Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameshiriki maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya miaka 50 ya Muungano wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam kama mgeni maalumu kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Taifa hilo Mhe. Bui Thanh Son yaliyofanyika jijini Ho Chi Minh, Viet Nam leo Aprili 30, 2025.
Akizungumza kwenye sherehe za maadhimisho hayo Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam Mheshimiwa Generali Lương Cường ameeleza kuwa, madhimisho hayo yanaandaliwa ikiwa ni ishara ya kutambua na kuheshimu mchango wa kipekee wa mashujaa wa Taifa hilo uliojenga misingi ya mafanikio yaliyofikiwa na Taifa hilo kwa kipindi cha nusu karne katika kujenga umoja wa kitaifa, maendeleo ya kiuchumi na mahusiano ya kimataifa.
“Miaka hamsini imepita tangu tupate ushindi wa kihistoria Aprili 30, 1975, lakini kumbukumbu za miaka hiyo ya mapigano makali hubakia kuwa hai katika mioyo ya watu wa Vietnam kila tunapokumbuka ushindi huu mkubwa. Kila tunapoadhimisha siku hii, naguswa sana ninapowakumbuka wenzangu waliotoa uhai na damu yao kama sadaka kwa ajili ya ushindi wa Taifa letu. Ninainamisha kichwa changu ikiwa ni ishara ya shukrani zangu nyingi kwa akina Mama shujaa wa Vietnam ambao walitoa vijana na waume zao wapendwa kwa ajili ya Nchi yetu”. Alisema Rais Generali Lương Cường.
Aliendelea kueleza kuwa ni suala la kujivunia, licha ya vita walivyopigana hadi kufikia wakati huu, ikiwa imepita takribani miaka 40 wanaendelea kuishi katika Taifa lenye amani, umoja, uhuru na kujitegemea huku wakiendelea kufuata misingi ya kijamaa iliyoasisiwa na chama.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi wa Nchi na Serikali, na Wanadiplomasia kutoka mbalimbali duniani, ambapo kutoka Afrika ni mataifa matatu pekee yaliyoalikwa kwenye maadhimisho hayo ambayo ni Tanzania, Angola na Msumbiji.
Mbali na kushiriki katika sherehe za uapisho huo, Waziri Kombo alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Viet Nam Mhe. Pham Minh Chinh jijini Ho Chi Minh, muda mfupi baada ya kumalizika kwa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya miaka 50 ya Uhuru na Muungano wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam.
Mazungumzo hayo yalijikita kujadili kuhusu masuala mbalimbali ya kudumisha na kukuza zaidi ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo; biashara na uwekezaji, utalii, uchumi wa bluu, viwanda, kilimo, elimu na mafunzo kwa lengo la kukuza ustawi kwa pande zote mbili za Mataifa hayo rafiki.
Waziri Kombo alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Viet Nam, ambapo amehitimisha leo Aprili 30, 2025.
No comments:
Post a Comment