisha na kuzipitia Sera za Wizara. Kuwa na “data base” ya takwimu sahihi ya taarifa zinazokusanywa na Wizara. Kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi na utaalamu katika fani ya Takwimu na Teknolojia ya Habari. Katika kutekeleza malengo hayo Idara imejipangia shughuli zifuatazo:-
             i.            Kusimamia matayarisho na mapitio ya Sera na Mipango ya kisekta  kwa maendeleo ya Wizara,
           ii.            Kuimarisha maendeleo ya Wizara kupitia matokeo ya takwimu za tafiti zinazofanywa.
          iii.            Kufuatilia na kutathmini Mipango na shughuli mbali mbali zinazotekelezwa katika Wizara.
         iv.        Kuendelea kuwalipia wafanyakazi wawili (2) waliopo masomoni pamoja na kumpatia mafunzo mfanyakazi mwengine mmoja (1) ambae anatarajiwa kujiunga na masomo katika kiwango cha Shahada ya Pili.
34.       Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iweze kufanikisha malengo yake katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa ufanisi, ninaiombea jumla ya shilingi 120,305,000/= kwa matumizi Mengineyo.
OFISI KUU PEMBA:
35.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Ofisi Kuu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Pemba ni kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Wizara Kisiwani Pemba. Ofisi hii ni kiunganishi katika kuhakikisha majukumu, malengo na shughuli zote za Wizara zilizopangwa zinatekelezwa kwa upande wa Pemba. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Ofisi hii ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kuhakikisha kuwa taasisi za Wizara zinashirikiana na kutoa huduma bora kwa jamii kwa maendeleo ya Wizara kwa upande wa Pemba.
       ii.            Kujenga mazingira bora yatakayoiwezesha Ofisi Kuu Pemba kufanya kazi kwa ufanisi.
UTEKELEZAJI HALISI:
36.       Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu imefanikiwa kutekeleza malengo yake kama ifuatavyo:-
         i.            Ofisi imeratibu utayarishaji wa vipindi 36 ambavyo vilihusisha hatua za maendeleo kisiwani Pemba ambapo wananchi walishiriki kutoa maoni yao juu ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa.
       ii.            Ofisi Kuu imeratibu shughuli za uendelezaji wa maeneo ya kihistoria ya Mkamandume na Msikiti Chooko ili kuyaweka katika hali nzuri na kutumika kwa miaka mingi zaidi.
      iii.            Ofisi Kuu imeratibu shughuli za uendelezaji wa Sekta ya Utalii kwa lengo la kuhimiza dhana ya utalii kwa wote ambapo kamati za utalii za Wilaya zimeanzishwa ili kuhakikisha utalii unaendelezwa kwa maendeleo ya nchi.
     iv.            Ofisi Kuu imeratibu matengenezo ya Uwanja wa Michezo Gombani kwa kuezua na kuezeka paa pamoja na kuendelea kuupaka rangi ili kuuweka katika hali nzuri.
      v.            Ofisi Kuu Pemba imeratibu ujenzi wa Jengo la Judo katika Uwanja wa Gombani Pemba kwa kushirikiana na Ubalozi wa Japan na Chama cha Judo Zanzibar, ambalo tayari limekamilika na kufunguliwa rasmi.
37.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Ofisi Kuu Pemba iliidhinishiwa jumla ya shilingi 672,624,750/= kwa kazi za kawaida na shilingi 100,000,000/= kwa kazi za maendeleo na hadi kufikia Mei  2014 imefanikiwa kupata shilingi 468,645,750/= sawa na asilimia 70 kwa kazi za kawaida na shilingi 90,000,000/= sawa na asilimia 90 kwa kazi za maendeleo .
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
38.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Ofisi hii imepanga kutekeleza malengo matatu nayo ni:- Kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi na utaalamu kwa kuwapatia wafanyakazi nafasi za masomo ndani na nje ya nchi. Kuwa na Mipango bora ya kisekta na Sera kwa kutayarisha na kupitia Sera za Wizara, kuwa na “data base” ya takwimu sahihi ya taarifa zinazokusanywa na Wizara. Kuwa na mashirikiano mazuri na taasisi za Wizara za Pemba kwa kutoa huduma bora na kujenga mazingira bora yatakayoiwezesha Ofisi Kuu Pemba kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Katika kutekeleza malengo Ofisi Kuu imejipangia shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuwajengea uwezo wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo wafanyakazi (6) katika kada mbali mbali na Kuimarisha mazingira bora ya wafanyakazi.
       ii.            Kuratibu na kufuatalia utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na taasisi za Wizara zilizo chini ya Ofisi Kuu Pemba zikiwemo za uwekaji wa njia ya kukimbilia (Running Track) katika Uwanja wa Gombani na kufanya matengenezo madogo madogo ya Ofisi Kuu na Uwanja wa Gombani.
39.       Mheshimiwa Spika, ili  Ofisi  Kuu ya Wizara  ya Habari,Utamaduni, Utalii na Michezo Pemba iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, naomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 1,278,161,000/= kwa kazi za kawaida.
SEKTA YA HABARI
40.       Mheshimiwa Spika, Sekta ya Habari imeundwa na taasisi tano ambazo ni Shirika la Utangazaji Zanzibar, Idara ya Habari Maelezo, Shirika la Magazeti ya Serikali, Tume ya Utangazaji, Kampuni ya Uunganishaji wa Maudhui (ZMUX) na Chuo cha Uandishi wa Habari. Majukumu ya msingi ya taasisi hizi ni kuarifu, kuelimisha na kuburudisha jamii, kuratibu uchapishaji wa magazeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kusimamia vyombo vya utangazaji vya Serikali na vya binafsi na kutoa taaluma kwa waandishi wa habari.
SHIRIKA LA UTANGAZAJI
41.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Shirika ni kutoa habari, kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha jamii juu ya masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 Shirika hili lilijipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kutayarisha vipindi vyenye kuvutia wasikilizaji na watazamaji wengi wa ndani na nje ya Zanzibar.
       ii.            Kujenga mazingira bora ya kazi ili kuliwezesha Shirika kutoa huduma bora na zenye ufanisi.
UTEKELEZAJI HALISI:
42.       Mheshimiwa Spika, Shirika la Utangazaji limefanikiwa kutekeleza malengo hayo kama ifuatavyo:-
         i.            Shirika limesimamia shughuli zake za kila siku za uendeshaji kwa kuipatia studio vifaa vikiwemo kamera, dv recoder, kompyuta za lap top pamoja na matengenezo ya studio kwa Unguja na Pemba.
       ii.            Katika kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shirika limeandaa na kurusha hewani vipindi 450 vinavyoelezea maendeleo na mafanikio yaliyofikiwa tokea kuasisiwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar. Vile vile vipindi maalumu 20 vya kupinga unyanyasaji, vipindi 119 vya kutangaza dhana ya utalii kwa wote na vipindi 101 vyevye kuelezea mafanikio ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika kuleta maendeleo.
      iii.            Shirika limewapatia mafunzo wafanyakazi wake wanne (4) ngazi ya Shahada ya Pili na mafunzo ya muda mfupi ya Habari wafanyakazi 10 nchini China.
     iv.            Shirika limewapatia watendaji wake mafunzo ya utayarishaji wa vipindi vya redio na televisheni vinavyolingana na nadharia vya vyombo vya habari vya umma yaliyoendeshwa na Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW). Vile vile Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW) limetoa mafunzo ya Uongozi wa Shirika kwa watendaji mbali mbali wa ZBC.
      v.            Shirika limeanza kazi ya ujenzi wa studio mbili za dijitali, moja Karume House na nyengine Mkoroshoni Pemba.
43.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Shirika la Utangazaji liliidhinishiwa jumla ya shilingi 2,050,000,000 /= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 1,607,749,741/= sawa na asilimia 78. Shirika lilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 280,000,000/= na kufanikiwa kukusanya shilingi 227,101,390/= sawa na asilimia 81. 
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
44.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Shirika la Utangazaji limepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni:- Kuwa na mazingira bora ya upatikanaji wa habari kwa jamii kwa kuongeza ujuzi na utaalamu kwa watendaji wa vyombo vya habari na kuwapatia huduma muhimu wafanyakazi pamoja na kuwapatia vitendea kazi. Kuhakikisha vyombo vya habari vinatoa taarifa zilizo bora kwa kuandaa vipindi vitakavyovutia jamii na kujenga uhusiano mzuri wa kitaifa na kimataifa kuhusiana na masuala ya habari. Katika kutekeleza malengo hayo Shirika limejipangia shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuwapatia mafunzo watendaji 10  wa vyombo vya habari katika kuwaongezea ujuzi na utaalamu katika fani ya Ufundi, Utayarishaji Habari na Teknolojia ya Habari.
       ii.            Kuandaa vipindi vipya na kuviimarisha vilivyopo ili kuwa na matangazo bora kwa wasikilizaji na watazamaji.
      iii.            Kutoa taarifa sahihi na kwa wakati pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vitendea kazi vilivyo bora kwa ajili ya kuondoa matatizo ya upokeaji habari.
     iv.            Kuendeleza mahusiano na wadau mbali mbali wa sekta ya habari.
      v.            Kuanzisha mitandao ya kijamii na kukamilisha muundo wa Shirika.
     vi.            Kuweka utaratibu wa vipindi vya redio kupitia kwa msambazaji wa maudhui (ZMUX).
   vii.            Kumalizia ujenzi wa studio mbili za dijitali Unguja na Pemba.
45.       Mheshimiwa Spika, ili Shirika la Utangazaji liweze kutekeleza malengo yake iliyojipangia katika mwaka wa fedha 2014/2015, naliombea liidhinishiwe jumla ya shilingi 1,814,536,000/= kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida na kukusanya shilingi 300,000,000/=.
IDARA YA HABARI MAELEZO
46.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Idara ya Habari Maelezo ni kutoa elimu kwa maendeleo mijini na vijijini, kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Serikali na taasisi mbali mbali za ndani na nje ya nchi, kutayarisha na kutoa vielelezo katika mfumo wa picha, sinema na majarida kuhusu shughuli za Serikali na kusimamia Sheria ya Habari Zanzibar.
47.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara hii ilipanga kutekeleza malengo makuu yafuatayo:-
         i.            Kuandaa na kuratibu mikutano ya waandishi wa habari kuhusiana na matukio mbali mbali Unguja na Pemba.
       ii.            Kuonesha sinema katika vijiji 18 Unguja na 12 Pemba.
      iii.            Kuweka picha za matukio muhimu kwenye mabango (Display Boards).
     iv.            Kufanya machapisho na ununuzi wa picha za viongozi wa kitaifa-Rais Kikwete 300 na Marehemu Mwalimu Nyerere 54.
      v.            Kuifanyia marekebisho ya Sheria namba 5 ya Usajili wa Magazeti na Vijarida ya mwaka 1988.
UTEKELEZAJI HALISI:
48.       Mheshimiwa Spika, Idara ya Habari Maelezo imefanikiwa kutekeleza malengo hayo kama ifuatavyo:-
         i.            Idara imefanya mikutano 40 ya waandishi wa habari ikiwemo inayohusiana na maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheria za umiliki wa ardhi na elimu juu ya maambukizi ya ukimwi.
       ii.            Maonesho ya sinema yamefanyika katika vijiji 50 kuhusu elimu juu ya maradhi yasioambukiza yakiwemo kisukari, kansa na sindikizo la damu.
      iii.            Aidha Idara imeweka picha katika mabango yake yaliyopo Unguja na Pemba, pamoja na kusambaza taarifa na matukio muhimu katika Blog na ofisi za mabalozi wa Tanzania zilizopo nje ya nchi.
     iv.            Idara imekamilisha kuifanyia marekebisho Sheria Na 5 ya Usajili wa Magazeti na Vijarida ya mwaka 1988 baada ya kufanya mikutano kadhaa na wadau wa habari kwa kutoa maoni yao juu ya marekebisho ya Sheria hiyo. Marekebisho hayo sasa yanaandaliwa kuwa mswada wa sheria ambao utawasilishwa katika ngazi zinazohusika.
49.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Idara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 378,912,301/= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 216,317,830/= sawa na asilimia 57. Idara ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 18,000,000/= na kufanikiwa kukusanya shilingi 5,645,000/= sawa na asilimia 31.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
50.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Idara ya Habari Maelezo imepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni:- Kuhakikisha wananchi wanapata taarifa muhimu kupitia njia za habari na mawasiliano, kusambaza taarifa katika ofisi za kibalozi, Blog na vyombo vya habari vya Serikali na binafsi na kuonesha sinema katika vijiji vya Unguja na Pemba. Kuwa na mazingira bora ya kazi kwa kuipatia ofisi vifaa vya kisasa vya kuhifadhia kumbukumbu, kufanya matengenezo ya jengo la ofisi na kuongeza ujuzi na utaalamu kwa wafanyakazi. Katika kutekeleza malengo hayo Idara imejipangia shughuli zifuatazo:-
         i.            Kutoa taarifa katika ofisi za kibalozi, Blog na Vyombo vya Habari.
       ii.            Kuonesha sinema katika vijiji 100 vya Unguja na Pemba.
      iii.            Kuweka mapazia matatu ya kieletroniki katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu kwa ajili ya kuonesha picha za maendeleo. Mapazia hayo mawili kwa Unguja na moja Pemba.
     iv.            Kuimarisha Idara kwa kuipatia vifaa vya kisasa ikiwa ni pamoja kununua mapazia ya kuoneshea sinema mjini na vijijini.
      v.            Kuwapatia mafunzo watendaji wa vyombo vya habari katika kuwaongezea ujuzi na utaalamu.
     vi.            Kuwasilisha Rasimu ya marekebisho ya Sheria  namba 5 ya vijarida na magazeti ya mwaka 1988 katika ngazi husika na baadae katika  baraza lako Tukufu..
 
51.    Mheshimiwa Spika, ili kukamilisha vyema malengo ya Idara ya Habari Maelezo katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, naomba kuidhinishwa jumla ya shilingi 380,828,000/= kwa kazi za kawaida na kukusanya shillingi 19,000,000/=.
 
 
 
 SHIRIKA LA MAGAZETI YA SERIKALI
52.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Shirika la Magazeti ya Serikali ni kusimamia uchapishaji wa magazeti ya Serikali ya Zanzibar, kuelimisha wananchi ili kukuza uelewa wao wa mambo, kutoa habari zenye kuhamasisha jamii na kushiriki kwenye harakati za maendeleo ya nchi.  Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Shirika la Magazeti ya Serikali lilipanga kutekeleza shughuli zifuatazo:
         i.            Kuchapisha magazeti ya kila siku.
       ii.            Kuchapisha magazeti ya kila wiki.
      iii.            Kusafirisha na kusambaza  magazeti ndani na nje ya Zanzibar
     iv.            Kufuatilia upatikanaji wa habari ndani na nje ya nchi pamoja na masoko mapya.
      v.            Kufanya malipo ya ‘hosting’ ya tovuti (website).
UTEKELEZAJI HALISI:
 
53.       Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Baraza lako kuwa, Shirika limeweza kutekeleza kwa kiasi kikubwa shughuli zake kwa mwaka 2013/2014 kama ifuatavyo:
i.        Shirika limekamilisha michoro ya ujenzi wa ofisi mpya na lipo katika hatua ya kukamilisha BoQ na “Tender document” kwa ajili ya ujenzi huo, ambao unategemewa kuanza mara zitakapopatikana fedha. Shirika la Magazeti ya Serikali linategemea kufanya ujenzi huo katika kiwanja chake kilichopo Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
ii.      Katika kuwajengea uwezo wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuongeza uzalishaji, Shirika limeweza kuwasomesha wafanyakazi wake sita (6) katika ngazi mbali mbali ndani na nje ya nchi. Wafanyakazi hao wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi na wengine wanaendelea na masomo.
iii.     Shirika limewapatia stahiki za likizo wafanyakazi wake. Pia Shirika lilimsaidia mfanyakazi wake mmoja gharama za matibabu nchini India.
iv.    Shirika lilisambaza magazeti katika Mikoa ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara.
v.     Malipo ya tovuti yamefanyika na tovuti imefunguliwa na inaitwa www.magazetismz.com
54.       Mheshimiwa Spika, Shirika linapenda kuliarifu Baraza lako kuwa, Gazeti la Zanzibar Leo limeweza kuwafikia wasomaji wengi zaidi kwa kuongeza maeneo ya usambazaji katika baadhi ya mikoa ya Tanzania bara.
55.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Shirika liliidhinishiwa jumla ya shilingi 816,000,000/= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei 2014 limefanikiwa kupata shilingi 504,459,728/=  sawa na asilimia 62. Shirika lilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 500,000,000/= na kufanikiwa kukusanya shilingi 379,677,521/= sawa na asilimia 76.
 
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
56.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Shirika la Magazeti ya Serikali limepanga kutekeleza malengo yake makuu mawili kama yafuatayo: Kuwa na magazeti yenye makala na habari za kielimu ambazo zinalenga kuondosha umasikini nchini na kuishajiisha jamii kushiriki katika mipango ya maendeleo ya nchi kwa kuchapisha na kusambaza magazeti ya kila siku na kila wiki. Kuwa na miundombinu bora ya ofisi na vitendea kazi na kuwaongezea ujuzi na uwezo wafanyakazi wa Shirika. Katika kutekeleza malengo hayo Shirika limejipangia shughuli zifuatazo:
         i.            Kufuatilia upatikanaji wa habari ndani na nje ya nchi pamoja na kufanya utafiti wa kutafuta masoko mapya ya habari.
       ii.            Kuchapisha magazeti ya kila siku na kila wiki pamoja na kusafirisha na kusambaza ndani na nje ya Zanzibar.
      iii.            Kuongeza ujuzi na utaalamu kwa watendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali.
     iv.            Kulipatia Shirika vitendea kazi bora na vya kisasa.
57.       Mheshimiwa Spika, ili Shirika la Magazeti ya Serikali liweze kutekeleza   malengo hayo, naliombea kuidhinishiwa shilingi 592,726,000/= kwa kazi za kawaida na kukusanya shilingi 500,000,000/=
 
TUME YA UTANGAZAJI
58.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Tume ya Utangazaji ni kusimamia vyombo vya utangazaji vya Serikali na vya binafsi vinavyoanzishwa nchini. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Tume ya Utangazaji ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kufuatilia ugawaji wa mawimbi na udhibiti wa utendaji wa vyombo vya utangazaji nchini.
       ii.            Kuhudhuria kongamano la kitaifa la matumizi ya mfumo wa utangazaji wa dijitali.
      iii.            Kugharamia vikao vya bodi.
UTEKELEZAJI HALISI:
59.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Tume ya Utangazaji imeweza kufanya mambo yafuatayo:
         i.            Tume imegawa mawimbi kwa redio jamii za Tumbatu na Mkoani pamoja na kuwasaidia gharama za uanzishwaji wake. Pia imegawa mawimbi kwa Redio Wananchi Fm.
       ii.            Tume imeweza kusimamia upatikanaji wa nafasi za masomo ya muda mrefu kwa watendaji wake wawili, mmoja (1) Stashahada katika fani ya Uhasibu na mwengine Stashahada ya Manunuzi.
      iii.            Imetoa mafunzo kwa wamiliki wa vyombo vya utangazaji kuhusu hatua mpya ya mfumo wa ugawaji wa mawimbi ya dijitali.
     iv.            Vikao vya Bodi vimefanyika na kupitia maombi ya kuanzisha vyombo vya utangazaji.
60.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Tume iliidhinishiwa jumla ya shilingi 187,537,951/= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 159,869,401/= sawa na asilimia 85. Tume imepangiwa kukusanya jumla ya shilingi 44,000,000/= na kufanikiwa kukusanya shilingi 46,862,960/= sawa na asilimia 107.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Tume ya Utangazaji imepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni:- Kuwa na maendeleo katika Sekta ya Utangazaji inayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa kwa kushiriki mikutano kuhusu matangazo ya teknolojia ya dijitali, kuratibu na kusimamia taratibu za utangazaji nchini kwa mujibu wa Sheria ya Utangazaji. Kuwa na mazingira bora ya kazi yatakayoiwezesha Tume kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kuipatia huduma, vifaa na kuwajengea uwezo wafanyakazi. Katika kutekeleza malengo hayo Tume imejipangia shughuli zifuatazo:-
      i.            Kufanya utafiti wa watazamaji kuhusu mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali.
    ii.            Kuanzisha mfumo wa kufuatilia na kurikodi vipindi vinavyorushwa na redio nchini (monitoring system) ili kufahamu maudhui yanayorushwa na vyombo vya utangazaji vya redo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya sheria Na 5 ya Tume ya Utangazaji.
   iii.            Kufuatilia mabadiliko ya teknolojia ya dijitali ili kuviweka vyombo vya utangazaji katika hali ya kuwa tayari katika mabadiliko yanayotokea kila mara.
  iv.            Kuwapatia mafunzo watendaji na kuipatia ofisi huduma na vitendea kazi.
62.       Mheshimiwa Spika, ili kukamilisha vyema malengo iliyojipangia Tume ya Utangazaji katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, naomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 201,499,000/= kwa kazi za kawaida na kukusanya shilingi 52,000,000/=.
KAMPUNI YA UUNGANISHAJI MAUDHUI (ZMUX)
63.  Mheshimiwa Spika, itakumbukwa katika bajeti iliyopita ya mwaka wa fedha 2013/2014 Kampuni hii ilieleza majukumu yake ya msingi yakiwemo. Kuendesha kwa ufanisi na kujitegemea kwa shughuli za kuunganisha maudhui kwa kutumia miundombinu ya dijitali na kuhakikisha Zanzibar inakwenda sambamba na mageuzi ya utangazaji yanayotokea duniani kila mara.
64.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Kampuni ya Uunganishaji Maudhui ilipanga kutekeleza mambo yafuatayo kwa fedha ambazo imekusanya.
         i.            Kuunganisha vipindi vinavyopendwa na watazamaji kupitia dijitali.
       ii.            Kusimamia zana na vifaa vilivyomo katika miundombinu ya dijitali.
      iii.            Kuwapatia wafanyakazi stahiki zao.
     iv.            Kuipatia ofisi vitendea kazi.
 
 
UTEKELEZAJI HALISI:
65.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Kampuni ya ZMUX imetekeleza shughuli zufuatazo:-
           i.            Kampuni imeimarisha huduma zake kwa kununua vifaa vya kukamatia matangazo kama vile SDI – converter, satellite dish moja (1) na decoders mbili (2) pamoja na kufanya matangazo (promotion).
         ii.            Kampuni imefanya utafiti mdogo ili kujua mahitaji ya wateja kwa lengo la kuimarisha huduma zake kwa Unguja na Pemba. Utafiti huo umebaini kwamba wateja wengi wanapendelea kuongeza chanali nyingi zaidi zikiwemo za mipira na maisha ya wanyama. Aidha, watazamaji wa Pemba wametaka kuondolewa kukatika kwa matangazo.  
        iii.            Ili kuwa na mazingira bora ya kazi na kuiwezesha Kampuni kutoa huduma bora na zenye ufanisi, Kampuni imenunua samani kwa ajili ya ofisi, vifaa vya kuandikia, malipo ya umeme kwa vituo vyake saba (7) kwa Unguja na Pemba pamoja na ununuzi wa mafuta kwa ajili ya majenereta.
66.     Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Uunganishaji Maudhui kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ilipanga kukusanya jumla ya shilingi 120,000,000/= na imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 86,000,000/= sawa na asilimia 72 hadi kufikia Mei 2014.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA WA 2014/2015
67.                Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Kampuni ya ZMUX imepanga kutekeleza malengo makuu mawili  nayo ni Kupitisha matangazo ya televisheni na redio kwenye miundo mbinu yake yanayotumia mfumo wa dijitali na kuwa na mazingira bora ya kazi ili kuiwezesha Kampuni kutoa huduma bora na zenye ufanisi.
  68.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza malengo hayo Kampuni imejipangia shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuunganisha vipindi vinavyopendwa na watazamaji kupitia mtandao wa dijitali.
       ii.            Kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za malipo, na kuongeza chanali  katika miundombinu.
      iii.            Kutunza zana na vifaa vilivyomo katika miundo mbinu ya dijitali, na kuondoa kukatika katika kwa matangazo kisiwani Pemba.
     iv.            Kuwapatia wafanyakazi stahiki zao
      v.            Kuipatia ofisi vitendea kazi.
     vi.            Kuwaongezea ujuzi na utaalamu wafanyakazi.
69.       Mheshimiwa Spika, ili Kampuni ya ZMUX iweze kutekeleza malengo yake naomba kuidhinishiwa makusanyo ya shilingi 140,000,000/= na kutumia shilingi 96,000,000/= kwa kazi za kawaida kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
CHUO CHA UANDISHI WA HABARI
70.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Chuo cha Uandishi wa Habari ni kutoa mafunzo ya taaluma ya uandishi wa habari na mawasiliano kwa ngazi ya Cheti na Diploma kwa kuzingatia matakwa ya soko la ajira sambamba na kufanya tafiti mbali mbali na kutoa ushauri unaotokana na matokeo ya tafiti hizo kwenye tasnia hiyo. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Chuo cha Uandishi wa Habari kilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kuongeza wataalamu wa fani ya Habari na Mawasiliano ya Umma yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira.
       ii.            Kuandaa mazingira bora ya kazi na kutoa huduma bora kwa wafanyakazi.
 
UTEKELEZAJI HALISI:
   71.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Chuo cha Uandishi wa Habari kimefanya shughuli zifuatazo:-
   i.            Chuo kimewapatia taaluma vijana 122 ambao wamehitimu ngazi ya Cheti na Diploma. Kati ya hao wanawake 83 na wanaume 39 ambapo ngazi ya Cheti ni 60 na Diploma 43 na 20 wanafunzi wa ngazi ya cheti cha msingi.
 ii.            Chuo kimeweza kusimamia shughuli za uendeshaji wa kila siku kwa kugharamia ununuzi wa vifaa na kuipatia huduma za ofisi, gharama za ufanyaji wa mitihani, ununuzi wa redio za kufundishia, kuajiri walimu wapya wanne na Afisa Manunuzi mmoja, kufanya mahafali ya tano ya kuwatunuku vyeti wanafunzi wa Diploma na Cheti.
iii.            Katika kusimamia upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, Chuo kimeweza kutayarisha na kuchapisha nakala 5000 za gazeti la mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na pia kushiriki katika maonesho ya Sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
iv.            Chuo kimewasomesha wafanyakazi watano kwa ngazi za Shahada ya Uzamili wawili (2) mmoja fani ya Uongozi na Utawala na mwengine fani ya Uongozi wa Fedha, Shahada ya Kwanza ya Mawasiliano ya Kimataifa mmoja (1) na Stashahada ya kawaida mmoja (1) na Shahada ya Udaktari wa Falsafa ya Mawasiliano kwa Umma mmoja (1). Aidha, wafanyakazi watatu wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi nchini China.
72.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Chuo kiliidhinishiwa jumla ya shilingi 275,000,000/= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 188,540,000/= sawa na asilimia 69. Chuo kilikadiria kukusanya jumla ya shilingi 103,153,000/= na hadi kufikia Mei 2014 shilingi 117,618,000/= zimekusanywa sawa na asilimia 114.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
73.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Chuo cha Uandishi wa Habari kimepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni Kuimarisha kiwango cha rasilimali watu katika taaluma ya habari kwa kuimarisha mtaala wa kufundishia na mafunzo kwa ajili kuongeza uwezo wa utoaji wa habari. Kuwa na mazingira mazuri ya kazi na kujifunza kwa kusimamia tafiti za wanafunzi, kutoa ushauri elekezi na kuandaa na kushiriki mijadala ya kimafunzo. Katika kutekeleza malengo hayo Chuo kimepanga shughuli zifuatazo:-
         i.         Kudahili wanafunzi wapya 100 kwa ngazi ya Cheti na Diploma.
       ii.         Kendelea kupitia mtaala wa kufundishia pamoja na  kuzipitia kanuni na miongozo mbali mbali kwa ajili ya kuifanya iwe bora zaidi
      iii.         Kutoa mafunzo kwa wafanyakazi na kufanya tathmini ya shughuli za Chuo.
     iv.            Kukuza na kuimarisha mahusiano na taasisi mbali mbali kwa kukitangaza Chuo ndani na nje ya nchi.
      v.            Kuongeza uwajibikaji kwa kuajiri walimu wapya watatu katika fani ya Mawasiliano kwa Umma, Uhusiano na Ukutubi.
     vi.            Kuliimarisha darasa la Lugha ya Kichina kwa kuanzisha programu ya muda mfupi kwa wanafunzi wa nje ya Chuo kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka China.
   vii.            Kujenga madarasa mapya ya Chuo katika eneo la Kilimani.
74.       Mheshimiwa Spika, ili kukamilisha vyema malengo ya Chuo cha Uandishi wa Habari katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, nakiombea kuidhinishiwa jumla ya shilingi 254,810,000/= kwa kazi za kawaida. Aidha, Chuo kimepanga kukusanya jumla ya shilingi 126,250,000/=.
SEKTA YA UTALII
75.       Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii inajumuisha Kamisheni ya Utalii, Chuo cha Maendeleo ya Utalii na Hoteli ya Bwawani. Taasisi hizi zimepewa jukumu la kupanga mikakati, kusimamia, kuendeleza Utalii na kuitangaza Zanzibar ili Sekta hii iende sambamba na Sera na Mikakati ya Serikali katika kufikia malengo makuu ya kuimarisha uchumi wa Taifa na kupunguza umasikini.
KAMISHENI YA UTALII
76.       Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Kamisheni ya Utalii Zanzibar ni kupanga mikakati, kuratibu, kusimamia, kuendeleza na kutangaza shughuli za Utalii ndani na nje ya nchi. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Kamisheni imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kuifanya Zanzibar kuwa kituo bora cha utalii katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.
       ii.             Kuhakikisha wananchi wengi wanashiriki katika shughuli za utalii ili kutekeleza dhana ya utalii kwa wote
      iii.             Kuiwezesha Kamisheni ya Utalii kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kujenga mazingira bora ya kazi.
 
 
UTEKELEZAJI HALISI:
77.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Kamisheni ya Utalii imetekeleza shughuli zifuatazo:-
         i.            Ofisi ya Uwanja wa Ndege imetengenezwa na kuwekewa kipoza hewa. Aidha, kwa msaada wa Kampuni ya SS Bakhresa ofisi ya Bandarini imefanyiwa matengenezo makubwa. Aidha jitihada za kupata ofisi katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere zinaendelea kufanyiwa kazi.
       ii.            Kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Kamisheni imefanya kazi ya uwekaji wa madaraja hoteli 71 zilizofikia vigezo vilivyowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika kazi hiyo, hoteli za nyota tano hoteli 16, nyota nne hoteli tisa, nyota tatu hoteli 43 na nyota mbili hoteli sita.
      iii.            Kamisheni imeandaa warsha mbili kwa watembezaji watalii pamoja na wadau wengine huko Pemba kwa lengo la kuwaelezea umuhimu wa utoaji wa taarifa sahihi za vivutio vya utalii.
     iv.            Kamisheni imeendelea kushiriki katika maonesho tofauti ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuitangaza nchi kiutalii. Maonesho hayo ni pamoja na Saba Saba mjini Dar es Salaam, Maonesho ya Siku ya Utalii mjini Mwanza, ‘World Trade Market’ London, ITB mjini Berlin, Arabian Travel Market (ATM) Dubai na INDABA Afrika ya Kusini. Lengo la kushiriki maonesho hayo ni kuitangaza Zanzibar na kuwavutia watalii wengi zaidi kutembelea nchini. Mafanikio ya maonesho hayo ni kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar ambapo Januari hadi Disemba 2013 imepokea idadi ya watalii 181,301 tofauti na mwaka 2012 ambapo ilipokea watalii 169,223. Kadhalika Zanzibar imeweza kuwaalika waandishi wa habari wa vyombo tofauti vya kimataifa kwa lengo la kutolewa taarifa za vivutio vya Zanzibar katika vyombo vya habari, magazeti na majarida ya masoko husika. Kutokana na ziara hizo Zanzibar imeendelea kuandikwa na majarida tofauti kama vile Petite Fute France, Exclusive Destination Netherland, Timeless Memories and Exceptional Destination_ Hilton World Wide Afrika Kusini. Aidha katika ushiriki huo Kamisheni imefanikiwa kuchapisha nakala 6500 za vipeperushi kwa lugha tofauti zikiwemo Kirusi (1500), Kijerumani (1500), Kichina (1500) na Kiingereza (2000).
      v.            Kamisheni imefanikiwa kushiriki katika ziara zilizofanyika nchini Seychelles na Singapore. Kufuatia ziara hizo Singapore imeahidi kuisaidia Kamisheni kuufanyia mapitio Mpango Mkuu wa Utalii Zanzibar.
     vi.            Kushiriki katika utafiti uliofanyika baina ya Kamisheni ya Utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii (T. Bara), Benki Kuu ya Tanzania, Idara ya Takwimu na Idara ya Uhamiaji kwa lengo la kubaini idadi halisi ya uingiaji na utokaji wa wageni wanaotembelea nchini. Utafiti huo sasa uko katika hatua ya uandishi wa ripoti. Aidha  utafiti uliofanyika katika kipindi cha mwaka  (2012/13) unaonesha  kuwa soko la Tanzania  bado  linategemea zaidi  bara la Ulaya na Amerika, japo kuwa kuna ongezeko la wageni  kutoka bara  la Asia na Mashariki ya Kati. Idadi ya siku za ukaazi kwa wageni bado imebaki kuwa siku 9 kwa Tanzania Bara na siku 6 kwa Zanzibar.
   vii.            Mafunzo ya wajumbe wa Kamati za Utalii za Wilaya yametolewa kwa ajili ya kuwawezesha kufahamu wajibu na majukumu yao kulingana na sheria.
  viii.            Katika kuhakikisha wananchi wanashiriki katika utalii kupitia mpango wa utalii kwa wote, Kamisheni  imeandaa na kurusha  hewani  jumla ya vipindi 36 vya utalii pamoja na kuandaa ziara za  kimafunzo  kwa wananchi  katika  maeneo ya utalii. Aidha, imeendesha mashindano ya resi za ngalawa kwa lengo la kuifufua michezo ya asili ikiwa ni sehemu ya vivutio vya utalii.
     ix.            Katika kuendeleza taaluma kwa wafanyakazi, Kamisheni imewapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi wanne (4), ngazi ya Stashahada mmoja (1), ngazi ya Shahada mmoja (1), na ngazi ya Shahada ya Pili wawili (2). Vile vile wafanyakazi wanne wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi, watatu (3) nchini China na mmoja (1) nchini Uholanzi.
78.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Kamisheni iliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,628,003,000/= kwa kazi za kawaida na shilingi 100,000,000/= kwa kazi za maendeleo na hadi kufikia Mei, 2014 imefanikiwa kupata shilingi 861,043,086/= sawa na asilimia 53 kwa kazi za kawaida na shilingi 30,000,000/= sawa na asilimia 30 kwa kazi za maendeleo. Aidha, ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 1,202,000,000/= katika Mfuko Mkuu wa Serikali na kufanikiwa kukusanya shilingi 1,354,091,365/= sawa na asilimia 113..
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
79.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Kamisheni ya Utalii imepanga kutekeleza malengo yake makuu matatu nayo ni Kuendelea kuifanya Zanzibar kuwa kituo bora cha utalii katika ukanda wa Bahari ya Hindi, kutekeleza dhana ya Utalii kwa Wote ili uwe na tija zaidi kwa wananchi na kujenga mazingira bora ya kazi yatakayoiwezesha Kamisheni ya Utalii kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Katika kutekeleza malengo hayo Kamisheni imejipangia shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuipatia ofisi zana bora za kufanyia kazi.
       ii.            Kufanya safari za kikazi kwa ajili ya kufuatilia utendaji wa kazi, utekelezaji na kuongeza mashirikiano na taasisi nyengine.
      iii.            Kushiriki katika maonesho ya matatu ya Kitaifa, manne ya Kimataifa.
     iv.            Kuendelea na utafiti wa kubaini vivutio vipya  vya utalii.
      v.            Kuandaa vipindi mbali mbali vya redio, televisheni na makala katika magazeti na kutengeneza vipeperushi
     vi.            Kutangaza Utalii kwa njia ya mtandao.
   vii.            Kuendeleza dhana ya utalii kwa wote kwa kufanya semina, makongamano kwa wananchi pamoja na taasisi za umma na za binafsi. 
  viii.            Kuziwezesha Kamati za Utalii za Wilaya kukutana na kuandaa Vikao vya Makamishna na Wadau wa Utalii.
     ix.            Kupitia Sera ya Utalii, Mpango Mkuu wa Utalii, Mpango Mkakati, Kanuni na Marekebisho ya Sheria.
      x.            Kufanya ukaguzi kwa miradi  ya utalii.
80.       Mheshimiwa Spika, ili Kamisheni iweze kutekeleza malengo yake, naiombea iidhinishiwe matumizi ya shilingi 1,389,200,000/= kwa kazi za kawaida kwa mwaka wa fedha 2014/2015. Aidha Kamisheni imepanga kukusanya shilingi 1,387,658,000/= kwa ajili ya kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2014/2015.
CHUO CHA MAENDELEO YA UTALII ZANZIBAR.
81.       Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar ni kutoa taaluma itakayowezesha kujenga rasilimali watu wenye ujuzi, utaalamu na stadi zinazohitajika na kukubalika katika viwango vya kimataifa ili kuimarisha Sekta ya Utalii Zanzibar. Katika mwaka wa fedha 2013/2014 Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar kilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
      i.            Kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuwasiliana kwa Lugha ya Kiingereza kwa kuwapatia moduli za kusomea stadi za mawasiliano katika shughuli za utalii (English for Hospitality and Tourism Level I & II).
    ii.            Kutangaza dhana ya utalii kwa wote kwa kufanya mazungumzo na vijana wa kizanzibari na kuwashajiisha kujiunga na Chuo kwa kuwaonesha shughuli mbali mbali  zinazofanywa na Chuo katika Skuli tisa (9) za Wilaya tisa (9) za Unguja na Pemba.
   iii.            Kuwajengea uwezo walimu kwa kuinua viwango vyao vya taaluma, mmoja Shahada ya Kwanza fani ya Utalii na Usafiri, watatu Stashahada fani ya Utalii, Ukarimu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
 
UTEKELEZAJI HALISI:
82.       Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 Chuo cha Maendeleo ya Utalii kimeweza kutekeleza yafuatayo:
         i.            Chuo kimewapatia wanafunzi moduli za kusomea stadi za mawasiliano katika shughuli za Utalii (English for Hospitality and Tourism level I & II).  Moduli nane (8) za level I na  level  II zimepatikana na bado ununuzi huo utaendelea kufanyika kadiri fedha zitakapopatikana katika makusanyo ya Chuo.
       ii.            Katika kutekeleza dhana ya utalii kwa wote, Chuo kimefanya mazungumzo na wanafunzi wa skuli za sekondari Unguja na Pemba kwa lengo la kuwashajiisha kujiunga na Chuo ili waweze kufaidika na utalii. Utekelezaji wa kazi hiyo ulifanywa katika Skuli 8 za wilaya nane (8) za Unguja na Pemba, ambazo ni Micheweni, Gando, Uweleni na Shamiani kwa Pemba na skuli za  Bububu, Mkwajuni, Uzini na Fumba kwa Unguja. Chuo kitaendelea na kazi hiyo kwa skuli nyengine zikiwemo za wilaya mbili zilizobaki za Unguja.
      iii.            Ili kuinua viwango vya elimu vya wakufunzi,  Chuo kimesomesha  mwalimu  mmoja Shahada ya Kwanza fani ya Utalii na Usafiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini  Kenya,  walimu wawili  Stashahada katika  fani ya Utalii na Ukarimu na mwalimu  mmoja Stashahada fani ya Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Uhasibu.
     iv.            Katika kutoa taaluma bora ya Utalii nchini, kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014. Chuo kilitoa wahitimu 163 kati ya hao Stashahada 53, wanawake 30 na wanaume 23 na kwa ngazi ya Cheti 110, wanawake 73 na wanaume 37.
      v.            Chuo kimetiliana saini hati ya ushirikiano baina yake na Chuo cha Utalii cha Nairobi-Kenya (KUC) kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na taaluma.
83.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Chuo kiliidhinishiwa jumla ya shilingi 423,479,359/= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei, 2014 imefanikiwa kupata shilingi 336,627,307/= sawa na asilimia 79. Chuo kilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 280,000,000/= na kufanikiwa kukusanya shilingi 316,496,350/= sawa na asilimia 113.
 
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
84.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Chuo cha Maendeleo ya Utalii kimepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni: Kuendeleza upatikanaji wa rasilimali watu watakaoweza kutoa huduma bora zenye viwango katika shughuli za utalii. Kuandaa mazingira bora ya kazi, ufundishaji na usomaji kwa kuimarisha shughuli za taaluma pamoja na kuwajengea uwezo wakufunzi na wafanyakazi. Katika kutekeleza malengo hayo Chuo kimepanga shughuli zifuatazo:-
         i.            Kudahili wanafunzi wapya 300, wakiwemo Stashahada 60 na 240 wa ngazi ya Cheti.
       ii.            Kuimarisha shughuli za taaluma ikiwemo  mitihani, kuongeza vipindi vya mafunzo ya vitendo (practical sessions), kuchapisha vyeti vya wahitimu 203 na kutunuku vyeti na stashahada kwa wahitimu 203,wanaume 148 na wanawake 57.
      iii.             Kuendelea kuwapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi sita wakiwemo mmoja ngazi ya shahada ya kwanza fani ya Utalii na Usafiri, mmoja ngazi ya stashahada fani ya Uongozi wa shughuli za Utalii na Ukarimu, mmoja ngazi ya stashahada fani ya Mapishi (Culinary Arts) na wafanyakazi  watatu – mmoja ngazi ya cheti fani ya Utunzaji kumbukumbu, mmoja ngazi ya cheti fani ya Mahusiano ya Umma na mmoja ngazi ya shahada ya pili fani ya Uongozi wa Fedha.
     iv.            Kuzipatia ofisi vitendea kazi kwa mujibu wa mahitaji.
      v.            Kutoa  mwamko  wa utalii kwa wote kwa wanafunzi wa skuli za sekondari kwa kuonesha shughuli zinazofanywa na Chuo cha Maendeleo ya Utalii ili kuwashajiisha kujiunga na Chuo.
     vi.            Kufanya mikutano miwili na wawekezaji wa hoteli za kitalii na taasisi nyengine zinazotoa huduma za kitalii.
   vii.            Kukusanya taarifa za uchambuzi wa hali halisi (situation analysis) kuangalia uwezekano wa kufungua tawi la Chuo Pemba.
85.       Mheshimiwa Spika, Ili Chuo kiweze kutekeleza malengo yake, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha matumizi ya shilingi 419,029,000/= kwa kazi za kawaida na kukusanya shilingi 360,000,000/=.
HOTELI YA BWAWANI
86.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Hoteli ya Bwawani ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kupokea idadi kubwa ya wageni katika Hoteli ya Bwawani.
       ii.            Kutoa huduma bora kwa wateja wa kitaifa na kimataifa.
UTEKELEZAJI HALISI:
         i.            Katika kuitangaza Hoteli vipeperushi 15,000 vya matangazo vya kuweka vyumbani vimechapishwa, kutayarishwa kadi za maoni 2,500 zinazojazwa na wageni na kutayarisha bango la matangazo. Vile vile vipindi 32 vimetayarishwa na kuoneshwa.
       ii.            Huduma za upatikanaji wa maji katika maeneo ya hoteli zimeimarishwa kwa kufunga mashine tano za kusukumia maji, kuimarisha miundombinu ya umeme pamoja na kufanyia matengenezo mashine za kufulia, kupigia pasi na kuimarisha huduma za jikoni.
      iii.            Ofisi ya mapokezi imeimarishwa kwa kutoa mafunzo maalum ya uwekaji takwimu za wageni wanaopokelewa hotelini na kuweka kompyuta maalum inayoweka takwimu hizo.
     iv.            Matengenezo ya vyumba 32 yamefanyika, kati ya hivyo, vyumba 26 matengenezo madogo madogo na vyumba 6 matengenezo makubwa, pamoja na matengenezo ya hita 10 za vyumba vya wageni. Aidha ukumbi wa Salama umefanyiwa matengenezo kwa kuwekwa vipoza hewa viwili, seti moja ya mapazia na zulia sehemu ya wageni mashuhuri.
      v.            Hoteli imeendelea kuwalipia ada ya masomo wafanyakazi wake 12 katika fani ya utunzaji nyumba wawili, Chakula na Vinywaji wawili, manunuzi mmoja, mapokezi mmoja, mapishi wawili, uongozi wa shughuli za utalii na ukarimu watatu na rasilimali watu mmoja.  
87.       Mheshimiwa Spika, Hoteli ya Bwawani kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Ilipanga kukusanya jumla ya shilingi 950,000,000/= na imefanikiwa kukusanya shilingi 850,154,351/= sawa asilimia 89 hadi Mei 2014.
 
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
                88.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Hoteli ya Bwawani imepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni:- Kuwa na idadi kubwa ya wageni kwa kuitangaza hoteli kwa njia ya  mtandao, vipeperushi na vipindi vya televisheni na redio, kutoa huduma bora kwa wateja wa kitaifa na kimataifa pamoja na kuanzisha “internet café”, kuweka takwimu sahihi za wageni wanaoingia na kutoka na kuimarisha mazingira ya hoteli. Kuwa na mazingira bora ya kazi kwa kuwaendeleza wafanyakazi kitaaluma katika fani ya Hoteli na kuipatia Hoteli vitendea kazi vitakavyowezesha Hoteli kufanya kazi kwa ufanisi. Katika kutekeleza malengo hayo Hoteli imejipangia shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuitangaza Hoteli kwa njia ya mtandao, vipeperushi na  kuandaa vipindi vya televisheni na redio kwa lengo la kuongeza idadi ya wageni.
       ii.            Kuipatia Hoteli huduma ya “internet café”.
      iii.            Kufanya ukarabati wa maeneo ya Hoteli vikiwemo vyumba na kumbi
     iv.            Kuwapatia wafanyakazi mafunzo na kuipatia Hoteli vitendea kazi vyenye ubora.
 
89.       Mheshimiwa Spika, ili Hoteli iweze kutekeleza malengo yake itahitaji kuidhinishiwa makusanyo ya shilingi 995,000,000/= na kutumia shilingi 850,000,000/= kwa kazi za kawaida kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
SEKTA YA UTAMADUNI NA MICHEZO
90.       Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utamaduni na michezo imeundwa na Kamisheni ya Utamaduni na Michezo, Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale, Baraza la Kiswahili, Baraza la Sanaa, Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonesho, na Baraza la Taifa la Michezo. Taasisi hizi zimepewa jukumu la kusimamia, kuratibu, kufufua, kuendeleza na kudumisha shughuli zote za Utamaduni na Michezo Zanzibar.
KAMISHENI YA UTAMADUNI NA MICHEZO
91.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Kamisheni ya Utamaduni na Michezo ni kuratibu na kusimamia maendeleo ya utamaduni na michezo hapa Zanzibar kwa kushirikiana na Idara na Mabaraza yaliyo chini yake. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Kamisheni ya Utamaduni na Michezo ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kuendeleza shughuli za Utamaduni na Michezo nchini.
       ii.            Kujenga mazingira bora ya kazi yenye kuleta ufanisi zaidi.
 UTEKELEZAJI HALISI:
92.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Kamisheni ya Utamaduni na Michezo imetekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kamisheni imeufanyia matengenezo Uwanja wa Amaani pamoja na kuweka nyasi bandia katika kiwanja hicho. Kazi ambayo imefanywa kwa ufanisi mkubwa na Kampuni ya Ekika ya Dar es Salaam na Viva Turf ya China.
       ii.            Katika kushajiisha wanamichezo kuwa na ari ya kushiriki katika mashindano ya kitaifa na kimataifa na kuiletea nchi ushindi na sifa, Kamisheni imewazawadia wanariadha walioshiriki katika mashindano ya Afrika ya Mashariki na Kati. Vile vile Kamisheni imegharamia Timu ya Taifa ya Zanzibar kushiriki katika mashindano ya Kombe la Chalenji yaliyofanyika nchini Uganda na kuiwezesha timu ya Chuoni kwenda kushiriki mashindano ya kombe la washindi Barani Afrika. Aidha, Kamisheni imesaidia kufanikisha mashindano ya kimataifa yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
      iii.            Kamisheni imeshiriki katika vikao vya mchakato wa kuanzishwa kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki ambayo makao makuu yake yatakuwa Zanzibar.
     iv.            Kamisheni imegharamia mafunzo ya wafanyakazi wake watano (5) kati ya hao mmoja Stashahada ya Uzamili ya Ustawi wa Jamii na watatu (3) wamejiunga na mafunzo ya Stashahada ya Rasilimali Watu na mmoja ni Shahada ya Pili ya Takwimu.
      v.            Kamisheni ilizindua kitabu cha “Urithi wa Utamaduni Usioshikika” kilichojumuisha utamaduni wa ngoma za asili na sanaa za Zanzibar. Kazi hii imefanywa na Kamisheni kwa kushirikiana na Shirika la UNESCO.
     vi.            Kazi ya ununuzi wa vifaa vya kurikodia sauti na picha kwa ajili ya Studio ya Muziki na Filamu inaendelea.
   vii.            Kamisheni imefanya mapitio ya Sera ya Michezo kwa kushirikisha wadau Unguja na Pemba. Hatua za kuikamilisha Sera hiyo kupitia vikao vinavyohusika zinaendelea.
  viii.            Kamisheni imeratibu matamasha yaliyofanyika Zanzibar yakiwemo Tamasha la Mwangapwani na Kojani, Tamasha la Nchi za Jahazi na Sauti za Busara.
93.       Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2013/2014. Kamisheni iliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,470,503,024/= kwa kazi za kawaida na shilingi 80,000,000/= kwa kazi za maendeleo, hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 1,178,165,048/= sawa na asilimia 80 kwa kazi za kawaida na shilingi 80,000,000/= sawa na asilimia 100 kwa kazi za maendeleo.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
94.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Kamisheni ya Utamaduni na Michezo imepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni:- Kuwa na maendeleo ya  Utamaduni na Michezo kwa kuanzisha Programu ya Bonanza za Utamaduni na Michezo, kuwezesha ushiriki wa timu katika mashindano ya kitaifa na kimataifa, kuendeleza Nyumba ya Sanaa na kufanya tafiti za utamaduni.  Kuwa na mazingira bora ya kazi kwa kuwapatia wafanyakazi nafasi za masomo na kuipatia ofisi vitendea kazi ili kuleta ufanisi zaidi. Katika kutekeleza malengo hayo Kamisheni imepanga shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuratibu na kusimamia ushiriki wa timu katika mashindano ya kitaifa na kimataifa
       ii.            Kuanzisha Programu ya Bonanza ili kuendeleza Utamaduni na Michezo katika Skuli za Unguja na Pemba na kusimamia Tamasha la Mzanzibari.
      iii.            Kuipatia nyezo za kufanyia kazi Nyumba ya Sanaa.
     iv.            Kuendeleza tafiti za Urithi wa Utamaduni Usioshikika.
      v.            Kutafuta maeneo ya kuanzisha viwanja vya michezo katika ngazi za Wilaya.
     vi.            Kukagua na kutathmini Programu za Michezo nchini.
   vii.            Kuratibu siku ya mazoezi ya viungo kitaifa.
  viii.            Kuifanyia marekebisho sheria ya Ngoma na Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonesho.
95.       Mheshimiwa Spika, ili Kamisheni ya Utamaduni na Michezo iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, naomba iidhinishiwe shilingi 901,531,000/= kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida.
IDARA YA MAKUMBUSHO NA MAMBO YA KALE.
96.       Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Idara hii ni kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza historia ya Zanzibar kwa kutumia Makumbusho, na maeneo ya kihistoria. Pia kuelimisha jamii juu ya umuhimu na faida za matumizi ya Makumbusho na Mambo ya Kale. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kuimarisha maeneo ya kihistoria ili yawe na hadhi ya kitaifa na kimataifa.
       ii.            Kuyatangaza maeneo ya kihistoria kwa manufaa ya wadau wote na maendeleo ya nchi.
      iii.            Kuandaa mazingira bora ya kazi yatakayowezesha Idara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
UTEKELEZAJI HALISI:
  97.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale imefanikiwa kutekeleza malengo yafuatayo:
         i.            Kazi za maendeleo zilizofanywa na Idara katika maeneo ya kihistoria Mangapwani ni ujenzi wa choo, uchimbaji wa kisima cha maji, na uungaji wa umeme. Shughuli nyengine zilizofanywa na Idara ni uwekaji wa nguzo za mipaka katika maeneo ya kihistoria ya Pete, Bungi, Unguja Ukuu, Chuini, Dunga na Shakani. Vile vile maeneo saba (7) ya kihistoria ya Mangapwani, Mnarani, Kisima cha Chini kwa Chini, Chemba ya Watumwa, Bi Khole, Kuumbi na Mwana Mpambe yamepimwa na kupatiwa hati miliki. Aidha maeneo ya kihistoria ya Mkamandume na Msikiti Chooko yameendelezwa ili kuyaweka katika hali nzuri.
       ii.            Idara imehifadhi eneo la Chuini kwa kulifanyia uchunguzi kutambua athari za urithi wa utamaduni na historia wa jamii zilizoishi katika eneo hilo “Cultural Heritage Impact Assessment” (CHIA).
      iii.            Idara kwa kushirikiana na watafiti kutoka Uingereza wanaendelea na kukusanya taarifa na takwimu za akiolojia   na kugundua mabaki ya historia na utamaduni katika eneo la Unguja Ukuu, Fukuchani na Kuumbi. Matokeo ya tafiti hizi zimeshatolewa, lakini taarifa zaidi za kimaabara zinaendelea kufanyiwa kazi. Vile vile taarifa za utafiti wa “geophysical research” kwa eneo la Unguja Ukuu ripoti yake tayari imeshakamilika kwa hatua za mwanzo.
     iv.            Idara imetoa mafunzo ya awali kwa viongozi wa vijiji vya Fukuchani, Mangapwani, Bungi na Mwanampambe juu ya umuhimu wa kuyatunza na kuyaendeleza maeneo ya kihistoria. Mafunzo kwa vijiji vyengine yataendelea.
      v.            Idara imekusanya taarifa za awali za maeneo matano ya kihistoria ya Pango la Kuumbi, Mwanampambe, Pango la Machaga Pete, Mwinyi Mkuu na Ras Mkumbuu kisiwani Pemba.
     vi.            Katika kuyatangaza maeneo ya kihistoria, Idara imetengeneza filamu (5) za vielelezo kwa maeneo matatu ya kihistoria ya Mangapwani, Mwanampambe na Hamam la Hamamni. Pia imetayarisha na kurusha hewani vipindi kumi na nne (14) kupitia ZBC Redio, TV na Zenj FM vyenye maudhui ya Mahusiano ya Zanzibar na Jumuiya za Kimataifa katika Karne ya 19, Historia ya Kasri ya Mfalme wa Tumbatu pamoja na Msikiti wa Jongowe, historia ya Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale kabla na baada ya Mapinduzi na vipindi sita (6) vya redio kuhusu Urithi wa Utamaduni wa Baharini. Aidha, Idara imesambaza vipeperushi vya maeneo manne (4) ya historia ya Mangapwani, Kisima cha Chini kwa Chini, Mahandaki ya Vita vya Pili vya Dunia pamoja na Mnara wa Vita, Mahodhi ya Kidichi. Pia Idara imetengeneza mabango ya matangazo kwenye maeneo ya Bandarini na Ngome Kongwe. Idara imeandika makala 12 kupitia Zanzibar Leo juu ya umuhimu wa maeneo ya kihistoria.
   vii.            Idara imekamilisha hatua za awali za kuwasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali juu ya uingizaji wa somo la uhifadhi katika mitaala ya elimu. Hatua za kuwapatia mafunzo wanafunzi zinaendelea kwa kuyatembelea maeneo ya kihistoria.
  viii.            Pia Idara imegharamia mafunzo ya wafanyakazi  kumi na tatu,  ngazi ya cheti fani ya Ukutubi (1), Stashahada  Uhifadhi wa Kumbukumbu (2), Manunuzi na Ugavi (1) Kazi za Kijamii (1), Urithi wa Utamaduni na Utalii (2), Utawala wa Umma (2) na  Mahusiano ya Kimataifa (1),Shahada ya Kwanza ya Sayansi  na Ualimu (1), Shahada ya Mawasiliano katika Uhandisi (1) na Shahada ya Uzamili ya Historia (1) 
     ix.            Idara imeshiriki maonesho ya kitaifa ya miaka 50 ya Mapinduzi na Siku ya Wafanyakazi Duniani.
98.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Idara iliidhinishiwa jumla  ya shilingi 748,209,200/= kwa kazi za kawaida na shilingi 230,000,000/= kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 404,973,500/= sawa na asilimia 54 kwa kazi za kawaida na shilingi 230,000,000/= sawa na asilimia 100 kwa kazi za maendeleo. Pia ilipangiwa kukusanya shilingi 210,000,000/= na kufanikiwa kukusanya shilingi 73,042,959/= sawa na asilimia 35 hadi kufikia Mei 2014.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
99.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale imepanga kutekeleza malengo makuu matatu nayo ni Kuwa na Makumbusho yenye ubora wa kimataifa kwa kuyaendeleza, kuyafanyia matengenezo na kuyawekea uzio ili kuhifadhi na kuendeleza Urithi wa Utamaduni na Historia nchini. Kuwa na maeneo ya kihistoria yalio endelevu kwa kuandaa mafunzo kwa viongozi wa Shehia katika kila Wilaya, kuanzisha programu zitakazowajengea wananchi mwamko juu ya umuhimu wa kuhifadhi na kulinda maeneo ya kihistoria kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini. Kuwa na mazingira bora ya kazi yatakayowezesha Idara kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuipatia vifaa muhimu vya kutendea kazi na kuwajenga wafanyakazi kielimu na kitaaluma. Katika kutekeleza malengo hayo Idara imepanga shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuyafanyia matengenezo maeneo ya kihistoria Unguja na Pemba na kuyawekea uzio Vitongoji na Ole Mandani.
       ii.            Kuanzisha programu zitakazowajengea wananchi muamko wa kulinda, kuhifadhi na kutunza maeneo ya kihistoria kupitia sinema, kufanya semina za wadau, vipindi vya televisheni na redio na filamu.
      iii.            Kuwapatia mafunzo masheha na Madiwani katika kila Wilaya.
     iv.            Kufanya utafiti wa maeneo ya kihistoria kwa ajili ya maendeleo ya utalii.
      v.            Kuendeleza Makumbusho ya Mnazimmoja ili kutoa huduma bora.
     vi.            Kushiriki katika matamasha ya kitaifa na kimataifa.
   vii.            Kuandaa mazingira bora ya kazi kwa wafanyakazi wake.
100.    Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Makumbusho iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015 naomba kuidhinishiwa matumizi ya shilingi 718,440,000/= kwa kazi za kawaida na shilingi 150,000,000/= kwa kazi za maendeleo. Aidha Idara imepanga kukusanya shilingi 210,000,000/=.
BARAZA LA KISWAHILI LA ZANZIBAR:
101.    Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Baraza la Kiswahili la Zanzibar ni kukuza, kushajiisha na kufuatilia matumizi na maendeleo ya Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza hili lilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kukuza na kuendeleza matumizi ya Kiswahili sahihi na fasaha kitaifa na kimataifa.
       ii.            Kuweka mazingira mazuri ya ofisi kwa kuipatia vifaa bora na vya kisasa.       
UTEKELEZAJI HALISI
102.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza la Kiswahili limetekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Katika kutoa taaluma kwa umma kuhusu matumizi ya Kiswahili fasaha, Baraza limetayarisha na kurusha vipindi 24 vya “Kiswahili Lugha Yetu” kupitia ZBC TV na Redio na vipindi sita (6) kupitia “Hits FM Redio” kwenye kipindi cha “Kasha la Kiswahili”. Baraza limechapisha jarida la “BAKIZA” toleo namba mbili, Kitabu cha Mawasiliano ya Misingi ya Kiswahili kwa Wageni na vitabu vidogo vidogo vya lugha tatu (Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa) na vipeperushi kwa ajili ya kuyasambaza ndani na nje ya nchi.
       ii.            Baraza linaendelea na kazi ya utafiti wa majina ya viumbe vya baharini na mazingira yao kwa lengo la kuandika kamusi ambapo kukamilika kwake kutasaidia kuhifadhi msamiati na kutoa fursa kwa watumiaji wa lugha, watafiti na wanaojifunza Kiswahili kuyaelewa majina hayo na kuyatumia ipasavyo.
      iii.            Baraza limegharamia mafunzo ya muda mrefu kwa watendaji wake watatu, kati ya hao mmoja (1) ni Shahada ya Pili ya Fasihi ya Lugha na wawili ni Diploma ya Usimamizi wa Fedha.
     iv.            Katika kuadhimisha siku ya Kiswahili Zanzibar, mashindano ya uandishi wa insha katika ngazi za Wilaya yamefanyika kwa skuli 33 za Serikali na binafsi Unguja na Pemba. 
      v.            Maktaba ya BAKIZA imeimarishwa kwa kuongezwa vitabu na majarida jambo ambalo limepelekea kuongezeka idadi ya watumiaji.
103.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Baraza la Kiswahili liliidhinishiwa jumla ya shilingi 76,900,000/= kwa matumizi ya Mengineyo na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 9,000,000/= sawa na asilimia 12. Baraza lilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 41,580,000/= na kufanikiwa kupata shilingi 1,038,000/= sawa na asilimia 2.  
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
104.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Baraza la Kiswahili limepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni Kukuza, kuendeleza na kutangaza matumizi ya Kiswahili sahihi na fasaha kitaifa na kimataifa na Kuwa na mazingira mazuri ya kazi kwa kuipatia ofisi vitendea kazi na kuwapatia wafanyakazi fursa za masomo. Katika kutekeleza malengo hayo Baraza limepanga shughuli zifuatazo:-
         i.            Kuandika na kuchapisha majarida, makala na vitabu vyenye maudhui mchanganyiko na kuvisambaza ndani na nje ya nchi.
       ii.            Kukitangaza Kiswahili kupitia vyombo vya habari, machapisho na maonesho ya kitaifa na kikanda.
      iii.            Kuendelea kukusanya msamiati wa viumbe vya baharini na ule wenye mnasaba na mazingira ya baharini.
     iv.            Kufanya mashindano ya uandishi wa Fani za Kiswahili utakaoshirikisha waandishi chipukizi na wanafunzi wa sekondari na kutambua michango ya watu na taasisi zinazoendeleza Kiswahili katika kuadhimisha Siku ya Kiswahili Zanzibar.
105.    Mheshimiwa  Spika, ili  Baraza  la  Kiswahili  Zanzibar liweze kutekeleza malengo yake ipasavyo, naomba liidhinishiwe shilingi 40,800,000/= kwa ajili ya matumizi Mengineyo na kuchangia shilingi 40,000,000/= kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.  
BODI YA SENSA YA FILAMU NA SANAA ZA MAONESHO
106.    Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonesho ni kukagua na kuhakiki filamu na sanaa za maonesho ili kuhakikisha kuwa haziharibu maadili ya jamii zinapooneshwa hadharani na kusikika kwenye vyombo vya habari na rekodi (CD,DVD). Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Bodi hii ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Kuongeza idadi na ubora wa filamu na Sanaa za maonesho zinazozingatia mila na silka za utamaduni wa Mzanzibari.
       ii.            Kuimarisha mazingira mazuri ya kazi na wafanyakazi pamoja na kuipatia ofisi vitendea kazi.
UTEKELEZAJI HALISI
107.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonesho imetekeleza malengo yafuatayo:-
         i.             Jumla ya vipindi vitatu (3) vilitayarishwa na kurushwa kwenye vyombo vya habari vya Shirika la Utangazaji la ZBC pamoja na kuandaa mikutano na wasanii kwa lengo la kuwaelimisha ubora wa sanaa zao katika kulinda maadili.
       ii.            Bodi imeendelea na uhakiki na ukaguzi wa filamu na kazi za sanaa mbali mbali zikiwemo matamasha mawili ya Tamasha la Jahazi Literary lililovishirikisha jumla ya vikundi tisa (9) kutoka mataifa mbali mbali ya nje ya nchi na Tamasha la Sauti za Busara ambalo lilivishirikisha jumla ya vikundi 38 navyo kutoka mataifa mbali mbali wakiwemo wenyeji Zanzibar. Uhakiki ulifanyika kwa filamu za michezo mchanganyiko na vikundi vya sanaa za maigizo Zanzibar ili kuhakikisha hazendi kinyume na maadili ya Zanzibar (Tafadhali angalia kiambatisho namba 4)
      iii.            Katika kuendeleza mikakati  ya ukaguzi ili kuweka mazingira yatakayoiokoa  jamii  na  wimbi  la  mmong’onyoko  wa  maadili kupitia fani ya sanaa, Bodi  ilifanya  kikao kimoja na watendaji wa Bodi ya Filamu ya Tanzania kwa lengo la kurahisisha  utendaji wa pamoja. Maamuzi yaliyofikiwa katika vikao hivyo yameanza kutekelezwa. Pia imetengeneza vipeperushu vyenye kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa maadili pamoja na matayarisho ya msingi ya matangazo mafupi ya elimu yatakayotumika kwenye vyombo vya habari na maeneo mbali mbali nchini.
     iv.            Filamu maalumu ya kutoa elimu juu ya usimamizi na uendelezaji wa maadili imetayarishwa na itaanza kuoneshwa hivi karibuni katika shehia mbali mbali za Unguja na Pemba.
108.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014. Bodi iliidhinishiwa jumla ya shilingi 38,000,000/= kwa matumizi Mengineyo na hadi kufikia Mei, 2014 imefanikiwa kupata shilingi 8,000,000/= sawa na asilimia 21.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
109.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonesho imepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni Kuwa na kazi za sanaa zilizo bora zenye kuzingatia mila, silka na utamaduni wa Kizanzibari. Kuwa na   mazingira  bora  ya kutendea  kazi  kwa  kuwajengea  uwezo wafanyakazi na kuipatia ofisi vitendea kazi muhimu. Katika kutekeleza malengo hayo Bodi imejipangia shughuli zifuatazo:-
      i.            Kukagua filamu na sanaa zinazooneshwa hadharani ili kuhakikisha zinaendana na maadili ya Kizanzibari.
    ii.            Kuandaa vikao viwili kwa vikundi vya sanaa katika kuwajengea uelewa juu ya kutayarisha kazi zinazoendana na maadili ya Kizanzibari.
   iii.            Kuratibu maendeleo ya sanaa na utamaduni wa Mzanzibari kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ndani na nje ya Zanzibar.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                           
110.    Mheshimiwa Spika, ili Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonesho iweze kukamilisha shughuli zake, naiombea shilingi 21,500,000/= kwa ajili ya matumizi Mengineyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.
BARAZA LA SANAA ZANZIBAR
111.    Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Baraza la Sanaa Zanzibar ni kusimamia na kuratibu maendeleo ya shughuli za sanaa Zanzibar. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza la Sanaa lilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:
         i.            Kuwafanya wananchi wengi kushiriki na kutekeleza shughuli za sanaa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
       ii.            Kuimarisha mazingira ya kazi yatakayowezesha Baraza kufanya kazi zake kwa ubora na ufanisi zaidi.
UTEKELEZAJI HALISI:
112.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza la Sanaa limetekeleza shughuli zifuatazo:-
         i.            Baraza limewahamasisha wasanii kwa kuwapatia taaluma ya utengenezaji wa bidhaa bora ili kuweza kupata soko kubwa zaidi ndani na nje ya nchi. Pamoja na kurusha hewani vipindi 6 kwa ZBC Redio, ZBC – TV na “Hits FM” vinavyozungumzia mambo ya sanaa na utamaduni.
       ii.            Baraza limeshiriki kwenye maonesho na fensi ya sherehe ya miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
      iii.            Mafunzo yametolewa kwa wasanii wa fani tofauti kuhusu maradhi ya Ukimwi kwa lengo la kuwapa taaluma na njia salama za kujikinga na maambukizi ya maradhi hayo.
     iv.            Kwa kuadhimisha miaka 50 ya Muungano Baraza kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utamaduni na Michezo limeandaa mashindano ya sanaa katika fani za Ushairi, Tenzi, Taarabu Asilia, Taarab ya Kisasa, Muziki wa Dansi na Ngoma Asilia pamoja na kuwazawadia washindi.
      v.            Baraza limeshughulikia malalamiko kuhusu ghasia za muziki na matendo yasiyoridhisha katika vijiji vya Nungwi, Jambiani, Paje, Tunguu na Bwejuu na kuyapatia ufumbuzi.
     vi.            Mashindano ya sanaa za uchoraji yamefanyika ili kuibua vipaji kwa wanafunzi wa skuli za Mwanakwerekwe ‘A hadi E’ ambapo wanafunzi 180 wameshiriki.
   vii.            Utafiti kwa ajili ya kuangalia vikwazo vinavyowakabili wasanii katika kuendeleza kazi zao umefanyika kwa Wilaya mbili za Unguja. Utafiti huo umebaini kwamba vipaji vipo, vinahitaji kuendelezwa na kutafutiwa soko la bidhaa zao. Utafiti wa aina hiyo utaendelea kwa Wilaya nyengine.
113.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza liliidhinishiwa jumla ya shilingi 30,466,925/= kwa ajili ya matumizi Mengineyo na hadi kufikia Mei 2014 limefanikiwa kupata shilingi 7,000,000/= sawa na asilimia 23. Aidha Baraza la Sanaa lilikadiriwa kukusanya jumla ya shilingi 7,000,000/= na limeweza kukusanya shilingi 4,800,000/= sawa na asilimia 68 hadi kufikia Mei 2014. 
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
114.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Baraza la Sanaa limepanga kutekeleza malengo makuu mawili nayo ni Kuwa na maendeleo ya sanaa na wasanii kwa kuwafanya wananchi wengi kushiriki na kutekeleza shughuli za sanaa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kuimarisha mazingira ya kazi kwa kuipatia ofisi vitendea kazi ili kuwezesha Baraza kufanya kazi zake kwa ubora na ufanisi zaidi. Katika kutekeleza malengo hayo Baraza limejipangia shughuli zifuatazo:-
           i.            Kuendelea kuibua vipaji vya sanaa kwa watoto na vijana katika Wilaya nane za Zanzibar.
         ii.            Kuwashajiisha wasanii kuziendeleza kazi zao na kuyatumia masoko yaliyopo kujiongezea mapato. 
        iii.            Kuendelea kufanya utafiti wa maendeleo ya kazi za sanaa katika Wilaya nane zilizobakia.
115.    Mheshimiwa Spika, ili Baraza liweze kutekeleza malengo yake ipasavyo, naliombea jumla ya shilingi 20,800,000/= kwa ajili ya matumizi Mengineyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 na kukusanya shilingi 10,000,000/=.
BARAZA LA TAIFA LA MICHEZO:
116.    Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar ni kusimamia maendeleo ya michezo yote iliyosajiliwa. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza hili limepanga kutekeleza malengo yafuatayo:
         i.            Kuchangia upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa vyama 10 vya michezo.
       ii.            Kutoa mafunzo kwa walimu na waamuzi wa michezo 10 (Mpira wa Miguu, Mikono, Pete, Wavu, Meza, Kikapu, Magongo, Mchezo wa Kuogelea, Judo na Riadha).
      iii.            Kutoa zawadi kwa wanamichezo waliofanya vizuri katika michezo ya kitaifa na kimataifa.
     iv.            Kusaidia uanzishaji wa viwanja vinne (4) vya michezo katika Wilaya ya Micheweni, Mkoani, Magharibi na Kusini Unguja.
      v.            Kusaidia uendeshaji wa mashindano ya ndani kwa vyama 10 vya michezo.
     vi.            Kuandaa mashindano ya michezo ya watoto na vijana chini ya umri wa miaka 21.
   vii.            Kusimamia mashindano ya michezo ya watu wenye ulemavu.
UTEKELEZAJI HALISI
117.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza la Taifa la Michezo limefanikiwa kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.            Baraza limewapatia vifaa vya michezo vyama vya Mpira wa Pete, Mpira wa Kikapu, Karati, Mpira wa Wavu, Mpira wa Mikono, Bao, Karata, Mpira wa Meza, Chama cha  Michezo cha Viziwi na Walemavu wa Akili. Vifaa hivyo ni jezi, meza, mabao, karata, nyavu na mabusati ambavyo vilitolewa kwa kujiandaa na mashindano ya kitaifa na kimataifa. (Mashindano mbali mbali kwa timu za Zanzibar zilizoshiriki kitaifa na kimataifa angalia kiambatisho namba 5).
       ii.            Baraza kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar kwa ufadhili wa Shirika la “Save the Children” limewapatia mafunzo walimu 150 wa michezo ya mpira wa miguu. Walimu hao ni wa michezo kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na wanaofundisha timu za mitaani. Aidha kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupitia mradi wa “International Inspiration” mafunzo ya makocha wa michezo ya mpira wa wavu na riadha yametolewa.
      iii.            Katika kuhakikisha michezo inaendelea kukuwa nchini. Baraza kwa kushirikiana na Idara ya Ardhi, Mipango Miji na Vijiji wametenga maeneo ya viwanja vya michezo midogo midogo kwa Unguja na Pemba. Kwa Wilaya ya Kaskazini eneo la Nungwi limetengwa na kupimwa kwa ajili ya shughuli hizo, kwa Wilaya ya Mjini eneo la Uwanja wa Tumbaku limepimwa na kupewa hati miliki. Kwa upande wa Pemba katika eneo la Uwanja Gombani, kuna eneo limetengwa kujengwa viwanja vitakavyoweza kutumika kwa michezo midogo midogo (Multipurpose Stadium).
     iv.            Baraza kupitia Kamisheni ya Utamaduni na Michezo limewapatia zawadi wanamichezo walioshinda katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya Judo na Riadha, pamoja na washindi walioshinda katika mashindano ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
      v.            Baraza limesaidia vyama 20 vya michezo kushiriki katika mashindano ya kitaifa pamoja na kukiwezesha Chama cha Mpira wa Pete kuandaa mashindano ya ligi kuu ya Zanzibar. Aidha Baraza limegharamia Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Riadha na kupata viongozi wapya.
     vi.            Mashindano ya timu za watoto za kombaini za Wilaya 10 yamefanyika kwa kushirikiana na Kamati ya Central Taifa kwa ufadhili wa Taasisi ya Arma Promotion ya Zanzibar.
vii.                        Mashindano ya michezo ya Watu wenye Ulemavu wa uziwi yamefanyika. Aidha Baraza limeandaa utaratibu uliowezesha kupatikana fedha zilizotumika kuwapeleka wanamichezo wa Chama cha Ulemavu wa Akili kwenye mashindano yaliyofanyika Kibaha Tanzania Bara.
118.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Baraza liliidhinishiwa jumla ya shilingi 141,699,406/= kwa kazi za kawaida na hadi kufikia Mei 2014 imefanikiwa kupata shilingi 11,646,350 /= sawa na asilimia 8.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
119.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Baraza la Taifa la Michezo limepanga kutekeleza malengo makuu mawili ambayo ni kuwa na mazingira bora ya shughuli za maendeleo ya michezo na kuwa na mazingira bora ya utendaji kazi yatakayowezesha Baraza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Katika kutekeleza malengo hayo Baraza limepanga shughuli zifuatazo:-
         i.            Kutoa mafunzo kwa walimu na wa
       ii.            amuzi kwa vyama 15 vya michezo.
      iii.            Kuwapatia vifaa vya michezo vyama 15 vya michezo.
     iv.            Kushajiisha  na kuhamasisha kuandaliwa kwa mashindano ya watoto na vijana chini ya umri wa miaka 19.
      v.            Kusaidia shughuli za maendeleo ya michezo kwa watu wenye ulemavu.
     vi.            Kufanya mapitio ya Katiba za vyama vinne vya michezo ya Karati, Judo, Kuogelea na Trithlon na kusimamia kanuni zake.
120.    Mheshimiwa Spika, ili Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar liweze kutekeleza malengo yake ipasavyo, naliombea kuidhinishiwa shilingi 90,000,000/= kwa ajili ya matumizi  Mengineyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.
SHUKRANI
121.    Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu naomba kuwashukuru wote waliochangia katika kutayarisha hotuba hii. Shukurani maalumu ziwaendee Mhe. Naibu Waziri Bihindi Hamad Khamis, Katibu Mkuu Dk. Ali Saleh Mwinyikai, Naibu Katibu Mkuu Nd. Issa Mlingoti, Afisa Mdhamini Pemba, Wakurugenzi, Wakuu wengine wa Taasisi za Wizara na wasaidizi wao wote kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu mkubwa. Kwa kweli wamekuwa wakinisaidia sana kutekeleza majukumu yangu. Pia nawashukuru Wenyeviti wa Mabaraza na Bodi mbali mbali kwa kusimamia vyema taasisi zetu na kunishauri kwa hekima na busara.
122.    Mheshimiwa Spika, naomba kuwashukuru wafanyakazi, wanamichezo, wasanii, wadau wa utalii na wananchi wote wa Unguja na Pemba kwa michango yao katika kufanikisha shughuli za Wizara. 
123.    Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhila kama sikuishukuru Wizara ya Fedha pamoja Tume ya Mipango kwa ushirikiano mkubwa waliotupa kwa mahitaji ya fedha na ushauri.
124.    Mheshimiwa Spika, naomba unuruhusu nizishukuru nchi mbali mbali na Mashirika kadhaa ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Serikali ya Misri, Japan, Serikali ya Oman, UNESCO na Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW) tuliyoshirikiana nao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu.
125.    Mheshimiwa Spika, mwisho naomba kukushukuru wewe binafsi, pamoja na Waheshimiwa wajumbe wote wa Baraza lako kwa kunisikiliza kwa utulivu na umakini mkubwa. Aidha, naomba kuishukuru Kamati ya Mifugo, Habari, Uwezeshaji na Utalii kwa namna ambavyo muda wote imekuwa ikinisaidia katika kuiongoza Wizara hii.
126.    Mheshimiwa Spika, naliomba sasa Baraza lako tukufu kujadili kwa kina matumizi jumla ya shilingi 15,366,575,000/=. Fedha hizo ni pamoja na miradi iliyoibuliwa kwenye maabara ya Utalii (Tourism Laboratory).  Kati ya hizo shilingi 9,371,200,000/= kwa kazi za kawaida na shilingi 400,000,000/= kwa kazi za maendeleo. Pia naomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 5,595,375,000/= kwa utekelezaji wa Programu ya Utalii. Aidha, naliomba Baraza lako liidhinishe makusanyo ya mapato ya shilingi 1,718,658,000/= kwa fedha zinazoingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Pia makusanyo ya shilingi 2,236,250,000/= ambazo hukusanywa na taasisi zilizoruhusiwa kutumia makusanyo hayo kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za taasisi hizo.
127.    Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa nawaomba wajumbe wa Baraza lako waijadili, watushauri, watuelekeze na baadae watupitishie bajeti hii ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kutoa Hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.