Habari za Punde

ZIRPP kuandaa makongamano Unguja na Pemba

Ndugu Wanachama,
Kwa ufadhili wa "The Foundation for Civil Society", ZIRPP inapenda kuwatangazia wanachama wake wote, pamoja na wananchi kwa jumla, kuwa imeandaa kongomano rasmi kuhusu "Makutano ya Fikra" litakalofanyika Unguja na Pemba.
Kwa upande wa Unguja, kongamano litafanyika siku ya Jumamosi tarehe 21 na Jumapili tarehe 22 Juni 2014, kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 11.00 jioni, katika Ukumbi wa ZIRPP uliopo katika Ofisi yake nyuma ya Majestic Cinema, Vuga.
Kwa upande wa Pemba, kongomano litafanyika siku ya Jumaane tarehe 24 na Jumatano tarehe 25 Juni 2014, kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 11 jioni, katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo, Chake Chake.
Waalikwa wasiozidi 40 wanatarajiwa kushiriki kikamilifu katika mijadala itakayojitokeza. Watoa mada wawili watawasilisha hoja mahsusi kwa madhumuni ya kuibua mjadala. Chakula pamoja na gharama za usafiri wa ndani zitatolewa na ZIRPP kwa waalikwa wote.
Ufuatao ni waraka maalum uliotayarishwa na ZIRPP kwa ajili ya kuelezea kusudio na madhumuni ya kongomano hili:
 
MAKUTANO YA FIKRA: NI MUUNDO, NI UGATUZI WA MADARAKA, AU NI KUDUMISHA MUUNGANO?
Utangulizi
Taifa la Tanzania linapita katika kipindi kigumu kuelekea kuzaliwa upya kwa Tanzania na kujitayarishia katiba yake. Zoezi hili ni lazima lifanyike kwa sababu hakuna mbadala wake. Hatua nyingi za awali zimepita katika jitihada za kutekeleza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na mambo mengine, hatua hizo zilijikita katika kukusanya maoni, kuyachambua na kutayarisha Rasimu ya Kwanza ambayo ilirudishwa tena kwa wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba kwa madhumuni ya kutolewa maoni.
Kulikuwa na Mabaraza ya Katiba ya aina mbili; yale yaliosimamiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na yale yaliyoanzishwa na  taasisi mbali mbali na ambayo yalikuwa yakijisimamia wenyewe. Kazi ya mabaraza hayo yote ilikuwa ni kuwapa fursa wajumbe wake ya kutoa mawazo kwa madhumuni ya  kuiboresha rasimu.
Hatua iliyofuata ilikuwa ni kutengeneza Rasimu ya Pili ambayo, tayari hivi sasa, iko mbele ya Bunge Maalum la Katiba baada ya kuwasilishwa rasmi na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba, na kufuatia kuzinduliwa kwa Bunge Maalum la Katiba kulikofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete.
Kwa bahati mbaya, katika kipindi chote ambacho Bunge Maalum la Katiba limekuwa likijadili Rasimu ya Pili, kumejitokeza hali ya kutatanisha, mikanganyo, mivutano na hata matukio ya kuumbuana na kukomoana miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Pia, kumekuwa na mkinzano wa kifikra na hasa zaidi, kwa kiwango kikubwa, hoja kuu imekuwa ni suala la muundo wa Muungano. Na tofauti kubwa  ya mawazo imejitokeza zaidi kati ya wale wanaotaka mfumo wa Muungano wa Serikali 2 uendelee baada ya kufanyiwa maboresho madogo; na wale wanaotaka mfumo wa Muungano wa serikali 3, kama ulivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mjadala nje ya Bunge
Hapana shaka yoyote ile kuwa afya nzuri ya kisiasa inaweza kupatikana iwapo mjadala juu ya kupatikana kwa Katiba Mpya utaendelezwa nje ya Bunge Maalum la Katiba. Pendekezo hili ni muhimu kwa sababau zifuatazo:
Kwanza, ni kwa sababu ya kuendeleza uhai wa mjadala wenyewe;
Pili,  ni kwa madhumuni ya kuendeleza ushiriki mpana wa Umma;
Tatu, ni muhimu kwa sababu ya uwezekano mkubwa wa kuweza kusikia hoja mpya ambazo zinaweza kujitokeza na ambazo hazimo katika rasimu;
Nne, ni kwa madhumuni ya kuwapa wananchi fursa nyingine tena ya  kujielewesha zaidi juu ya mchakato wa katiba; hasa zaidi kutokana na ukweli kuwa wao ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho katika jitihada za kupata katiba mpya kupitia Kura ya Maoni; na
Tano, na muhimu kuliko yote, ni kupata uwakilishi wa kweli wa wananchi katika Bunge hilo, kwa vile inaonekana wazi kuwa Wabunge wa Bunge hilo huwa wanadai kuwa wametumwa na wananchi ilhali hawajakutana nao kabisa.
Hiyo ndio dhana na msukumo wa mradi huu ambao utajikita zaidi kwa upande wa Unguja na Pemba; upande ambao ndio uliotia fora katika Bunge Maalum la Katiba. Na kama inavyosemwa: “Zumari likipulizwa Zanzibar; basi wananchi wa Maziwa Makubwa hucharukwa”. Na kwa mtazamo huo, kuyumba kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar, kuna athari mbaya ya kuliyumbisha Bunge zima.
Mjadala: Makutano ya Fikra
Madhumuni ya mradi huu ni moja katika jitihada za kuendeleza mjadala utakaokutanisha, kugongesha na kupimisha fikra za wananchi katika suala ambalo linaonekana kuchapisha zaidi vichwa vya habari katika vyombo mbali mbali vya habari; lakini pia kugusia hisia na vichwa vya wananchi.
Ni jambo lisolokuwa na ubishi kuwa nje ya Bunge Maalum la Katiba, bado hakujafanyika mjadala wa wazi wenye lengo la kukutananisha pande mbili kuu katika kujadili suala zima la muundo wa Muungano; lakini ni jambo lililojitokeza wazi na lisilopingika kuwa kila upande hukaa peke yake na kijijadili suala hilo kivyake;  kama vile Waswahili wasemavyo: “ Msema pweke hakosei”.
Kwa muktadha huu, mjadala wa Makutano ya Fikra utasaidia sana katika mambo muhimu yafuatayo:
i) kupanua mawazo baina ya kambi tofauti;
ii) kuondoa khofu miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
iii)  kuonyeshana faida, mapungufu na hasara zinazoweza kupatikana;
iv) kuonyeshana au kutanabahishana juu ya maeneo ya maridhiano.
Jitihada za aina hii ni muhimu sana katika kufikia maridhiano ya kweli; kwa sababu, mwisho wa siku, wote wale wenye fikra zinazokinzana katika mjadala huu muhimu katika historia ya taifa letu, wataweza kujenga nyumba moja iliyo imara badala ya kunyang’anyiana fito.
La muhimu zaidi katika mjadala huu ni kuwa Makutano ya Fikra yatasaidia sana katika kufanikisha jitihada za kujenga maridhiano endelevu kutokana na ukweli kuwa haijapata kutokea na haitatokea kabisa katiba ya nchi kupatikana au kuundwa bila ya maridhiano kutoka kwa wananchi wenyewe.
Eneo na muda wa mradi
Eneo la utekelezaji wa mradi huu ni Zanzibar; yaani Unguja na Pemba.  Eneo hili ni muhimu sana kwa sababu, mara nyingi, ndilo ambalo miripuko na migogoro mingi ya  kisiasa na athari zake mbaya kwa taifa huanzia na kuchipukia.
Dalili za uwezekano wa kutokea mripuko mkubwa zimeshaanza kuonekana hivi karibuni wakati wa kikao chaBunge Maalum la Katiba kule Dodoma ambapo Wazanzibari walionekana wazi wazi wakipingana na kukinzana kisiasa nje ya utaratibu na kanuni za mikutano, na ustaarabu na utamaduni wa Kitanzania.
La kusikitisha zaidi ni kuwa Wazanzibari walishindwa kusimama pamoja, hata katika mambo ya msingi na yenye mguso wa pamoja (common touch), na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kutikisa na kuliendesha kombo Bunge Maalum la Katiba.
Sasa, kwa vile Bunge Maalum la Katiba limeakhirishwa hadi mwezi Agosti 2014 baada ya Bunge la kawaida kukamilisha vikao vyake vya kujadili bajeti ya serikali, itakuwa vyema kuitumia fursa hii kwa madhumuni ya kuanzisha jitihada mpya kwa lengo la kukutanisha fikra, na kuchemsha bongo juu ya namna bora ya kutokana na mkwamo ambao nchi, kwa bahati mbaya, imejikuta imeingia hivi sasa.
Mkwamo wa Bunge
Kwa sasa, ingawaje imejitokeza fursa moja nzuri inayotokana na haja na ulazima wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano kujadili Bajeti za Serikali za Mwaka wa Fedha 2014/2015, lakini, ni kweli pia kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR, DP na UDP wameamua kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba chini ya uongozi na uamuzi wa umoja unaoitwa UKAWA.
Isitoshe, kumekuwa na mkorogano zaidi baina ya UKAWA, kwa upande mmoja, na TANZANIA KWANZA, Umoja unaojumuisha chama tawala - CCM na vyama vingine vidogo vya upinzani, kwa upande mwingine. Malumbano, mivutano na kushambuliana hadharani imekuwa ikitamalaki ndani ya Bunge Maalum la Katiba, huku kila upande ukidai kuwa hoja yake ndio madhubuti na ndio inayofaa kupitishwa katika Bunge Maalum la Katiba.
Wadau mbali mbali wametoa wito kuitaka Serikali, au CCM yenyewe, kuchukua hatua zipasazo kwa madhumuni ya kufungua milango ya mazungumzo katika jitihada za kujikwamua; lakini, chama tawala, CCM, ambacho ndicho chenye nafasi na uwezo mkubwa wa kufanya hivyo, kimeshatoa tamko kuwa hilo halitatokea.
Kwa maana hiyo, haitokuwa rahisi au itahitaji bidii kubwa kutoka pande mbili hizo, hasa UKAWA, kurudi tena katika Bunge Maalum la Katiba, kwa maslahi ya taifa, ili Katiba Mpya iweze kupatikana, kama lilivyokuwa inatarajiwa, katika jitihada za kufanikisha lengo la awali.
Utekelezaji wa mradi
Mradi utatekelezwa kwa hatua zifuatazo:
1)    Mikutano 2 ya siku mbili itayokutanisha wasomi na mabingwa na wataalamu  wa fani mbali mbali itaitishwa kwa madhumuni ya kupitia historia, hali ya kisiasa na rasimu iliopo, ili kuyapitia kwa karibu zaidi maeneo yanayobishaniwa, kutafuta njia ya kupunguza tofauti na kupendekeza njia mbali mbali au hatua ambazo Zanzibar inaweza kuchukua katika jitihada za kupata maridhiano;
Vikao vitaendeshwa kwa namna ambayo itasaidia kuzuia USIASA ili kuweza kupata ufumbuzi au suluhisho la kudumu kuhusu tatizo linalolikumba Bunge Maalum  la katiba. 
Mkutano mmoja utafanyika Unguja na mwengine utafanyika Pemba.
     2.   Mdahalo 1 utakaofanyika Unguja na kushirikisha pande kinzani, utarushwa moja kwa moja hewani kupitia vyombo vya habari vya Zanzibar. Mdahalo huo utakutanisha wajumbe wa pande zote wenye fikra zinazokinzana, waliokuwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wawakilishi wa Kundi la 201 na wadau wengine mbali mbali na wananchi kwa jumla.
 
Natanguliza shukrani zetu za dhati kwa ushirikiano wenu.

Muhammad Yussuf
Executive Director
Zanzibar Institute for Research and Public PolicyP.O. Box 4523
Zanzibar
TANZANIA
Tel: 0777 707820 Cellular
Tel: 0242 223 8474 Office
Fax: 0242 223 8475
Email: 
yussufm@gmail.com
Website: www.zirpp.org

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.