HOTUBA
YA WAZIRI WA AFYA MHESHIMIWA JUMA DUNI HAJI KUHUSU MAKADIRIO NA MATUMIZI YA
WIZARA YA AFYA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15 KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI,
ZANZIBAR
1.0 UTANGULIZI
1.0.1 Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja kwamba sasa Baraza lako
tukufu likae katika kamati ya matumizi ili isikilize maelezo ya makadirio ya
mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa kazi za kawaida na kazi za maendeleo
kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
1.0.2 Mheshimiwa
Spika, kabla ya yote, sina budi kuanza kumshukuru
Mola wetu mtukufu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema, usalama wa nchi uliotuwezesha
kukutana hapa na kuniwezesha kutoa hotuba ya wizara yangu mbele ya wajumbe wa
Baraza hili tukufu. Pongezi maalum
ziende kwa Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamo
wa Kwanza wa Rais na Makamo wa Pili wa Rais kwa busara na hekima za utawala
katika kuiongoza nchi hii.
1.0.3 Mheshmiwa
Spika, nichukuwe nafasi hii pia kuwashukuru
wajumbe wa Baraza lako, viongozi wa mikoa, wilaya na kwenye jamii, pamoja na
wananchi wenyewe. Natambua michango yao
ya hali na mali waliyoitoa, imeshajiisha kwa kiasi kikubwa kujenga dhamira, ari
na imani kubwa kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kutoa huduma zilizobora. Aidha
naomba nichukue fursa hii kumpongeza Naibu Waziri wa Afya, Katibu Mkuu,
Wakurugenzi, Watendaji na Wataalamu wote wa wizara yangu kwa juhudi na
mashirikiano waliyonipa na utendaji wao wa kuwahudumia wananchi kwa uadilifu
uliopelekea kufanikisha kazi zilizopangwa. Vile
vile napenda kuchuchua fursa hii kuliomba Baraza lako tukufu kupitia
Waheshimiwa wajumbe kuzidi kumuombea dua Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dk.
Malick Abdalla Juma baada ya kupata ajali ya kuvamiwa na majambazi alipokuwa
Nairobi siku ya tarehe 23 Novemba 2013.
1.0.4 Mheshimiwa
Spika, baada ya kutoa pongezi zangu hizo, naomba
uniruhusu nitoe maelezo ya mapato na matumizi, utekelezaji wa majukumu na
malengo makuu pamoja na changamoto zilizojitokeza kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Hatimae nitoe malengo na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/2015.
2.0 MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA
2013/2014
2.1 Mheshimiwa Spika,
upatikanaji wa rasilimali fedha una mchango mkubwa katika kutekeleza malengo ya
wizara, kama msemo wa kiswahili unavyosema gogo haliendi ila kwa nyenzo. Kwa
mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara ya Afya ilipangiwa kuchangia jumla ya Tsh. 924,000,000 kwenye mfuko mkuu wa
serikali kupitia vyanzo mbali mbali vya mapato.
Aidha, wizara iliidhinishiwa kutumia
Tsh 21,318,000,000, kati ya hizo Tsh
5,764,000,000 kwa kazi za kawaida, Tsh
1,536,585,000 ikiwa ni ruzuku na Tsh
14, 017,415,000 kwa mishahara na
maposho. Kwa upande wa kazi za maendeleo jumla ya Tsh 6,333,000,000 ziliidhinishwa kutoka SMZ na Tsh 42,335,617,000 kutoka kwa wahisani wa
maendeleo.
2.2 Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia mwezi wa Machi, 2014 wizara iliweza kuchangia Tsh 443,829,558 (48%) katika Mfuko Mkuu wa
Serikali. Vile vile katika kipindi hicho wizara imeingiziwa jumla ya Tsh 1,502,189,520 (26%) kwa kazi za
kawaida, Tsh 13,520,636,477 (96.4%)
kwa mishahara na posho, Tsh 614,292,912(45%)
ikiwa ni ruzuku. Kwa kazi za maendeleo wizara ilikwisha ingiziwa Tsh 1,767,181,149 (28%) kutoka SMZ na Tsh 13,042,037,000 (31%) kutoka kwa
washirika wa maendeleo.
2.3 Mheshimiwa Spika,
baada ya kueleza kwa muhtasari mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/2014
sasa nieleze utekelezaji wa malengo makuu ya wizara na kazi za kila siku kupitia
idara na taasisi ziliomo ndani ya wizara hii.
3.0 MAFANIKIO KWA MWAKA 2013/14
3.1 Mheshimiwa Spika, wizara
imepata mafanikio mazuri katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na
utekelezaji wa malengo yake makuu ya mwaka 2013/2014. Mafanikio hayo yanatokana
na kuwepo na usalama wa nchi kwa kipindi chote,
busara na hekima za utawala na uendeshaji wa nchi kutoka kwa viongozi
wetu wa kitaifa.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na:-
1. Kuongezeka
kwa upatikanaji wa fedha za kununulia dawa na vifaa tiba kutoka Tsh 3,028,372,981 kwa mwaka 2012/2013 hadi
kufikia Tsh 5,718,583,149 mwaka
2013/2014. Asilimia 25 ya fedha hizi
zilitoka Serikalini na asilimia 75
kutoka kwa washirika wa maendeleo. Kufanikiwa huku kumepunguza manung’uniko
makubwa ya ukosefu wa dawa katika hospitali na vituo vya afya.
2. Kuwapatia
wafanyakazi wa hospitali na vituo vya afya posho maalumu la mazingira hatarishi
(Risk Allowance).
3. Wizara imefanikiwa kusomesha wafanyakazi wake ambapo
kwa mwaka 2013/2014 jumla ya wafanyakazi 142
wamepelekwa masomoni kati yao wamo
madaktari saba wanaosomea fani mbali mbali za udaktari bingwa.
4. Kukamilika kwa
jengo la ofisi ya Mradi Shirikishi wa Afya ya Uzazi na Mtoto (IRCH) liliopo
Kidongo Chekundu.
5. Kuongezeka kwa kinamama wanaojifungua katika vituo vya
afya na hospitali kutoka asilimia 49.4
mwaka 2012 hadi asilimia 56.6 mwaka
2013.
6. Kuongezeka kwa asilimia ya watoto chini ya mwaka mmoja
waliopata chanjo (Penta 3) kutoka asilimia 81
mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 84.4
mwaka 2013.
7. Kupungua kwa ugonjwa wa Malaria katika jamii kutoka
asilimia 0.06 mwaka 2010 hadi
kufikia asilimia 0.03 mwaka 2013
8. Kujengwa kwa jengo jipya kwa ajili ya kutolea huduma
za upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo (Neurosurgical Services) katika
hospitali ya Mnazi Mmoja.
9. Kukamilika ujenzi na kulipatia
vifaa na samani jengo la wodi ya wagonjwa wa akili katika hospitali ya Wete
Pemba.
10. Ujenzi
wa vituo vya afya na nyumba za wafanyakazi Mzambarauni Pemba na Mwera Unguja
11. Ujenzi
wa jengo la huduma za akinamama na
huduma za uzazi ambalo limejumuisha wodi za wajawazito, magonjwa ya akinamama,
chumba cha upasuaji, maabara, sehemu ya kufulia na kliniki katika hospitali ya Wete
12. Kufunga mtambo wa kuchomea taka katika
hospitali ya Mnazi Mmoja
13. Ujenzi
wa chumba cha maiti katika hospitali ya Wete pamoja na ukarabati mkubwa wa Wodi
ya Mapinduzi Kongwe
14. Kuajiriwa
kwa wafanyakazi wapya 840 wa kada mbali mbali kama vile
madaktari, wauguzi, wasaidizi wafamasia,madaktari wasaidizi, madaktari
wasaidizi wa meno, mafundi sanifu wa maabara, maafisa afya ya
mazingira,wapishi,walinzi, maodali,
makarani, madereva na kadhalika.
3.2 Mheshimiwa Spika, baada
ya kueleza kwa muhutasari mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka wa fedha 2013/2014,
sasa naomba uniruhusu nieleze utekelezaji wa kazi kwa kila Idara na taasisi
ziliomo ndani ya wizara hii.
4.0 IDARA YA KINGA NA ELIMU YA AFYA
4.0.1 Mheshimiwa Spika,
Idara ya Kinga na Elimu ya Afya ina jukumu la kutoa huduma bora za kinga pamoja
na elimu ya afya kwa wananchi ili kujikinga na maradhi ya kuambukiza na yasiyo ambukiza.
Utekelezwaji wa kazi za Idara hii kwa mwaka 2013/2014 unaelezwa kupitia vitengo
mbali mbali kama ifuatavyo:
4.1 Kitengo
cha Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza
4.1.1 Mheshimiwa Spika,
kumekuwa na juhudi mbali mbali zinazofanywa ili kukuza uwelewa wa jamii juu
maradhi yasiyoambukiza, mojawapo ni filamu maalum iliyoandaliwa yenye kueleza
mambo hatarishi yanayochangia katika kupata maradhi haya. Filamu hii imetayarishwa
kwa kushirikiana na Idara ya Habari maelezo na kuionesha katika vijiji mbali
mbali vya Unguja. Pia vipindi mbali mbali vya televisheni na redio kuhusiana na
lengo hilo vimerushwa hewani.
4.1.2 Mheshimiwa Spika,
muongozo wa matibabu ya maradhi yasiyoambukiza umeandaliwa na wataalamu wetu
pamoja na madaktari bingwa na tayari sasa unatumika. Muongozo huu umezingatia
matibabu ya maradhi haya kwa upana wake. Aidha, kwa kushirikiana na Jumuiya ya
Watu Wanaoishi na Kisukari, kumeanzishwa vikundi vya mazoezi katika Wilaya zote
za Unguja na Pemba kwa nia ya kujikinga na maradhi haya. Vikundi hivi vimekuwa
vikipitiwa mara kwa mara kwa kupewa maelekezo na pia kualikwa katika tamasha
tofauti yanayohusiana na ufanyaji wa mazoezi.
4.1.3 Mheshimiwa Spika, utafiti
unaongalia mtizamo, na uelewa juu ya maradhi yasioambukiza umefanyika katika
Wilaya za Mjini, Magharibi, Kaskazini A, Chake Chake na Micheweni. Hatua
inayoendelea kwa sasa ni uchambuzi wa taarifa zilizokusanywa. Matokeo ya
utafiti huu yatasaidia katika kuweka mikakati itakayosaidia katika kupambana na
maradhi haya thakili kwa afya na maisha ya wanadamu.
4.1.4 Mheshimiwa Spika, katika
kuadhimisha kutimia miaka 50 ya Mapinduzi kitengo kilitoa huduma ya upimaji wa
hiari wa maradhi ya kisukari na shindikizo la damu. Jumla ya watu 574 walichunguzwa kati yao 85 walikuwa na dalili za shindikizo la
damu na watu 10 walikuwa na dalili za kisukari na kushauriwa kurudia
uchunguzi katika vituo vya afya vilivyo karibu nao.
4.1.5
Mheshimiwa Spika,
kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa maradhi ya moyo kutoka hospitali ya Mnazi
Mmoja Zanzibar, huduma ya siku tano kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo na
shindikizo la damu katika hospitali tatu za wilaya za Chake Chake, Wete na
Abdalla Mzee zilitolewa. Jumla ya watu 92
walichunguzwa (wanawake 64; wanaume 28), kati yao watu 11 waligundulika
kuwa na matatizo ya moyo wakiwemo watoto wawili ambao walipewa rufaa kwenda
katika hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
4.1.6 Mheshimiwa Spika, kwa
kushirikiana na Jumuiya ya Wanafunzi wa Udaktari - Tanzania Medical Students’
Association (TAMSA), kitengo kimefanya uchunguzi wa Kisukari na Presha katika
Wilaya za Mjini, Magharibi, Kati, Kusini, Kaskazini A na Kaskazini B. Jumla ya watu 1,800 walifanyiwa uchunguzi na matibabu yalitolewa kwa
waliogunduliwa na matatizo.
4.1.7 Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2014/2015 kitengo
kimepanga kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1. Kuanzisha
kamati ya kitaalamu itakayojumuisha wajumbe kutoka sekta mbali mbali ambayo
itakuwa na jukumu la kushauri, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mikakati
mbali mbali ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
2. Kuanzisha
daftari la usajili wa magonjwa yasiyoambukiza
3. Kuwasilisha
matokeo ya utafiti uliolenga kupima uelewa na mitazamo ya jamii juu ya magonjwa
yasiyoambukiza katika ngazi tofauti na kuyafanyia kazi.
4.2 Kitengo
Cha Kufuatilia Mwenendo wa Maradhi
4.2.1 Mheshimiwa
Spika, kwa kipindi cha mwaka
2013/2014 jumla ya watu 80 walitafunwa
na mbwa (wanaume 57 na wanawake 23) kutoka katika wilaya tofauti za
Zanzibar na kusababisha watu wawili kutoka maeneo ya Kiwengwa na Ndijani
Mseweni kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa (Rabies). Hivyo, kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo
na Uvuvi mikakati maalum ya kuweza kukabiliana na tatizo hilo imetayarishwa
ikiwemo kuendesha zoezi la uchanjaji wa mbwa katika shehia za Unguja,
kufuatilia taarifa za waliotafunwa na mbwa kwa kila siku, kutoa elimu kwa jamii
na kusimamia upatikanaji wa chanjo kwa wale waliotafunwa.
4.2.2 Mheshimiwa Spika, jumla ya wafanyakazi
wa afya 187 wanaoshughulika na utoaji wa taarifa za Wiki - Infectious Disease
Weekly Ending (IDWE) wamepatiwa mafunzo yanayohusiana na ugonjwa wa mafua ya
ndege (bird flu), ugonjwa wa bonde la ufa (Rift valley fever) na ugonjwa wa
kichaa cha mbwa (Rabies). Mafunzo haya yalifanywa kwa ushirikiano na kitengo
cha Epidemiolojia na Idara ya Mifugo.
4.2.3 Mheshimiwa Spika, sampuli
za maji zilichukuliwa kutoka maeneo tofauti baada ya kubainika kuwepo kwa
maradhi ya kuharisha katika maeneo hayo. Matokeo yalionesha maji kutoka visima
vya Fuoni Kibondeni na Chunga yana vimelea vya maradhi ya kuharisha. Hatua za kutia
dawa ya kuua vidudu kwenye maji hayo zimechukulia kwa kushirikiana na Mamlaka
ya Maji.
4.2.4 Mheshimiwa Spika, hivi
karibuni tumeshuhudia kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya “dengue” hapa nchini
unoambukizwa na virusi vinavyoenezwa na mbu aina ya “Aedeis”. Hadi sasa Hospitali ya Mnazi Mmoja imepokea
wagonjwa wanane kutoka maeneo ya Mwera (3), Kwamtipura (1), Darajabovu (1), Kama
(1) Fuoni (1) na Dar es Salaam (1)
waliodhaniwa kuwa na ugonjwa huu kutokana na dalili walizokuwa nazo. Kati ya wagonjwa
hao mgonjwa mmoja tu aliyetoka Darajabovu ndie aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa
huo ameshatibiwa na kupewa ruhusa.
4.2.6 Mheshimiwa Spika,
Wizara imechukuwa hatua mbali mbali katika kukabiliana na maradhi haya zikiwemo
kufanya mkutano na waandishi wa habari, kuelimisha jamii kupitia vyombo vya
habari (redio na televisheni), kutafuta vifaa vya kufanyia uchunguzi na kuandaa
mpango maalum wa kuwakumbusha wafanyakazi wa afya wa ngazi mbali mbali. Nachukua fursa hii kuwaomba wananchi kufuata
maelekezo yanayotolewa na wataalamu ili kuweka tahadhari ya kujikinga na
maradhi haya.
4.2.7 Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015, kitengo kimepanga kutekeleza
kazi kuu zifuatazo:-
1. Kutoa mafunzo ya afya
maskulini juu ya maradhi ya miripuko kwa yale maradhi yanayoibuka na
yanayo rejea (Emerging and Re-emmernging Infectious Diseases)
2. Kuendelea kufuatilia mienendo ya maradhi mbali mbali yanayo jitokeza katika jamii.
4.3 Kitengo cha
Huduma za Matibabu ya Macho
4.3.1 Mheshimiwa
Spika, kwa mashirikiano na uongozi wa Shirika la
Alnour Charitable Agency liliopo hapa Zanzibar, kambi kubwa ya uchunguzi na
matibabu ya macho ilifanyika kwa muda wa wiki mbili huko Pemba. Jumla ya watu 2,235 walipatiwa huduma, kati ya hao
waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho ni 152.
Vile vile watu 750 walipatiwa miwani
(wanaume 400 na wanawake 350).
Aidha, huduma za macho pia zilitolewa huko Pemba kwa ushirikiano na
Shirika la Bilal Muslim Agency kutoka Arusha Tanzania Bara, jumla ya watu 250 walichunguzwa na wagonjwa 68 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa
macho.
4.3.2 Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa watoto, huduma za upasuaji
macho zimefanyika kwa kushirikiana na daktari bingwa wa macho wa watoto kutoka
Tanzania Bara. Kwa mwaka 2013/2014 ni watoto wanane waliopelekwa Tanzania Bara kati
ya watoto zaidi ya 30 waliokuwa
wakihitaji huduma hiyo, hii ni kwa sababu madaktari hawa wanatoa huduma kwa
Tanzania nzima hivyo huwepo nje ya Mkoa wa
Dar er Salaam kwa kipindi kirefu.
Aidha, ufuatiliaji wa watoto wanaofanyiwa upasuaji umefanyika kwa kuwatembelea
watoto 69 (wanaume 29 na wanawake 40) kati yao watoto 34 walionekana
wanaendelea vizuri.
4.3.3 Mheshimiwa
Spika, kwa kushirikiana na Kitengo cha Elimu
mjumuisho na Stadi za Maisha cha Wizara ya Elimu kumeanzishwa mpango maalum wa
kuwafundisha walimu jinsi ya kuwapima wanafunzi wao uwezo wa macho kuona
(Vision Assessment). Hali hii inawezesha wanafunzi wengi kupimwa uwezo wa macho
kuona na kugundua matatizo yao ya macho na kurahisisha kazi ya uchunguzi wa
kitaalam kwa madaktari. Jumla ya walimu 348 wa Unguja na Pemba wa skuli tofauti
walipata mafunzo hayo na wao waliwagundua
wanafunzi 1,125 wana matatizo ya uoni.
4.3.4 Mheshimiwa
Spika, vifaa kadhaa vya kufanyia kazi katika hospitali
na huduma za vijijini vimepatikana ikiwemo gari moja kwa huduma za Macho
Pemba, pikipiki mbili, vifaa vinne vya kupimia miwani “Trial case” (vitatu
kwa Pemba na kifaa kimoja Unguja), mashine ya kupimia presha ya macho ya kisasa
imewekwa Hospitali ya Wete. Aidha, kumenunuliwa mashine
za kupimia macho (Slit lamps) na kupelekwa Pemba.
4.3.5 Mheshimiwa
Spika, kwa mashirikiano na Maabara ya Afya ya Jamii
(Public Health Laboratory) kumefanyika utafiti wa maradhi ya macho kwa watoto
wachanga wenye umri wa siku 28 za
kuzaliwa. Utafiti huu ulichukuwa takriban miezi 11 na kuhusisha watoto wote waliozaliwa kwa kipindi hicho na
kuwachunguza na kuwangalia kama wana maambukizo ya macho tongo
yanayosababishwa na vimelea (Clamidia na Gonococus). Jumla ya watoto 8,385 walizaliwa na kuingizwa katika
utafiti huo, kati yao watoto 511
walibainika kuwa na matatizo ya macho hivyo walipatiwa huduma stahiki.
4.3.6 Mheshimiwa
Spika, huduma za uchunguzi na matibabu ya macho zimeendelea kutolewa kupitia vituo vya Afya na mikusanyiko ya jamii
katika siku za afya za vijiji zinazosimamiwa na Timu za
Afya za Wilaya.
Jumla ya vijiji
na vituo vya Afya 22 vilitembelewa na kupatiwa huduma za macho ambapo wananchi 32,269 walifanyiwa uchunguzi, kwa wale
waliobainika na matatizo walitibiwa na pia ushauri uliotolewa kulingana na
matatizo yaliyobanika.
4.3.7 Mheshimiwa Spika, kwa
kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 kitengo kimepanga kutekeleza kazi kuu
zifuatazo:-
1. Kuendeleza
kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya macho kwa wananchi kwa mashirikiano ya
Timu za Afya za Wilaya (DHMTs)
2. Kutoa
huduma za matibabu ya macho kwa watoto hususan za upasuaji kwa msaada mkubwa wa
madaktari bingwa wa watoto kutoka Muhimbili chini ya mradi maalum wa Muhimbili
Childhood Initiative (MCBI).
3. Kuendelea
kutoa mafunzo ya msingi ya muda mfupi ya uchunguzi na utibabu wa macho kwa
wafanyakazi wa vituo vya Afya.
4.4 Kitengo cha
Kupambana na Maradhi Yasiyopewa Kipaumbele
4.4.1 Mheshimiwa
Spika, wizara imo katika kutekeleza mpango nzima
wa kuondoa kabisa maradhi ya kichocho na matende hapa visiwani. Kwa kipindi cha mwaka
2013 jumla ya wananchi 1,902 wamekaguliwa
Kichocho kati yao watu 1,249
walibainika na maradhi hayo sawa na 65.7%. Kwa upande wa matende wananchi 121 walikaguliwa na hakuna mtu hata
mmoja aliyebainika na vimelea vya Matende.
4.4.2 Mheshimiwa Spika, katika
jitihada za kuondoa maradhi ya kichocho, wizara imetiliana saini na Serikali ya
Watu wa China chini ya ushirikiano na usimamizi wa WHO kufanya utafiti wa
kuondoa kabisa maradhi ya kichocho nchini.
Mpango huu ni wa miaka mitano na utashughulikia ufuatiliaji wa
makonokono katika mito na mabwawa, mabadiliko ya tabia kwa wananchi dhidi ya
maradhi ya kichocho na ulishaji wa dawa za kichocho.
4.4.3 Mheshimiwa Spika, ukaguzi
katika baadhi ya mito na mabwawa 40 umefanyika
kwa lengo la kuangalia makonokono wenye uwezo wa kusambaza maradhi ya kichocho.
Ukaguzi huu ulifanyika katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba ambapo
makonokono yanayosababisha ugonjwa wa kichocho yaligunduliwa katika shehia 15.
4.4.4 Mheshimiwa Spika, ulishaji
wa dawa za kichocho, minyoo na
matende unaendelea kwa lengo la kutibu na kupunguza maambukizo
mapya ya maradhi hayo. Dawa hizi zinatolewa kwa wale wote wanaostahiki. Kwa Unguja jumla ya watu 744,434
walistahiki kula dawa, kati yao watu 625,092 (84%) walikula dawa. Kwa upande
wa Pemba waliostahiki kula dawa ni 348,570,
kati yao watu 290,862 (83%) walikula
dawa.
4.4.5 Mheshimiwa Spika, ili kukuza uelewa juu ya kujikinga na maradhi ya
kichocho, wizara imetoa mafunzo katika shehia 15 na skuli zilizomo katika shehia ya Mwera, Dole na Mwanakwerekwe. Aidha, wanafunzi
6,017 kati ya wanafunzi 7,317 wa skuli 15 zinazofanyiwa majaribio (82.2%)
wamehamasishwa kujikinga na kichocho kwa njia za michezo salama ya kurekebisha
tabia. Pia wanajamii 600 kutoka
shehia 15 wameelimishwa kuhusu kinga
dhidi ya maradhi ya kichocho.
4.4.6 Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka 2014/2015 kitengo kimejipangia kutekeleza kazi
kuu zifuatazo:-
1. Kuendeleza kazi za utafiti kwa ajili ya mapambano dhidi
ya maradhi ya Kichocho, Minyoo, Matende
pamoja na maradhi mengineyo yasiyopewa
kipaumbele.
2. Kitengo kitaendelea na kudumisha utafiti wa makonokono
ambao ni walezi wa viini vya maradhi ya kichocho katika mito na maziwa.
4.5 Kitengo cha Lishe
4.5.1 Mheshimiwa Spika, ulishaji
wa matone ya vitamini “A” na dawa za minyoo kwa watoto chini ya miaka mitano
ulifanyika kwa awamu mbili. Taarifa zinaonesha kuongezeka kwa kiwango cha
ulishaji wa matone ya vitamini A na dawa za minyoo kutoka 61.5% ya mwaka 2012 hadi kufikia 77.5% mwaka 2013. Matone ya Vitamin A yanasaidia kuwakinga watoto dhidi
ya magonjwa mbali mbali yakiwemo ya uoni mdogo na maradhi ya ngozi.
4.5.2 Mheshimiwa Spika, ili
kuongeza kiwango cha matumizi ya chumvi iliyowekewa madini joto katika jamii
yetu, wizara imefanya mafunzo kwa wauzaji wa chumvi wa rejareja na jumla juu ya
umuhimu wa ununuzi na usambazaji wa chumvi yenye madini hayo. Jumla ya wauzaji
chumvi 35 kwa Unguja na 30 kwa Pemba pamoja na wazalishaji wa
chumvi walishiriki mafunzo hayo.
4.5.3 Mheshimiwa Spika, ufuatiliaji
shirikishi wa huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa hospitali nane na vituo
vyote vya afya, umefanyika. Mapungufu yaliyobainika ni pamoja na uwekaji wa
taarifa za utapiamlo mkali kutoridhisha, jambo linalopelekea kukosa taarifa
sahihi juu ya hali ya utapiamlo mkali. Suala la utapiamlo limehimizwa sana
katika mkutano wa WHO Geneva na katika mikutano ya mawaziri wa afya waliokutana
Luanda nchini Angola mwezi Aprili, 2014.
4.5.4 Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka 2014/2015 kitengo kimepanga kutekeleza kazi kuu zifuatazo;-
1. Kuongeza kiwango cha utoaji
wa matone ya Vitamin A kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka asilimia
77.5 mwaka 2013 hadi asilimia 90 kwa mwaka 2014.
2. Kutengeneza
na kuchapisha miongozo mbali mbali juu ya unyonyeshaji na ulishaji wa watoto
wadogo.
4.6 Kitengo cha Afya
ya Wafanyakazi
4.6.1 Mheshimiwa Spika,
uchunguzi wa wafanyakazi umefanyika kwa wafanyakazi 8,108, kati yao 106 walibainika
kuwa na matatizo ya kiafya ikiwemo ugonjwa wa ini, homa ya tumbo, UKIMWI, shindikizo
la damu na uoni mdogo. Wafanyakazi hawa wametokea sehemu tofauti ikiwemo
maduka, mashirika ya uma, masoko, wafanyakazi wa viwanda. Kwa wale wote
waliobainika na maradhi, walishauriwa kwenda hospitali na kupata matibabu. Taarifa
hizi zinaongeza uelewa wa kuhitajika wafanyakazi tukiwemo sisi wawakilishi,
kupima afya zetu mapema kabla hatujaugua.
4.6.2 Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka 2014/2015 kitengo kitaendelea na kazi za ukaguzi sehemu za kazi pamoja na
kufanya uchunguzi wa afya za wafanyakazi.
4.7 Kitengo cha Afya
ya Mazingira
4.7.1 Mheshimiwa
Spika, katika hatua za utekelezaji wa sheria ya
afya ya jamii na mazingira namba 11
ya mwaka 2012, kitengo kimeweza kutengeneza muongozo wa utekelezaji wa sheria
kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa. Kazi hii imefanywa kwa kushirikiana na
wadau mbali mbali wakiwemo Chuo cha Afya Mbweni, Idara ya Mazingira, “Zanzibar
Chamber of Commerce”, Umoja wa Walemavu Zanzibar, Mamlaka ya Maji, Wizara ya
Biashara, Viwanda na Masoko, “Zanzibar Investment Promotion Authority”, na Baraza
la Manispaa.
4.7.2 Mheshimiwa
Spika, mnamo tarehe 23/10/2013, wizara yetu
iliadhimisha siku ya kunawa mikono duniani katika shehia ya Mangapwani wilaya
ya Kaskazini B. Maadhimisho hayo yalitanguliwa na utoaji wa elimu katika skuli 12 za msingi juu ya unawaji sahihi wa
mikono. Jumla ya wanafunzi 2,000
wanakisiwa kufaidika na elimu hii. Zoezi hili liliambatana na shindano la
kujibu maswali mafupi ambapo washindi watatu kutoka skuli ya Nyerere, Kiongwe
na Muungoni walipewa zawadi ya vifaa vya kunawia mikono mashuleni. Aidha, maadhimisho hayo yalijumuisha
kurushwa kwa ujumbe mfupi kwenye Redio na Televisheni. Pia Vipeperushi 500 na fulana 250 zinazobeba ujumbe wa kuhamasisha juu ya umuhimu wa kunawa
mikono zilichapishwa na kusambazwa kwa jamii.
4.7.3 Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kazi kuu zifuatazo
zitatekelezwa:-
1. Kufanya uhamasishaji wa sheria ya
afya ya jamii na mazingira ili
kuweza kueleweka.
2. Kutengeneza mwongozo wa maradhi ya kipindupindu.
4.8 Kitengo cha Afya
Bandarini
4.8.1 Mheshimiwa Spika,
kitengo hiki kinajumuisha huduma za afya za bandarini, Uwanja wa ndege na
chanjo kwa wasafiri wa kimataifa. Kitengo kimepewa dhamana ya kuzuia uingizwaji
na usafirishwaji wa maradhi pamoja na wadudu wasababishao maradhi toka nje ya
Zanzibar pamoja na kukabiliana na majanga ya kiafya.
4.8.2 Mheshimiwa Spika, kiasi
cha wasafiri 1,125 walitarajiwa
kuchanjwa, kati ya hao waliochanjwa ni wasafiri 814 (72.3%). Mbali na uchanjaji huo, ukaguzi wa vyombo vya usafiri
wa baharini na mizigo pia umefanyika, vyombo vilivyotarajiwa kuingia kukaguliwa
vilikuwa 1,557 ingawa vyombo
vilivyoingia na kukaguliwa vilikuwa zaidi ya matarajo na kuifikia 1,996 sawa na asilimia 128.1. Matokeo ya ukaguzi yamebainisha
kuwepo kwa vyombo 45 vilivyopatikana
na wadudu, vyombo 31 kati ya hivyo
vimefanyiwa ufukizwaji (fumigation) na Vyombo 14 vimefanyiwa hatua za usafi (upuliziaji/mitego). Aidha, mabaharia
98 wamekaguliwa, kati yao 46 walibainika kuwa hawajapima afya zao
hivyo kupatiwa chanjo zilizostahiki.
4.8.3 Mheshimiwa Spika, kontena 270 za mitumba na vifaa vilivyotumika zimekaguliwa zikiwemo tani za nguo 88, tani za viatu 16, mikoba na friji tani 123.
Jumla ya tani 15 za nguo na
tani 1.7 za viatu zimeangamizwa
baada kuonekana hazifai kwa matumizi ya binadamu. Pia kontena zote zilizoingia zimefanyiwa
ufukizaji.
4.8.4 Mheshimiwa Spika, ukaguzi
wa maiti 93 na wagonjwa 172 waliopitishwa bandarini na uwanja
wa ndege ulifanyika na hakukuwa na mgonjwa wala maiti aliyeonesha dalili za maradhi
ya kuambukiza. Aidha, wageni 62,736 walifayiwa ukaguzi kati yao 13,805 walibainika hawana kadi za
chanjo, 13,328 walitoka katika
maeneo yasio hatarishi, wenye sababu za kiafya walikuwa 453 na 24 walichanjwa
wakati wa kuwasili.
4.8.5 Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka 2014/2015 kitengo kinatarajia kufanya kazi kuu zifuatazo:-
1. Kuendelea
kutoa chanjo kwa wasafiri wa kimataifa.
2. Kuendelea
na ukaguzi wa mazingira ya bandari na utoaji wa elimu ya afya kwa mabaharia.
5.0 IDARA YA TIBA
5.1.1 Mheshimiwa Spika,
Idara ya Tiba ina jukumu la kutoa huduma za tiba kupitia hospitali za Chake Chake,
Abdalla Mzee, Wete, Kivunge, Makunduchi, Micheweni na Vitongoji. Pamoja na utoaji
wa huduma za tiba, Idara hii pia inasimamia uendeshaji wa Mpango wa Damu
Salama, Mradi wa Chuo cha Madaktari Zanzibar na usafirishaji wa wagonjwa nje ya
nchi.
5.1.2 Mheshimiwa Spika,
Hospitali hizi zimeendelea kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa ndani na wa
nje pamoja na kutoa huduma za uchunguzi wa maradhi mbali mbali. Hadi kufikia
Machi, 2014 jumla ya wagonjwa wa nje 227,251
walipokelewa na kupatiwa huduma za matibabu ya nje (101,708 wanaume na 125,543 wanawake).
Wagonjwa waliolazwa walikuwa ni 25,465
(6,272 wanaume, 19,193 wanawake), kati yao 389
(2%) walifariki dunia ukilinganisha
na 1.02% mwaka 2013/14. Ufafanuzi
unaonekana kwenye kiambatisho namba1.
5.1.3 Mheshimiwa Spika, wastani wa idadi ya siku za wagonjwa
ambazo hulazwa katika hospitali zetu ni siku mbili, hali hii iko chini ya
kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya kuwa kila
mgonjwa anapaswa kulazwa hospitali kati ya siku tatu hadi saba. Mambo ambayo yanafikiriwa
kuchangia ni pamoja kukosekana vyumba vya kupumzikia wagonjwa (retention room)
mara baada ya kupewa matibabu na kuwa chini ya uangalizi wa daktari na
changamoto za uwekaji wa kumbukumbu za wagonjwa. Hata hivyo, matumizi ya
vitanda yanaonekana kuwa yapo chini ya kiwango kinacho stahili kulingana na
viwango vya matibabu vilivyowekwa ambacho ni (60%), hospitali za Makunduchi
(69%) na Micheweni (63%) pekee ndizo zilizofikia kiwango kinachostahili.
5.1.4 Mheshimiwa Spika, huduma
za mama wajawazito kujifungua katika hospitali zimeendelea kutolewa katika
hospitali zote zilizo chini ya Idara ya Tiba. Jumla ya kina mama wajawazito 10,913 walilazwa, kati yao wajawazito 8,189 walijifungua kwa njia ya kawaida,
na wajawazito 651 walijifungua kwa
njia ya upasuaji. Aidha, akina mama 21
walifariki dunia kwa sababu mbali mbali za kiafya zikiwemo kutoka damu kwa wingi
kabla au baada ya kujifungua, kifafa cha mimba na shindikizo la damu. Ufafanuzi
zaidi unaonekana katika kiambatisho
namba 2.
5.1.5 Mheshimiwa Spika,
hospitali hizi pia zinahusika na utoaji wa huduma za kliniki maalum
zikiwemo huduma za maradhi ya kisukari, shindikizo la damu, macho, pua,
masikio, koo, kifua kikuu pamoja na magonjwa ya wanawake. Kwa kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014,
jumla ya wagonjwa 66,856 walipatiwa
huduma katika kliniki hizo ukilinganisha na wagonjwa 83,557 mwaka 2012/13. Ufafanuzi zaidi unaonekana katika kiambatisho namba 3.
5.1.6 Mheshimiwa Spika, vifaa
vilipokelewa kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi kwa hospitali ya Kivunge,
vikijumuisha vifaa kwa ajili ya chumba cha upasuaji pamoja na vitanda sita kwa ajili ya wodi ya kina mama
wajawazito na vitanda 20 kwa ajili ya wodi ya watoto, mashine 20 za kupimia presha, “Stethoscope” 20, “vacum exrtractors na Doppler. Aidha,nguo za kuvaa katika
chumba cha upasuaji (Theatre) zilipokelewa katika hospitali ya Abdalla Mzee.
5.2 Matibabu Nje ya
Zanzibar
5.2.1 Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014 jumla ya wagonjwa 234 walifanyiwa tathmini. Kati ya hao wagonjwa 120 walihitaji kupatiwa matibabu nje ya Zanzibar. Wagonjwa 110 (92%) walipelekwa nje ya nchi na
wagonjwa 28 (21%), walipelekwa Tanzania
Bara. Jumla ya Tshs 2,564,627,947
zilitumika kwa matibabu nje ya nchi ya Tanzania na Tsh 32,487,750 zilitumika kutibia wagonjwa nje ya Zanzibar. Idadi hii
ya fedha zilizotumika ni kubwa ukilinganisha na fedha zilizopangwa ambazo
zilikuwaTsh 500,000,000.
5.3 Mpango wa Damu Salama
5.3.1 Mheshimiwa Spika, kwa
kipindi cha mwaka 2013/2014 Mpango wa Damu Salama ulipanga kukusanya “unit” 8,200 za damu kwa mwaka kutoka kwa
wachangiaji wa hiari, hadi kufikia Machi 2014 jumla ya ‘units’ za damu 6,671 (81.3%) zilikwisha kusanywa. Damu
hiyo ilifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya “HIV”, “Syphilis”, “Hepatitis B” na
“Hepatitis C” kabla ya kusambazwa katika hospitali mbali mbali Unguja na Pemba.
Damu iliyokusanywa iligawiwa katika hospitali zote 14 zinazotoa huduma ya damu.
5.3.2 Mheshimiwa Spika,
elimu ya afya juu ya uchangiaji wa damu kwa hiari imeendelea kutolewa katika skuli,
vyuo, mikusanyiko ya kidini, vilabu vya mipira na sanaa, vikosi vya ulinzi,
vilabu vya damu na vikundi vya mazoezi. Jambo
hili linasaidia kupata damu nyingi na kuwa na wachangiaji wa kudumu.
5.3.3 Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Tiba imejipangia kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1.
Kufufua kitengo cha kuratibu shughuli za uchunguzi (Diagnostic Unit)
2.
Kuimarisha upatikanaji wa
chakula kwa wagonjwa wote wanaolazwa katika hospitali.
3.
Kukusanya damu units 10,000.
4.
Kusambaza damu kwa asilimia
100 kwa hospitali zote zinazotoa tiba ya damu.
6.0 IDARA YA HOSPITALI YA MNAZI MMOJA
6.0.1 Mheshimiwa Spika,
Idara ya Hospitali ya Mnazi Mmoja ina jukumu la kutoa huduma za rufaa za
matibabu na uchunguzi wa maradhi mbali mbali. Idara
hii inajumuisha hospitali za Mnazi Mmoja, Mwembeladu na Kidongo Chekundu.
6.0.2 Mheshimiwa
Spika, nimeshawahi kueleza mbele ya Baraza hili
azma ya Wizara kuifanya idara hii kuwa ni taasisi yenye kujitegemea
kiuendeshaji, kwa nia ya kuimarisha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika
utekelezaji wa majukumu yake. Kwa nia ya kulifanikisha suala hili wizara
imewasilisha waraka rasmi katika kamati ya Baraza la Mapinduzi na kueleza
gharama za kuendesha hospitali hizo. Kimsingi kamati hiyo ya Baraza la
Mapinduzi iliridhia mapendekezo hayo na kuagiza waraka huo uwasilishwe katika
kikao cha Makatibu Wakuu.
6.0.3 Mheshimiwa
Spika, kikao cha makatibu wakuu kiliagiza wizara
kuipitia tena rasimu ya sheria hiyo ili kuiimarisha zaidi. Aidha, kikao
kiliagiza kwa mwaka 2014/15 Idara ya Hospitali ya Mnazi Mmoja ipewe kasma
(vote) yake badala ya kutegemea kasma ya Wizara. Nachukuwa fursa hii kuliarifu
Baraza hili kwamba tayari kasma kwa ajili ya idara hii imeshaanzishwa na
itaanza kutumika mwaka huu wa fedha.
6.0.4 Mheshimiwa Spika,
upatikanaji wa wafanyakazi wenye ujuzi ni miongoni mwa mambo muhimu ya
kufanikisha utoaji wa huduma bora. Kwa
kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ilipokea na kuwapangia kazi
wafanyakazi 115 wakiwemo
madaktari wa kawaida (Medical
Doctors) tisa, wauguzi watatu wenye
shahada ya pili, wauguzi 11
wenye shahada ya kwanza, wauguzi wanane wenye stashahada, wahudumu wa
Hospitali 80 na madereva wanne. Aidha, idara
imepata daktari bingwa wa maradhi ya akinamama (Gynaecologist) kupitia
ushirikiano na Chuo Kikuu cha Haukeland ambae atatoa huduma hospitalini hapo
kwa muda wa miaka miwili.
6.1 Hospitali ya
Mnazi Mmoja
6.1.1 Mheshimiwa Spika,
huduma katika hospitali hii ziliendelea kutolewa kama kawaida. Katika
kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, jumla ya wagonjwa wa nje 44,545 (wanawake 22,942 na wanaume 21,603)
walitibiwa. Wagonjwa waliolazwa kwa kipindi hicho ni 27,654 kati yao 822 walifariki dunia kwa maradhi tofauti. Angalia kiambatisho namba 4. Vile vile kiambatisho
namba 5 kinaonesha
wagonjwa waliotibiwa katika kliniki
maalum zikiwemo za meno, macho, masikio,koo na pua, maradhi ya mifupa, maradhi ya kina mama, maradhi ya
ngozi,maradhi ya kisukari na shindikizo la damu.
6.1.2 Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14 Wizara imeanzisha
huduma ya uchunguzi wa saratani katika hospitali hii, ambapo hadi kufikia Machi
2014 jumla ya wagonjwa 50 wamechunguzwa
(biopsy), kati yao 35 wamegundulika kuwa
na saratani na asilimia 43 ya
waliobainika walikuwa na saratani ya shingo ya kizazi. Idadi hii ni kubwa na ya
kutisha sana katika maendeleo ya afya ya kizazi. Hali hii inatoa umuhimu wa
kinamama kufanya uchunguzi wa afya zao mapema hususan katika suala la saratani
ya kizazi.
6.1.3 Mheshimiwa
Spika, hospitali imeanza kutoa huduma ya
uchunguzi wa maradhi ya kifua kikuu kwa kutumia mashine mpya ya kisasa (Gene
expert) yenye uwezo mkubwa wa kugundua vimelea vya maradhi hayo kwa haraka na
kubainika hata kama vimelea vya maradhi ni kidogo.
6.1.4 Mheshimiwa
Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana kwa
hospitali hii ni kuanzishwa kwa huduma za uchunguzi wa maradhi na tiba
za mfumo wa chakula (Gastro-enterology Endoscopic services). Aidha, huduma hizi
zimewezekana kutolewa baada ya kupata msaada wa vifaa na mtaalamu wa kutoa
huduma hizo kutoka Jamhuri ya Watu wa China. Hadi sasa ni wagonjwa 95 ambao wameweza kupatiwa huduma hizo.
6.1.5 Mheshimiwa
Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2013/14
nilieleza kwamba wizara imeajiri kampuni binafsi kwa ajili ya kusimamia ulinzi
katika hospitali hii, jambo ambalo limesaidia kupunguza msongamano wa jamaa
wanaokwenda kuangalia wagonjwa wao. Sambamba na hili wizara inaendelea na maandalizi
ya ujenzi wa jengo la kusubiria jamaa wa wagonjwa waliolazwa. Kwa sasa hatua
iliyofikiwa ni kupatiwa eneo na ruhusa ya ujenzi kutoka Wizara ya Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati pamoja na kutayarisha michoro. Hatua inayoendelea ni mazungumzo
kati ya Wizara ya Afya na Mamlaka ya Mji Mkongwe ili kuweza kujuwa ni jengo la
aina gani lijengwe bila ya kuathiri uhifadhi wa Mji Mkongwe.
6.1.6 Mheshimiwa
Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar
wanapata huduma na kuipunguzia gharama serikali za kupeleka wagonjwa nje ya
nchi, hospitali imeendeleza kuhudumia kambi za madakatari bingwa kutoka Spain,
Uholanzi na Ujerumani. Hadi kufikia Machi 2014 jumla ya wagonjwa 114
walichunguzwa na madaktari wa Uholanzi, kati yao wagonjwa 77 walifanyiwa upasuaji ikiwemo matatizo ya njia ya mkojo na matatizo
ya maradhi ya uti wa mgongo.
6.1.7 Mheshimiwa
Spika, kwa kushirikiana na jumuiya isiyokuwa ya
kiserikali Zanzibar Out Reach Programme (ZOP), idara imeendelea kuendesha kambi
za matibabu 48 zikiwemo za upasuaji
katika maeneo tofauti ya visiwa vyetu.
Idadi ya wagonjwa walioonwa ni 6,961
na waliofanyiwa upasuaji ni 433, pia
jumla ya watu 643 walipatiwa miwani. Naomba nichukue fursa hii kuipongeza
jumuiya hii kwa jitihada zao za kusaidiana na Serikali katika kuhakikisha
upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
6.1.8 Mheshimiwa Spika,
huduma za kujifungua ni moja ya huduma inayopewa kipaumbele katika hospitali
hii, ambapo kufikia Machi 2014, jumla ya wajawazito 8,420 walilazwa, kati yao 6,553
walijifungua kwa njia ya kawaida (normal delivery) na wajawazito 1,557 walijifungua kwa njia ya upasuaji. Pia wajawazito 21 walifariki dunia kutokana na sababu mbali mbali ikilinganishwa
na wajawazito 24 waliofariki mwaka
jana. Kiambatisho namba 6 kinaeleza zaidi.
6.2 Hospitali ya
Wazazi Mwembeladu
6.2.1 Mheshimiwa Spika,
hospitali hii ni maalum kwa ajili ya huduma za kujifungua ambapo hadi kufikia
Machi 2014 jumla ya kinamama 5,230 walipokelewa
na kinamama 4,873 walijifungua kwa
njia ya kawaida na 14 walijifungua kwa njia ya upasuaji na kwa bahati nzuri hakukutokea
kifo cha uzazi.
6.2.2 Mheshimiwa Spika,
napenda kuwaarifu wananchi kuwa baada ya kupata madaktari wazelendo pamoja na
wataalamu wa kutoa dawa za usingizi kuanzia mwezi wa Februari mwaka huu huduma
za kujifungua kwa njia ya upasuaji zinaendelea vizuri katika hospitali hii.
6.3 Hospitali ya Kidongo
Chekundu
6.3.1 Mheshimiwa
Spika, Hospitali ya Kidongo Chekundu ni hospitali
pekee ya rufaa kwa wagonjwa wa akili. Kwa kipindi cha Julai 2013 hadi Machi
2014, jumla ya wagonjwa waliolazwa ni 995 (651
wanaume na 344 wanawake), hili ni
ongezeko la wagojwa 479 ukilinganisha
na mwaka uliopita. Aidha, hospitali hii hutoa huduma za msingi ambapo jumla ya
wagonjwa wa nje 10,831 walipatiwa
matibabu (5,240 wanaume na 5,591 wanawake). Mgonjwa mmoja wa kike
alifariki dunia.
6.3.2 Mheshimiwa
Spika, kupitia mpango wa ubadilishanaji
wafanyakazi kati ya Idara ya Hospitali ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Chuo
Kikuu cha Haukeland, wafanyakazi wawili wa Hospitali ya Kidongo Chekundu
wamepelekwa Norway kupata uzoefu wa namna ya utoaji wa huduma hizo na muuguzi
mmoja kutoka Norway yupo Hospitali ya Kidongo Chekundu. Muuguzi huyo anatoa
mafunzo kwa wafanyakazi wa hospitali hii na vijana walioamua kuacha dawa za
kulevya waliokuwemo katika nyumba zinazotoa huduma za matibabu hayo (Sober House).
6.3.3 Mheshimiwa
Spika, katika hotuba ya wizara ya mwaka 2013/14
nilieleza kuwa wizara iliazimia kuimarisha huduma za mikoba kwa wagonjwa wa
akili. Napenda kuliarifu Baraza hili kuwa madakatari kutoka hospitali hii
hufanya matibabu ya huduma za mikoba katika hospitali za Wete Pemba mara moja
kwa mwezi na hospitali ya Makunduchi mara moja kwa kila wiki. Utaratibu huu
umesaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuwafikia na kuwapatia huduma mapema watu
wenye matatizo ya akili.
6.3.4 Mheshimiwa
Spika, Wizara imeshatengeneza ramani ya jengo la kutolea
huduma za matibabu kwa vijana walioathirika na madawa ya kulevya
(Detoxification centre). Kwa sasa hatua inayofuata ni kuitisha zabuni ya ujenzi
wa jengo hilo litakalogharamiwa na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Huakeland.
6.3.5 Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka 2014/15, Idara inategemea
kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1.
Kuendelea kufanya
marekebisho ya rasimu ya sheria ya kuifanya Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ni
taasisi yenye kujitegemea.
2.
Kujenga
jengo la kutolea huduma kwa waathirika wa madawa ya kulevya (detoxification
centre) katika hospitali ya Kidongo Chekundu.
3.
Kufanya
ukarabati wa wodi ya wanawake na wanaume.
4.
Kujenga
jengo la wagonjwa mahututi (ICU).
7.0 OFISI YA
MFAMASIA MKUU WA SERIKALI
7.1 Mheshimiwa
Spika, Ofisi ya Mfamasia
Mkuu wa Serikali ina jukumu la kusimamia utekelezaji
wa Sera ya Dawa (National Medicine Policy), ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
upatikanaji na utumiaji sahihi wa dawa (Rational Use of Medicine).
7.2 Mheshimiwa Spika, kuwepo
kwa dawa muhimu na vifaa tiba ni moja kati ya nyenzo muhimu katika kuimarisha afya
ya mwananchi. Kwa mwaka wa fedha 2013/14 wizara iliendelea kununua dawa na vifaa
tiba kwa kutumia fedha kutoka serikalini na washirika wa maendeleo. Kwa upande
wa Serikali kati ya Tsh. 2,166,801,000
zilizotengwa kwa mwaka 2013/14 Tsh. 1,443,804,904
(67%) zimepatikana. Pia Wizara imepokea dawa na vifaa tiba vyenye thamani
ya Tsh. 4,274,778,245 kutoka kwa Washirika wa
Maendeleo na misaada ya aina hiyo kutoka kwenye Taasisi mbali mbali. Kiambatisho namba 7 kinatoa ufafanuzi.
7.3 Mheshimiwa Spika, wizara inaendelea na
juhudi za kuanzisha mfuko maalumu wa dawa (Essential Medicine Account) ambapo
serikali na washirika wa maendeleo wataingiza fedha katika mfuko huo. Hatua za kufungua
akaunti pamoja na kusaini hati ya makubaliano (Memorandum of understanding) ya
mfuko huu zimeshakamilika. Aidha, hatua za ununuzi wa dawa kupitia mfuko huu
zimeshaanza, ni matarajio yetu kwamba mfuko huu utasaidia kudumisha upatikanaji
wa dawa muhimu na vifaa tiba kwa wananchi.
7.4 Mheshimiwa Spika,
ofisi pia imeweza kukamilisha Mpango Mkakati (Strategic Plan) wa Miaka Mitano
kwa kazi za uimarishaji wa huduma za dawa hapa Zanzibar. Wizara imeshaanza kuutangaza
mpango huo kwa Washirika wa Maendeleo kwenye mkutano wa Washirika wa Maendeleo uliofanyika
Dar-es-salaam tarehe 21/02/2014. Mashirika ya USAID, CDC, DANIDA, UNFPA, JSI na
GF yameonesha nia ya kusaidia utekelezaji wa mpango huo.
7.5 Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka 2014/2015 Ofisi ya Mfamasia
Mkuu imejipangia kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1.
Kuendelea kununua dawa na vifaa tiba kwa kutumia
mfumo wa ‘Framework Contract’
2.
Kuendelea kusimamia utumiaji sahihi wa dawa na
vifaa tiba (Rational use of Medicine).
8.0 IDARA YA BOHARI KUU YA DAWA
8.1 Mheshimiwa
Spika, Idara ya Bohari kuu ya Dawa ina jukumu la kupokea, kutunza,
kusambaza na kufanya ukaguzi wa dawa katika hospitali na vituo vyote vya afya
vinavyo milikiwa na serikali Unguja na Pemba.
8.2 Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha
huduma za usambazaji wa dawa na vifaa tiba, idara inaendelea kuuimarisha mfumo
wa usambazaji kwa kulingana na mahitaji (Pull system). Aidha, Mfumo huu umeonesha
mafanikio makubwa na ya kuridhisha ambapo idara imefanikiwa kuingiza vituo
vyote 144 katika mfumo wa “Pull
System” Unguja na Pemba kuanzia Disemba 2013, ambapo mahitaji halisi ya dawa na
vifaa tiba hubainishwa na kituo cha afya kupitia timu ya afya ya wilaya husika,
wakati huo huo mafunzo juu mfumo wa utunzaji na uwekaji mzuri wa dawa (mSupply),
yalitolewa kwa wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa.
8.3 Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka
wa fedha 2014/2015 Idara imejipangia kutekelaza kazi zifuatazo:-
1. Kuandaa rasimu ya sheria
ya Bohari kuu ya Dawa.
2. Kuendelea kuimarisha
mifumo ya uendeshaji kwa kazi za Bohari.
Mfumo wa usambazaji wa mSupply katika kuhifadhi, kutoa na kusambaza dawa.
3. Kuendelea kuwajengea
uwezo watendaji wa Bohari kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ili waweze kuitumia
mifumo iliyopo kwa umakini na ufanisi.
9.0 MAABARA
YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI
9.1 Mheshimiwa
Spika, Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali ina jukumu la kutoa huduma za kitaalamu na za kisayansi kwa kuangalia ubora na
usalama wa vyakula, madawa, udhibiti wa kemikali na kufanya uchunguzi wa
vielelezo vinavyowasilishwa kutoka taasisi tofauti vikiwemo vile vinavyohusiana
na makosa ya jinai.
9.2 Mheshimiwa
Spika, maabara
imeendelea na kazi zake za kufanya uchunguzi ambapo jumla ya vielelezo 489 vilichunguzwa kati ya Julai 2013 hadi
Machi 2014. Vielelezo hivi vinatoka Jeshi la Polisi, Vikosi vya SMZ na watu
binafsi kama inavyoonekana katika kiambatisho
namba 8.
9.3 Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
wa fedha uliopita maabara imetayarisha sheria ya kemikali na hivi sasa rasimu
(draft) ya kwanza ya sheria hii imepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa
ushauri zaidi wa kitaalamu wa kisheria.
9.4 Mheshimiwa
Spika, shughuli
nyengine zilizofanyika katika kipindi kilichopita ni pamoja na kufanya ziara ya
kimasomo huko Tanzania Bara katika Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili
kuweza kujifunza kwa vitendo shughuli zinavyofanyika katika maabara hiyo. Aidha, Mpango Mkakati wa miaka mitano (2013 –
2018) umetayarishwa na hivi sasa upo katika hatua za mwisho kukamilika.
9.5 Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka
2014/15 maabara imejipangia kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1. Kuendelea kufanya uchunguzi wa sampuli mbali
mbali zitakazowasilishwa katika maabara
2. Kukamilisha rasimu ya sheria ya kemikali pamoja
na kanuni zake.
3. Kuendelea na ukarabati wa jengo la Mkemia Mkuu
wa Serikali.
10.0 IDARA YA SERA, MIPANGO NA UTAFITI
10.1 Mheshimiwa
Spika, Idara
hii ina jukumu la kutayarisha sera, miongozo, na mipango
mikuu ya wizara pamoja na kusimamia utekelezaji wake. Aidha, Idara inaratibu tafiti zote za afya na
kusimamamia ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa taarifa za afya.
10.2 Mheshimiwa
Spika,
Idara inaendelea kuufanyia gharama Mpango Mkakati wa Tatu wa Sekta ya Afya
(2013/14 – 2018/19), kazi hii inafanyika kwa kushirikiana na Shirika la Afya
Duniani (WHO) kwa kutumia programu maalum ya Computer (One Health Costing
Tool). Program hii itasaidia kujua gharama halisi za utekelezaji wa mpango huu
kwa kipindi cha miaka mitano ijayo na kutoa matokeo ya muda mrefu hadi mpango
huu utakapomaliza kipindi cha utekelezaji wake. Kazi inayoendelea hivi sasa ni
ukusanyaji wa taarifa na kuziingiza katika program hiyo.
10.3 Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza wizara
imefanya utafiti wa kujua matumizi ya huduma za afya (National Health Accounts)
kutoka serikalini, washirika wa maendeleo, jumuia zisizo za serikali, waajiri na
watu binafsi kwa mwaka 2011/12 na mwaka 2012/13. Matokeo ya utafiti huo
yameonesha kwamba bado matumizi ya fedha kwa ajili ya huduma za afya kwa mtu mmoja
ni kidogo ($27 per capita) ukilinganisha
na kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni ($60).
10.4 Mheshimiwa
Spika, katika
kipindi hicho asilimia 32 ya fedha
za uendeshaji wa huduma za afya zimetoka kwa washirika wa maendeleo, asillimia 37.9 zilitoka serikalini na asilimia 25.8 zilitoka kwa wananchi. Matokeo
mengine ya utafiti huu yanaonesha kuwa kwa kulinganisha matumizi yote ya
serikali, sekta ya afya imepata asilimia 6.9
tu, kima ambacho ni kidogo ukilinganisha na Azimio la Abuja la kuwa sekta ya
afya ipatiwe asilimia 15 ya matumizi yote ya serikali. Hali hii inadhihirisha
kuwa kuna haja ya kutafuta njia mbadala za kugharamia huduma za afya ikiwemo
serikali kuongeza mgao wake kwa sekta ya afya.
10.5 Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka wa fedha 2013/2014, moja ya lengo kubwa
kati ya malengo ya makuu ya wizara ni suala zima la kuangalia njia mbadala za
kugharamia huduma za afya. Lengo hili limekuwa likitekelezwa na kusimamiwa na
Idara ya Sera, Mipango na Utafiti. Hatua
zilizofikwa hadi sasa ni kuanza kuzifanyia kazi njia kuu mbili endelevu za
upatikanaji wa fedha ambazo ni bima ya afya na kuazisha kodi maalum kwa
wasafiri wa kimataifa kupitia tiketi za ndege (International Arrivals Levy) kwa
ajili ya huduma za malaria na afya ya uzazi.
10.6 Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa bima afya ripoti ya awali ya mapendekezo
(Zero Draft) imewaslishwa kwa kamati ya wataalamu na kujadiliwa. Mapendekezo
hayo yatapimwa kwa kutumia takwimu za idadi ya watu na za kiuchumi (Acturial
study) ili kuangaliwa uwezo wa wananchi kuchangia mfuko wa bima pamoja na
uendeshaji wake. Aidha mapendekezo ya kodi kwenye tiketi za ndege kwa ajili ya
kugharamia huduma za kumaliza malaria nchini pamoja na huduma za afya ya uzazi
yamewasilishwa kwa Makatibu wa wakuu kwa njia ya semina na wametoa maoni yao
ikiwemo kuangalia zaidi vyanzo vya fedha vya ndani.
10.7 Mheshimiwa Spika, katika kuinua viwango vya
huduma za afya zinazotolewa, wizara imeanza kutekeleza rasmi mfumo wa kuwazawadia
wafanyakazi ‘Performance Based Financing’ kwa vituo vya afya, kwa kuanzia na
wilaya ya Mkoani kwa Pemba na Magharibi kwa Unguja kwa majaribio. Mfumo huu pia
una shabaha ya kuwafanya wafanyakazi wavutiwe na kazi wanayoifanya na waweze
kubakia kazini badala ya kutafuta kazi nje ya wizara hii. Hivyo viashiria
maalumu huangaliwa kabla ya kuwazawadia wafanyakazi.
10.8 Mheshimiwa Spika, matokeo ya awali kwa
kipindi cha miezi sita (Julai 2013 – Disemba 2013), yameonesha kuongezeka kwa
utumiaji sahihi wa miongozo ya matibabu, kuongezeka kwa wateja wa huduma za
uzazi wa mpango, kuongezeka ufuatiliaji wa watoto waliokosa chanjo mbali mbali
majumbani, huduma baada ya kujifungua na huduma nyengine za mama na mtoto,
kuwepo kwa mazingira salama (IPC) na pia kuengezeka kwa kiwango cha idadi ya
watoto wa kike kupatiwa chanjo ili kujikinga dhidi ya pepopunda.
10.9 Mheshimiwa Spika, katika kuendelea
na ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa za afya, Idara ilifanya ukaguzi elekezi wa
usahihi wa taarifa
za afya (DQA). Aidha, katika kupunguza vifo vya kinamama na watoto ili kufikia
malengo ya MKUZA, wizara imeanzisha programu maalum ya kompyuta ili kuwezesha
kufuatilia kwa urahisi taarifa za afya za mama kuanzia anapobeba ujauzito hadi
kujifungua kwake na mtoto kuanzia anapozaliwa hadi kufikia umri wa miaka
miwili. Kwa kuanzia programu hii iinatekelezwa kwa majaribio katika hospitali
ya Chake Chake.
10.10 Mheshimiwa Spika, takwimu
zinaonesha kwamba maradhi yaliyoongoza katika hospitali na vituo vya afya kwa
mwaka 2013 ni maradhi ya njia ya hewa (18.5%) maradhi mengineyo ya ngozi (4.7%), maradhi mengine ya kuharisha yasiyokuwa
kuharisha damu na kipindupindu (4.4%) masikio pua na koo (4.08%) maradhi ya
nimonia (3.2%), maradhi ya maambukizo ya njia ya mkojo (2.3%), majeraha (2.2%),
minyoo (1.7%), maradhi ya macho (1.5%), maradhi ya kinywa (1.5%) na magonjwa
yote yaliyobaki (55.4%).
10.11 Mheshimiwa Spika, shughuli za tafiti zinazohusu afya zimeendelea kuratibiwa katika wizara kwa
kufanya tafiti mbali mbali ukiwemo utafiti wa mahitaji
na matumizi ya damu ambao umehusisha
Hospital za Unguja na Pemba ili kujua usahihi wa mahitaji ya damu katika
hospital zetu, Aidha
jumla ya tafiti tisa zimepokelewa na kupitiwa ambazo kati ya hizo tafiti sita
zimeruhusiwa kuendelea na tafiti tatu zinaendelea kupata maelekezo zaidi ili ziendane na maadili ya tafiti za afya.
10.12 Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka 2014/2015, Idara ya Sera, Mipango na Utafiti imejipangia kutekeleza kazi
kuu zifuatazo:-
1. Kuendelea
kutafuta njia mbadala za kugharamia huduma za afya;
2. Kutayarisha
Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara;
3. Kuendelea
na ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa za afya;
4. Kushajiisha
ufanyaji wa tafiti mbali mbali za kiafya (Clinical Research) ili kuibua mambo
zaidi ya kitaaluma yanayohusiana na magonjwa
5. Kufanya
tathmini ya utekelezaji wa mfumo wa kuzawadia wafanyakazi kwa wilaya mbili za
majaribio ( Mkoani na Magharibi)
6. Kutayarisha na kupitia miongozo mbali mbali kwa ajili ya
utekelezaji wa shughuli za afya;
11.0 IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI
11.0.1
Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na
Utumishi ina majukumu ya kusimamia uwajibijikaji kazini, maslahi, haki, nidhamu
na stahiki na kujenga uwezo wa nguvu kazi ya afya. Aidha, idara hii husimamia masuala ya usafiri
utunzaji wa kumbukumbu pamoja na miundombinu yote iliyomo ndani ya wizara.
11.1 Nguvukazi ya Sekta ya Afya
11.1.1 Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya wizara ya mwaka 2013/2014 wizara
iliahidi kuwaombea wafanyakazi kulipwa posho la kufanyakazi katika mazingira
hatarishi (Risk allowance). Napenda kulijulisha baraza lako kuwa baada ya
makubaliano na sekta husika posho hilo limeshaanza kulipwa kwa wafanyakazi wa
hospitali na Vituo vya Afya.
11.1.2 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 jumla ya wafanyakazi 142 wa kada mbali mbali wamepelekwa masomoni ndani na nje ya nchi. Hivyo
kufanya idadi ya wafanyakazi wote wanaoendelea na masomo kufikia 246 (wanaume 110 na wanawake 136. Aidha, jumla ya wafanyakazi 44 wamerudi masomoni na kupangiwa kazi
kwa mujibu wa taaluma zao. Kiambatisho
namba 9 kinatoa ufafanuzi. Sambamba na hilo Wizara
imeajiri wafanyakazi 840 wa kada tofauti,
jumla ya wafanyakazi 83 (Unguja 57 na Pemba 26) wamestaafishwa kwa mujibu wa sheria na wafanyakazi tisa
(5 Unguja na 4 Pemba) wamefariki dunia.
11.2 Utawala na Uendeshaji
11.2.1 Mheshimiwa Spika,katika
kuimarisha miundombinu ya wizara vituo vya afya 20 vinaendelea na matengenezo chini ya ufadhili wa Shirika la
Danida. Vituo hivyo ni pamoja na kituo
cha Afya Mtangani ambacho kinajengwa upya, kituo hiki kimefikia katika hatua ya
kuezekwa. Vituo vyengine vinafanyiwa upanuzi kwa kujengwa chumba cha kuzalia
“matenity ward” vituo hivyo ni Selem,Chumbuni, Fundo, Sebleni na Muyuni. Ujenzi katika vituo hivyo upo katika hatua
tofauti.
11.2.2 Mheshimiwa Spika, matengenezo mengine yaliyofanyika ni katika kituo cha Wesha, Ukutini, Makangale na
Kombeni. Pia Kituo cha Nungwi, Kiombamvua, Bumbwini Misufini na Chwaka tayari
vimeshamalizika. Vituo vya Afya viwili
vinavyofadhiliwa na ufadhili wa ADB ambavyo ni Mzambarauni kwa upande wa Pemba
na Mwera kwa upande wa Unguja vipo
katika hatua ya mwisho za kumalizika.
Vile vile vituo vya Afya 21 vinatarajiwa kutengenezwa na Mradi
wa Orio ingawa bado ujenzi haujaanza lakini wakandarasi wameshaanza hatua za
kupima.
11.2.3
Mheshimiwa Spika, wizara imefanikiwa kuanzisha mfumo wa
ufuatiliaji wa miundo mbinu ya
wizara ikiwemo majengo, usafiri pamoja na vifaa. Katika kulisimamia hili mfumo
maalum wa uwekaji kumbu kumbu wa vyombo vyote vya moto umetayarishwa. Mfumo huu
una lengo la kuweza kufuatilia kazi zote ambazo zitatumia vyombo vya usafiri
ili kuweza kujua gari hizo zimepangiwa kazi gani. Zoezi hili tayari limeshaanza
ambapo jumla ya gari 80 kati ya 134 zimeshaingizwa kwenye mfumo huo.
11.2.4
Mheshimiwa Spika, Idara imeweza
kupitisha zabuni mbali mbali za ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya,
nyumba za wafanyakazi, pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya hospitali
kama vile “Mobile X-Ray” na Mashine ya kuchomea taka “Incenerator” kwa
ajili ya hospitali ya Mnazi Mmoja pamoja
na kusimamia zabuni ya ununuzi wa gari tatu, gari mbili kwa ajili ya kitengo shirikishi cha Ukimwi, Kifua Kikuu na
Ukoma, na gari moja ya Ofisi ya Mfamasia
Mkuu. Zabuni nyengine zilizopitishwa ni pamoja na zabuni ya upanuzi wa wodi ya wanawake na
wanaume Micheweni Pemba na zabuni ya ujenzi wa jengo la upasuaji wa uti wa
mgongo (Neurosurgery) ya hospitali ya Mnazi Mmoja.
11.2.5 Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa
fedha 2014/2015 Idara imejipangia kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1.
Kukamilisha mpango utakaosaidia
kuwahamasisha wafanyakazi kubaki kazini (Retension Strategy)
2.
Kuendeleza kuwapa mafunzo
ya muda mrefu na muda mfupi wafanyakazi wa afya
3.
Kutayarisha sera ya usafiri
ya wizara.
12.0 TAASISI MAALUM
12.1 Chuo cha Taaluma
za Sayansi za Afya - Zanzibar
12.1.1 Mheshimiwa Spika,
Chuo kinaendelea kutoa taaluma za afya kwa kiwango cha stashahada katika fani mbali
mbali. Kwa sasa chuo kina jumla ya wanafunzi 821 wakiwemo wauguzi (204),
wasaidizi madaktari (198), Maafisa afya
ya mazingira (136), Ufundi sanifu wa
maabara (122), Wasaidizi madaktari
wa afya ya kinywa na meno (21),
Wafamasia (127), na Ufundi sanifu wa
vifaa tiba “Biomedical Engineers” (13).
Ili kuweka mazingira mazuri kiutendaji na hatimae kuongezeka kwa motisha kwa
wafanyakazi wa Chuo, Muundo wa Utumishi kwa wafanyakazi wa Chuo umetayarishwa na
tayari umeshawasilishwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma
kwa utekelezaji.
12.1.2 Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 chuo
kinatarajia kutoa wahitimu 281
wakiwemo; wauguzi 67, Maafisa tabibu
51, Maafisa Afya Mazingira 49, Mafundi dawa 48, Madaktari wasaidizi wa afya ya kinywa na meno 13, mafundi sanifu wa maabara 40 na mafundi sanifu wa vifaa tiba 13. Wahitimu hawa pindipo wakiajiriwa
watasaidia sana katika kutatua tatizo la uhaba wa nguvu kazi ya afya katika
maeneo tofauti visiwani.
12.1.3 Mheshimiwa Spika, chuo
kimeanzisha masomo ya kujiendeleza kwa wafanyakazi wenye cheti kwa muda mrefu
na hawakupata bahati ya kujiendeleza kielimu katika fani zao. Hivyo kwa mwaka
wa masomo 2013/14, jumla ya wanafunzi 183
wanaendelea na mafunzo chuoni hapo na pia wanafunzi 11 wanaendelea na mafunzo ya elimu masafa kupitia AMREF.
12.1.4 Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Chuo
kimejipangia kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1. Kuendelea kutoa
mafunzo ya sayansi za afya na utabibu ambayo inakidhi mahitaji na viwango vya
kitaaluma kitaifa na kimataifa.
2. Kuanzisha Stashahada ya Physiotherapy
na Shahada ya Uuguzi kwa mwaka wa
masomo 2014/2015
3. Kuandaa Mpango wa Chuo wa kujiendesha (Bussiness Plan)
12.2 Bodi ya Chakula,
Dawa na Vipodozi
12.2.1 Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2013/2014, Bodi ilisajili jumla ya maduka 284 ya Chakula ya jumla na rejareja,
Ghala 25 za Chakula, Bekari 18, Hoteli 64, Mikahawa 45, viwanda
vya chakula tisa, “supermarket” tisa,
maduka ya kuuzia nyama 81, vyumba
vya baridi tisa, bidhaa za vyakula 10, maduka
ya dawa 106, maduka ya vipodozi 31, duka moja la vifaa tiba, ghala
mbili za dawa, dawa 12 na
virutubisho saba.
12.2.2 Mheshimiwa Spika, Bodi
ilikagua maduka 537 kutoka maduka 637 ya chakula ya jumla na rejareja
ambayo yalikaguliwa mwaka uliopita, ghala 18
za chakula, hoteli 56, mikahawa 39, viwanda vya chakula tisa,
“supermarket” tisa, maduka ya
kuuzia nyama 100, vyumba vya baridi tisa,
machinjio tisa, tani 247.72 za chumvi yenye madini joto, lita
1,488,073 za maziwa, tani 33.64 za bidhaa na mazao ya baharini, maduka ya dawa 132, ghala mbili za dawa, maduka ya vipodozi 35 na duka moja la vifaa tiba.
12.2.3 Mheshimiwa Spika, maabara
ya bodi hii ilipokea na kuchunguza sampuli
824 za chakula, sampuli 812 zilikua salama na sampuli 12 hazikufaa
kwa matumizi ya binadamu. Aidha,
sampuli 15 za dawa zilichunguzwa na
zote ziligundulika kuwa zinafaa kwa matumizi. Sampuli 16 za vipodozi zilichunguzwa na
hazikuonekana kuwa na madhara yoyote. Pia sampuli 10 za dawa za mitishamba zilichunguzwa ambazo zote zilionekana zinafaa kwa
matumizi ya binadamu.
12.2.4 Mheshimiwa Spika, jumla
ya tani 40 za bidhaa za chakula na
tani mbili za bidhaa za dawa na vipodozi zisizofaa kwa matumizi ya binaadamu
ambazo zilikamatwa kwenye maduka na bandari ndogo ndogo ziliteketezwa. Aidha, jumla ya tani 573.8 za bidhaa za chakula zisizofaa
kwa matumizi ya binaadamu zilirejeshwa zilikotoka.
12.2.5Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha 2014/2015 bodi imejipangia kazi kuu zifuatazo:-
1. Kusimamia marekebisho ya sheria ili kuifanya
Bodi kuwa na Mamlaka kamili.
2. Kumalizia ujenzi wa ofisi mpya za Bodi katika
eneo la Mombasa, Zanzibar.
12.3 Bodi ya Ushauri wa
Hospitali Binafsi
12.3.1
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Hospitali Binafsi ina jukumu
la kusimamia mwenendo wa hospitali binafsi kwa mujibu wa sheria za kuendesha hospitali
hizo (Private Hospital Regulation) Act No. 04 of 1994, Kazi kubwa ya bodi hii
ni kusajili, kutoa leseni kwa hospitali zinazokidhi viwango, kukagua, kusimamia
uanzishaji na uendeshaji wa hospitali na vituo binafsi vya afya pamoja na
kuzifungia zisizofikia viwango.
12.3.2
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014, bodi ilifanya ukaguzi
wa hospitali nne na vituo vya afya 67,
katika ukaguzi huo vituo 10 vilisimamishwa
kutoa huduma na vituo vitano kupewa onyo kali kutokana na kwenda kinyume na
sheria na miongozo ya uendeshaji wa hospitali binafsi. Aidha, jumla ya vituo
vipya viwili vimesajiliwa navyo ni Lancent Laboratory na F&M Rehabilitation
Clinic, hadi sasa kuna jumla ya vituo vya afya binafsi 71 (60 Unguja na 11 Pemba).
12.3.3 Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2014/2015 bodi
imejipangia kufanya kazi zifuatazo:-
1. Kupitia sheria ya kuendesha Hospitali binafsi.
2. Kufanya ukaguzi wa pamoja na wakaguzi kutoka Kamisheni ya
utalii kwa Hospitali zilizomo ndani ya Mahoteli ya Kitalii.
12.4 Baraza la Tiba Asili
na Tiba Mbadala
12.4.1
Mheshimiwa Spika, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala
(Traditional and Alternative Medicine Council) ni baraza liliopo chini ya
sheria No.8 ya mwaka 2008, baraza hili
linafanyakazi zake kisheria
katika kusimamia shughuli zote za tiba asili, kutoa usajili, kudhibiti,
kutangaza, kuelimisha jamii na kusaidia katika maendeleao ya shughuli za tiba
asili na tiba mbadala, pamoja na kuelimisha jamii kwa kutumia vyombo vya habari
kama TV, redio, mikutano ya waganga kupitia kwa masheha na madiwani au wakuu wa
wilaya na pia kutumia vipeperushi.
12.4.2
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014 baraza
la tiba asili liliweza kuongeza idadi ya waganga waliosajiliwa na kufikia 193 Unguja na Pemba kwa kuweza kutimiza
masharti ikiwa ni pamoja na kuwa na sehemu maalum ya kutoa huduma kwa wagonjwa.
Aidha, jumla ya maduka ya dawa za asili 31
yalisajiliwa kwa kutimiza masharti ya sheria za baraza, Kliniki za tiba asili
na tiba mbadala ni 11, (Unguja 9 na Pemba 2), wasaidizi waganga 58,
na vilinge 112, na sampuli za dawa
asili zilizochunguzwa na Maabara ya Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi ni 23 na zote zilionekana zinafaa kwa
matumizi ya binaadamu.
12.4.3
Mheshimiwa Spika, Baraza limefanya utafiti
mdogo juu ya tiba asili na tiba mbadala ambapo imegunduwa kwamba mahusiano ni
madogo yaliyopo baina ya waganga wa asili na waganga wa kisasa. Katika utafiti
huo imeonekana kutokuweko kwa mashirikiano baina yao katika kutoa huduma za
matibabu, kitu ambacho kinapelekea hata mgonjwa anapoanza kufuata matibabu kwa
mganga wa asili inakuwa ngumu kumpa rufaa kwenda kwa mganga wa kitaalam.
12.4.4
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2014/15 Baraza la Tiba Asili limedhamiria kufanya kazi kuu zifuatazo:
1. Kuendelea
kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa tiba asili na utumiaji mzuri na unaofaa wa
dawa za miti shamba kwa kutumia vyombo vya habari kama TV, Redio na pia kutumia
vipeperushi.
2. Kuhamasisha
usajili na kushajihisha hasa kwa waganga.
3. Kuendelea
na ukaguzi wa mara kwa mara katika sehemu wanazofanyia kazi waganga(vilinge) na wanazouza dawa hasa
misikitini na barabarani,na kufanya
ukaguzi wa kliniki za tiba mbadala na maduka ya dawa asili .
12.5 Baraza la Wauguzi na Wakunga
12.5.1
Mheshimiwa Spika, Baraza la wauguzi na
wakunga limefanya ukaguzi katika vyuo binafsi na vya Serikali vinavyotoa
mafunzo ya uuguzi ili kuhakikisha kiwango kinachotolewa kama kinakidhi mahitaji
ya taaluma na kutoa ushauri. Ukaguzi huo uliangalia mitaala ya kufundishia kama
inafuatwa ipasavyo, kuangalia utaratibu wa kujiunga na chuo kama unafuatwa kwa
mujibu wa miongozo, uendeshaji na usimamizi wa mitihani ya mwisho ya kila
daraja. Vyuo vilivyokaguliwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Zanzibar (Zanzibar
University) na Zanzibar School of Health. Mambo yaliyobainika katika ukaguzi
huo yalionekana mapungufu mbali mbali yakiwemo ya kimitaala na ukosefu wa
walimu wa kudumu.
12.5.2
Mheshimiwa Spika, Baraza limeweza kuandaa
mkutano wa pamoja wa kutayarisha “Scope of Midwifery Practice” kwa kushirikiana
na shirika la UNFPA na Jhipiego. Lengo la kikao hicho ni kuwa na muongozo wa
wauguzi ambaoutapelekea kutambua mipaka na majukumu katika utoaji wa huduma za
uuguzi. Aidha, Baraza limeweza kukisimamia kwa kutoa maelekezo ya kitaalamu kwa
Chuo cha Zanzibar School of Health katika kujiunga na mamlaka ya elimu ya juu
Tanzania National Commission for Technical Education (NACTE).
12.5.3
Mheshimiwa Spika, Baraza limeipitia upya
sheria ya Uuguzi na kuifanyia marekebisho na hivi sasa inasubiri kupelekwa
Baraza la Mapinduzi kwa mara ya pili. Aidha, Baraza limeendeleza ushirikiano na
mabaraza ya Wauguzi ya Afrika Mashariki na Kati kwa kuhudhuria mikutano na kutekeleza
maamuzi ya mikutano hiyo.
12.5.4
Mheshimiwa Spika, katika kuadhimisha siku ya wauguzi
duniani Baraza lilifanya uchunguzi wa awali wa saratani ya shingo ya kizazi
(Cervix Carcinoma) kwa kinamama, Jumla ya kinamama 350 wamefanyiwa uchunguzi kati yao 14 wamegundulika na matatizo hayo na kupewa huduma zinazostahiki.
12.5.5
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
2014/2015 Baraza limejipangia kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1. Kukamilisha
mapitio ya sheria ya Baraza la Wauguzi na Wakunga
2. Kufanya
ukaguzi katika hospitali Unguja na Pemba
3. Kutayarisha
“Nursing Procedure Manual”
4. Kuendelea
kusimamia maadili na haki za uuguzi.
12.6 Maabara ya Afya ya
Jamii -Pemba
12.6.1Mheshimiwa
Spika, Maabara ya Afya ya Jamii (PHL) imeanzishwa
kwa lengo la kuiwezesha sekta ya afya kuwa na chombo cha kufanya tafiti za
afya, kuangalia nyendo za maradhi mbali mbali na kutafuta mbinu za kuyadhibiti.
12.6.2Mheshimiwa
Spika, kwa mashirikiano na Chuo Kikuu cha John
Hopkins maabara inaendelea kutekeleza mradi wa miaka mitatu wa “Chlorehexdine
Study” kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga walio katika
umri wa siku 28 tokea kuzaliwa (reduction of neonatal deaths). Katika
kutekeleza hili watoto wote wanaozaliwa katika kipindi hiki wanapatiwa huduma
za vitovu (cord care). Katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Machi 2014 jumla ya
watoto 9,973 (wanaume 4,968; wanawake 5,005) wamepatiwa huduma hizo.
12.6.3Mheshimiwa
Spika, katika
kufanya uchunguzi wa kupandikiza makohozi kwa ajili ya kuona vimelea vya TB
(sputum Culture), maabara imepandikiza sampuli 574 za makohozi
kati ya hizo sampuli43
ziligundulika kuwa na vimelea vya TB na sampuli 531 zilionekana kuwa hazina vimelea vya TB.
12.6.4Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/15 maabara itaanza
kutekeleza mradi wa kutokomeza Kichocho
katika shehia za Mtangani, Wingwi na Kiuyu Minungwini.
13.0
MIRADI YA MAENDELEO
13.1 Mradi Shirikishi
wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Ukoma.
13.1.1Mheshimiwa Spika, mradi huu una lengo la kupambana na maradhi ya
UKIMWI, Kifua Kikuu na Ukoma ili kuwakinga wananchi wote wa Zanzibar kutokana
na maradhi haya. Mradi huu unahusisha utoaji wa huduma mbali mbali zikiwemo za
ushauri nasaha na uchunguzi, huduma za tiba pamoja na huduma za wagojwa
majumbani.
13.1.2Mheshimiwa Spika, jumla ya vituo 91 vinatoa huduma ya ushauri nasaha na upimaji wa VVU ukilinganisha
na vituo 87 mwaka 2012 kati ya hivyo
Unguja 58 na Pemba 33. Katika vituo hivyo jumla ya watu 61,921 walichunguzwa (wanawake 32,477 na wanaume 29,444). Katika uchunguzi huo jumla ya watu 966 (1.56%)
waligundulika kuwa wanaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU); wanawake ni 520 (54%) na wanaume 446 (46%).
13.1.3 Mheshimiwa Spika, katika utoaji wa huduma za tiba, hadi kufikia
mwishoni wa mwezi wa Machi 2014, jumla ya wagonjwa 6,982 walikuwa tayari wameshasajiliwa kwenye kliniki za tiba,
miongoni mwao wagonjwa 4,494 (64% -
lengo lilikuwa ni kufikia asilimia 65%) wanatumia dawa za ARVs, kati yao watoto
ni 397 (9%) Hili ni ongezeko la
asilimia sita ukilinganisha na mwaka 2012. Pia, kitengo kimeanzisha kliniki ya
tiba kwa wanaoishi na VVU kwenye Taasisi isiyo ya Serikali (NGO) ya ZAYEDESA.
Hii inafanya jumla ya kliniki hizo kufikia 11
(7 Unguja na 4 Pemba) ukilinganisha na mwaka 2012 ambapo kulikuwa na kliniki 10.
13.1.4Mheshimiwa
Spika, katika mapambano dhidi ya maradhi ya Ukoma elimu ya afya ilitolewa kwa
wananchi. Jumla ya vijiji 24 vya
Unguja na Pemba vilifanyiwa mikutano na kupatiwa elimu ya Ukoma, jumla ya watu 1,280 (Unguja 805, Pemba 475 walihudhuria
mikutano hiyo, kati yao watu 31
walishukiwa kuwa na dalili za Ukoma na watu saba waligundulika na Ukoma.
Kupitia juhudi za waratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma vituo vitatu vya kutoa
huduma za kujitunza ili wasiweze kupata ulevamu zaidi vimeanzishwa. Madhumuni
ni kuwafundisha wagonjwa namna ya kujitunza na kujilinda na ulemavu na baadae
waweze kujihudumia katika vikundi vyao.
13.1.5Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/2015, mradi
utatekeleza kazi kuu zifuatazo:-
- Kuongeza na kupanua
huduma za ushauri nasaha na upimaji kutoka vituo 91 2013/14 hadi kufikia
100.
- Kufanya tathmini ya
VVU na maradhi mengine ya kujamiiana katika makundi mbali mbali yakiwemo
kundi la mama wajawazito na wavuvi ili kuweza
kufuatilia mwenendo wa maradhi hayo.
- Kuanzisha huduma za
ushauri nasaha na upimaji VVU majumbani (HBHTC) katika Wilaya ya Kati kwa kufikia nyumba 1,846 za Shehia saba zilizomo katika wilaya ya kati.
13.2 Mradi wa Kumaliza Malaria
Zanzibar
13.2.1Mheshimiwa
Spika, katika jitihada za kumaliza Malaria
visiwani Zanzibar, mradi huu ulipanga kupiga dawa jumla ya nyumba 51,546
katika wilaya zote isipokua wilaya ya Mjini, Kati ya nyumba hizo nyumba 50,869 (98.6%) zimefanikiwa kupigwa dawa. Upigaji huu wa dawa ulihusisha
maeneo maalumu yaliobainika kuwepo kwa wagonjwa wengi wa Malaria.
13.2.2Mheshimiwa Spika, unyunyizaji dawa kwenye madimbwi ya maji yenye
viluilui vya mbu pia umefanyika. Kwa Unguja maeneo yaliyohusishwa ni Kaburi
kikombe, Kwa Binti Amrani, Sebleni, Mnazi Mmoja, Karakana, Kilimani, Mbuyuni, Kijitoupele, Kwa Mtumwajeni na Chumbuni.
Kwa upande wa Pemba kazi hii imefanyika katika maeneo ya Chimba, Tumbe,
Minungwini, Chwale, Uwandani na Gando.
13.2.3Mheshimiwa Spika, kwa vile kila
homa si malaria kuna umuhimu mkubwa wa kuchunguza damu kwanza ili kuhakikisha
iwapo ina vimalea vya malaria au la kabla ya kuanza kutumia dawa. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014
jumla ya watu 346,626 walichunguzwa
damu, watoto chini ya miaka mitano walikuwa 108,074. Kati ya waliochunguzwa, waliobainika kuwa na vimelea vya
malaria ni 2,680 (0.8%), kati ya hao watoto chini ya umri
wa miaka mitano walikuwa 406 (0.4%).
Asilimia 33 ya kinamama wajawazito
waliohudhuria kliniki (76,584), walichunguzwa
damu. Kati yao akinamama 77 (0.1%) waligundulika kuwa na malaria na
kupewa tiba sahihi juu ya kinga dhidi ya malaria.
13.2.4Mheshimiwa Spika, kazi ya kuwafuatilia wagonjwa majumbani na
kuchunguza familia zao iliendelea kufanyika. Wagonjwa
771 (76%) pamoja na familia zao (3,053)
waliweza kufuatiliwa hadi majumbani kwao. Kati ya 3,053, wanakaya 245 (8%) waligunduliwa kuwa na vimelea vya
malaria bila ya kuwa na dalili wala ishara ya kuumwa.
13.2.5Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 mradi unalenga
kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1. Kuupitia na
kuufanyia marekebisho muongozo wa uchunguzi na tiba ya malaria hapa Zanzibar
kuendana na hali halisi ya malaria hapa visiwani.
2. Kutengeneza
mwongozo wa Uchunguzi wa malaria kwa
kinamama wajawazito baada ya kusimamisha tiba ya tahadhari kwa wajawazito.
3. Kuendelea
kupiga dawa kwa maeneo yatakayobainika kuwa na wagonjwa wengi wa malaria.
4. Kuendelea
na kunyunyiza dawa kwenye madimbwi ya mazalio ya mbu.
5. Kuendelea
kugawa vyandarua kwa mama wajawazito, watoto walio chini ya umri wa miaka
mitano na kwa familia ambazo vyandarua vyao vimeharibika.
3.3 Mradi wa Kustawisha Siha za
Wazanzibari
13.3.1Mheshimiwa
Spika, mradi huu una jukumu la kuhakikisha kwamba jamii ya
wazanzibari inapata elimu ya kutosha jinsi ya kujikinga na maradhi
mbali mbali yakiwemo ya kuambukiza na yale yasiyoambukiza.
13.3.2 Mheshimiwa Spika, elimu ya afya iliendelea kutolewa kwa wananchi
kwa njia ya redio na televisheni ambapo jumla ya vipindi 80 vya aina mbali mbali vimerushwa hewani. Miongoni mwa mada zilizozungumzwa ni pamoja na afya ya akili,
maradhi ya minyoo, afya ya uzazi, maradhi ya kuharisha, maradhi ya kichaa cha mbwa, madhara ya pombe
na athari za unyanyapaa kwa wagonjwa wa UKIMWI, ugonjwa wa kisukari, shindikizo
la damu na ugonjwa wa kupooza. Aidha, uoneshaji wa filamu
inayohamasisha umuhimu wa kutumia choo inaendelea kuonyeshwa katika shehia 15
za wilaya sita za Unguja.
13.3.3 Mheshimiwa
Spika,
elimu ya afya pia iliendelea kutolewa maskulini ambapo jumla ya skuli 125 (80 kwa Unguja na 45 kwa
Pemba) zilipatiwa mafunzo kuhusu kinga ya maradhi mbali mbali. Aidha, uchunguzi
wa afya ya kinywa na meno kwa wanafunzi wa skuli za msingi Unguja na Pemba pia
ulifanyika. Jumla ya wanafunzi 3,420
walikaguliwa kati yao 1,437 (42%)
walionekana na matatizo mbali mbali ya meno hivyo kupatiwa matibabu pamoja na elimu
ya afya.
13.3.4Mheshimiwa Spika, nilieleza katika hotuba zangu zilizopita
kwamba Wizara ina nia ya kuanzisha redio maalumu kwa ajili ya kuelimisha jamii
masuala yanayohusu afya (Afya FM Redio). Hatua iliyofikia sasa ni kupatiwa
vyumba katika jengo jipya la Mradi wa Afya ya Uzazi na Mtoto lililopo Kidongo
Chekundu vitakavyotumika kwa ajili ya kufanyia matangazo yake.
13.3.5Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Mkakati wa Afya ya Jamii
(Community Health Strategy), mradi umetayarisha muongozo wa pamoja wa
utekelezaji wa Mkakati huu na muongozo wa kufundishia kamati Kiongozi za Afya
za Shehia. Kwa kuanzia Kamati Kiongozi za Afya za Shehia 30 zinatarajiwa kuundwa katika wilaya ya Mkoani na Magharibi,
mkutano wa uhamasishaji wa viongozi wa wilaya umefanyika na hatua za uundaji wa
kamati zinaendelea katika wilaya ya Magharibi.
13.3.5Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha matatizo mbali mbali ya afya yaliyomo katika
jamii yanaibuliwa mapema hasa katika maeneo ambayo
yako mbali na vituo vya afya na ni vigumu kufikika kwa urahisi, mradi umefanya
zoezi maalumu katika
Shehia ya Kandwi Wilaya ya Kaskazini A. Zoezi
hili limebainisha kwamba asilimia 31 ya wakuu wa kaya hawaelewi
muda wa kuhudhuria kliniki kwa mama wajawazito, akina mama wengi bado
wanajifungulia majumbani (76%), matumizi ya vyoo yako (51%) na
matumizi ya chumvi yenye madini joto (9%) tu ya kaya zote.
13.3.6Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/15 mradi umejipangia kutekeleza
kazi kuu zifuatazo:-
1. Kuunda na kuzifundisha
kamati kiongozi za Afya za shehia.
2. Kuongeza
kasi ya utoaji wa elimu ya afya katika jamii ili waweze kujiepusha na
vihatarishi vinavyopelekea kupata magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
13.4 Mradi Shirikishi
wa Afya ya Uzazi na Mtoto
13.4.1Mheshimiwa
Spika, mradi huu una lengo la kuimarisha afya ya
uzazi na mtoto pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Idadi ya vifo vya
uzazi vilivyotokea katika hospitali zetu kwa mwaka 2013 ni 103 (Unguja 68, Pemba 35) ambavyo ni ongezeko la vifo 37 kwa mwaka 2012. Sababu kuu zilizochangia
kutokea kwa vifo hivyo ni kutoka damu kwa wingi baada ya kujifungua (PPH), matatizo
ya shindikizo la damu “hypertensive disorder”, kutoka damu kwa wingi kabla ya
kujifungua, upungufu mkubwa wa damu na kupasuka kwa fuko la uzazi.
13.4.2Mheshimiwa
Spika,taarifa zinaonesha
kwamba, asilimia ya akina mama waliojifungulia katika vituo vya afya
imeongezeka kwa asilimia 7.2 kutoka 49.4% mwaka 2012 hadi kufikia 56.6 % ya
mwaka 2013. Nachukua fursa hii kuwapongeza kinamama na kina baba kwa kuwa na mwamko na kuuona
umuhimu wa kujifungua katika hospitali na vituo vya afya, pia nawaomba wazidi kuwa na moyo huu kwani inasaidia
kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya
mama na watoto kabla na baada ya kujifungua.
13.4.3Mheshimiwa
Spika, uzazi wa mpango ni
moja ya mikakati inayotumika katika kuimarisha afya ya mama na mtoto, taarifa
zinaonesha kwamba kina mama waliojiunga na uzazi wa mpango kwa njia za kisasa (new family planning
acceptance) kwa Unguja imepungua kutoka 6.6% (2012) hadi 5.5% (2013)
na Pemba imeonekana kuengezeka kutoka 3.1% (2012) hadi 6.9% (2013). Kwa Zanzibar hali inaonesha kuongezeka kutoka
5.3% (2012) hadi 5.8% (2013). Naomba kuchukuwa fursa hii kuwaomba
kinababa kutoa mashirikiano katika matumizi ya huduma hizi ili kuimarisha afya
ya mama na mtoto.
13.4.4Mheshimiwa
Spika, hatua ya akinamama
wajawazito kufika kwa wakati katika kliniki ni moja ya njia inayosaidia
kutambua mapema matatizo yanayowakabili hivyo kuweza kuchukua hatua za kufaa
kwa muda unaotakiwa. Kwa upande wa Pemba akinamama
waliopata huduma za ujauzito kabla ya wiki 16 (ANC visits before 16 weeks) imeongezeka kutoka 14.5% mwaka 2012 kufikia 23.4%
mwaka 2013. Kwa upande wa Unguja imeongezeka kutoka 20.8% mwaka 2012 hadi 22.8%
mwaka 2013. Kitaifa, hali pia imeonekana kuongezeka kutoka 19.5% (2012) hadi kufikia 21.3%
(2013). Ni vyema tukajenga tabia ya
kuwahimiza kinamama kufika hospitali mara tu watakapojibaini kuwa ni wajawazito
ili waweze kujua maendeleo ya afya zao na watoto walio tumboni.
13.4.5Mheshimiwa
Spika, jumla ya wajawazito 47,978
waliweza kuchunguzwa VVU katika kliniki na wodi za wazazi. Kati ya hao, kina mama wajawazito 171 waligundulika kuwa na VVU na jumla
ya kina mama wajawazito 158 walipewa
dawa za kupunguza makali ya VVU. Vile vile watoto 114 waliozaliwa
na mama wenye VVU walipewa dawa za nevirapin (NVP). Aidha, wenza/kina baba 880 waliweza kupimwa na kati yao kina
baba/wenza watano waligundulika kuwa na VVU.
13.4.6Mheshimiwa
Spika, kitaifa kiwango cha uchanjaji watoto chini ya mwaka mmoja
kimeongezeka kutoka 81% mwaka 2012
na kufikia 84.4% mwaka 2013. Wilaya
zote zimeweza kufikia asilimia zaidi ya 80 ya uchanjaji isipokuwa wilaya ya Magharibi Unguja ambayo imechanja 66.7% na wilaya ya Mkoani ambayo imechanja 56%. Kiambatisho namba 10
kinafafanua.
13.4.7Mheshimiwa Spika, jumla ya wagonjwa 664
wa surua wameweza kuripotiwa ambapo Wilaya za Mjini na Magharibi zimeoneesha
kuongoza kuwa na wagonjwa wengi zaidi. Asilimia 53.2 ya wagonjwa wote wa surua ni watoto chini ya umri wa miaka
mitano. Hii inaashiria kuwa wapo watoto
wengi ambao hawajachanjwa na wamo hatarini kuambukizwa. Wizara inaendelea
kutekeleza mkakati maalumu wa kuwafikia watoto wote. (Reach Every Child).
13.4.8Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 mradi umejipangia
kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1. Kutoa mafunzo ya IMCI kwa njia ya masafa,
mafunzo ya kuangalia maendeleo na makuaji ya mtoto na mafunzo ya huduma ya
watoto wachanga.
2. Kuinua kiwango cha chanjo zote kufikia zaidi ya
asilimia 90 kwa wilaya zilizo chini
ya lengo.
3.
Kuanzisha dozi ya pili ya chanjo ya surua (measles 2nd
dose) na kufanya kampeni ya surua.
4. Kuimarisha usimamizi, ufatiliaji na tathmini ya kazi
za chanjo katika ngazi zote.
5. Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa yanayokingwa
kwa chanjo (Surua, Pepopunda ya watoto wachanga na ulemavu wa ghafla) ili kufikia viwango na malengo
yaliyowekwa kimataifa.
13.5 Mradi wa Uimarishaji wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
13.5.1Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Mradi wa Uimarishaji wa
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali - Pemba maabara iliweza kuchora ramani na
kufanya makisio ya ujenzi. Jumla ya Tsh 16,000, 000/- zinahitajika kwa ajili ya
uchoraji wa ramani, Tsh. 22,535,000/-
zinahitajika kwa ajili ya uchunguzi wa udongo, na Tsh. 11,465,000/- kwa ajili ya kuzungusha uzio. Kwa mwaka wa fedha
2014/2015 Maabara imeazimia kujenga jengo la maabara ya Mkemia huko Pemba.
13.6 Mradi wa Kupandisha
Hadhi Hospitali za Wilaya na Vijiji
13.6.1 Mheshimiwa Spika, mradi huu umeanzishwa
kwa lengo la kuzipandisha hadhi hospitali za vijiji kuwa za wilaya na hospitali
mbili za wilaya kuwa za mkoa (Abdalla Mzee na Wete).
Hospitali za Wilaya
13.6.2Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ujenzi wa
hospitali ya Abdalla Mzee, wizara imeshalipa fidia kwa wamiliki wa nyumba,
mashamba na majengo ya ibada kwa wahusika ambapo jumla ya Tsh 900,000,000 zimetumika. Vile
vile mkandarasi kwa ajili ya ujenzi huu ameshapatikana na ujenzi
unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Hospitali za Vijiji
13.6.3Mheshimiwa Spika, ujenzi wa wodi ya
wanawake na wanaume katika hospitali ya Micheweni unaendelea ambao utaenda
sambamba na ujenzi wa chumba maalum cha upasuaji zimetumika. Aidha, matengenezo
ya nyumba za wafanyakazi, chumba cha upasuaji na ukarabati wa wodi za watoto
katika hospitali ya Kivunge yamefanyika.
13.6.4
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/15 mradi umejipangia
kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1. Kuendelea
na kazi ya ujenzi wa hospitali ya Abdalla Mzee.
2. Kuzipatia
hospitali vifaa na zana za tiba.
3. Kumalizia
ujenzi wa wodi ya wanawake na wanaume na chumba cha upasuaji katika hospitali
ya Micheweni.
13.7 Mradi
wa Kupandisha Hadhi Hospitali ya Mnazi Mmoja.
13.7.1Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, wizara kupitia mradi
huu imeanza ujenzi wa jengo litakalotumika kwa ajili ya huduma za upasuaji wa maradhi ya mgongo na ubongo
(neurosurgical services). Ujenzi
unatarajiwa kumalizika Oktoba mwaka 2014. Kumalizika kwa ujenzi wa jengo
hilo litakalokuwa na chumba cha upasuaji, chumba cha ICU na wodi za wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji kutaimarisha upatikanaji wa huduma hii na kuwapunguzia
wananchi na serikali gharama za kupeleka wagonjwa wa maradhi hayo nje ya nchi. Kitengo hiki kitasaidia kuwapatia ujuzi
madaktari wetu pindi wakiwa kazini.
13.7.2 Mheshimiwa Spika, moja kati ya changamoto
niliyoieleza katika hotuba
ya Wizara ya mwaka 2013/14 ni kukosekana kwa mtambo wa kuchomea takataka za hospitali
(Incenerator), napenda kuwaarifu wajumbe wa Baraza lako kuwa, wizara
imefanikiwa kununua kifaa hicho, tayari kimeshafungwa na kinaendelea kufanya
kazi.
13.7.3Mheshimiwa Spika, mradi wa Orio unaoendeshwa kwa mashirikiano na
Serikali ya Uholanzi tayari umeanza
utekelezaji wake kwa kutangaza zabuni za ujenzi. Wakandarasi
watatu tayari wamepatikana na
wameshapewa nyaraka za zabuni ili ziweze kutathminiwa. Kazi hiyo itahusisha ujenzi wa kliniki za maradhi maalumu, wodi ya kina
mama ya kujifungulia na baada ya kujifungua na chumba cha huduma za dharura
(Emergency Units/casuality). Eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi huu ni
katika majengo ya zamani ya kiwanda cha dawa kilichopo katika eneo la hospitali
ya Mnazi Mmoja.
13.7.4Mheshimiwa Spika, ujenzi
mwengine unahusisha wodi mpya ya watoto itakayokuwa na sehemu ya kutibu wagonjwa wenye maradhi ya figo (Dialysis).
Ujenzi huu unatarajiwa kuanza mwezi wa Julai 2014, tayari ramani ya jengo
imeshatengenezwa, zabuni imeshaitishwa na mkadandarasi ameshapatikana na
kukabidhiwa kazi hiyo.
13.7.5Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2014/15, mradi unatarajia kutekeleza kazi kuu zifuatazo:-
1.
Kukamilisha
ujenzi wa jengo litakalotoa huduma za upasuaji wa maradhi ya uti wa mgongo na
ubongo (neurosurgical services).
2. Kuendelea na ujenzi wa jengo la watoto lenye sehemu ya matibabu ya
maradhi ya figo (Dialysis)
3. Kuanza
ujenzi wa jengo la kliniki
za maradhi maalumu, wodi ya kina mama ya kujifungulia na baada ya kujifungua na
chumba cha huduma za dharura (Emergency Units/casuality).
4. Kulifanyia
matengenezo jengo la kutolea huduma za matibabu ya macho.
13.8 Mradi wa Kusaidia
Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi
13.8.1Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kusaidia
Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi umetekelezwa kupitia Mkopo kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB). Mradi huu umetelekezwa kwa awamu ya kwanza kwa
kipindi cha miaka mitano (2007-2012). Awamu ya pili ilianza Januari 2013 - June
2014, kipindi ambacho mradi uliongezewa muda wa mwaka mmoja na nusu.
13.8.2Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
nyongeza mradi uliweza kufanikisha kazi za ujenzi wa kituo cha afya na nyumba ya
wafanyakazi Mzambarauni Pemba. Kwa upande wa Unguja ujenzi wa kituo kipya cha
afya Mwera, nyumba ya wafanyakazi pamoja na matengenezo makubwa ya kituo
kikongwe ambacho kitatumika kwa ofisi za afya wilaya ya kati ulifanyika. Mradi
pia uliweza kufanya utanuzi na matengenezo ya jengo la wodi ya wazazi na watoto
katika hospitali ya Wete. Aidha, ununuzi wa vifaa kwa ajili ya wodi ya wagonjwa
wa akili (Mental Wing) katika hospitali ya Wete umefanyika.
13.9 Mradi wa Chuo cha
Madaktari Zanzibar (Zanzibar Medical School)
13.9.1Mheshimiwa
Spika, Chuo cha Madaktari kinachoendeshwa kwa
mashirikiano na Chuo Kikuu cha Matansus cha Cuba kimeendelea kutoa mafunzo ya
udaktari kwa wanafunzi (Unguja 38 na Pemba 12), mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano mkubwa na madaktari
wazalendo wa hapa Zanzibar.
13.9.2Mheshimiwa
Spika, chuo hiki kimepata mafanikio makubwa kwani
tayari kinatambuliwa na Taasisi ya Umoja wa Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuvifanyia matengenezo vifaa
mbali mbali kama vile “photocopy mashine” na computer pamoja na kuboresha
miundombinu ya mawasiliano ya “internet” katika eneo la chuo, ili kuleta
mazingira mazuri ya kujifunza. Aidha, wanafunzi 38 kwa Unguja wanatarajia kumaliza masomo yao ifikapo Julai, 2014.
13.9.3Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 wizara itahakikisha
kwamba wanafunzi 12 wa udaktari waliopo mwaka wa tano Pemba wanaendelea vizuri
kimasomo kwa kuwapatia nyenzo zote zitakazohitajika katika masomo yao.
13.10 Mradi wa
Kuimarisha Huduma za Afya Wilayani
13.10.1Mheshimiwa Spika,
mradi huu unatekelezwa kupitia mfuko wa fedha wa pamoja ‘Basket Fund’ ambao
hupata fedha zake kutoka Serikalini na washirika wa maendeleo. Katika utekezaji
wake mradi umelenga kusaidia maendeleo ya afya wilayani ambapo kila wilaya
hulazimika kuandaa mpango kazi kulingana na mahitaji na vipaumbele vya wilaya
husika.
13.10.2Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kamati za afya za wilaya Unguja na Pemba zilipata
mafanikio makubwa; mafanikio hayo ni pamoja na kuchimba visima kwa ajili ya
Kituo cha Afya cha Kwamtipura na Chumbuni, kukipatia umeme kituo kipya cha
Pwani Mchangani na vituo sita vya Wilaya Kaskazini “A” vilipatiwa matangi mapya
ya maji. Wakati huo huo, matengenezo ya sakafu, madirisha, mapaa, milango na
sehemu ya kuhifadhia dawa yalifanywa katika vituo vya Donge Mchangani, Mtende,
Muyuni na Muungoni.
13.10.3Mheshimiwa Spika,
matengenezo mengine yaliyofanywa ni kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya Bwagamoyo
pamoja na kufanyiwa matengenezo madogo madogo kwa vituo vya Kiwani, Vumba,
Junguni na Minungwini. Aidha, kituo cha afya cha Mgelema kimefanyiwa “fitting”
ya umeme na kupatiwa maji, pia ujenzi wa mashimo maalum ya kutupia mazalio
kwenye vituo vya Wingwi, Maziwa ng’ombe na Tundauwa ulifanyika.
13.10.4 Mheshimiwa Spika, kazi
nyengine iliyofanywa na mradi huu ni kununua vifaa vya usafi na kuvisambaza
katika vituo vyote vya afya. Kuwepo kwa vifaa hivi kumeongeza usafi katika
vituo hivyo. Aidha, wilaya zimeweza kulipia bili za umeme na maji katika vituo
vyote vya afya jambo ambalo limeleta faraja kwa uendeshaji wa vituo hivyo; hata
hivyo wizara bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kulipishwa umeme na maji
kama ni taasisi za kibiashara na hivyo kukwamisha hatua za kumaliza madeni ya
umeme yanayotukabili.
13.10.5 Mheshimiwa Spika, kazi
za utoaji wa huduma za mkoba za chanjo zimeendelea kutolewa katika maeneo
ambayo ni tabu kufikika kirahisi. Huduma hizi zimechangia sana kuongeza kiwango
cha chanjo na kufikia asilimia 84.4 kutoka
asilimia 81 ya mwaka 2012.
Halkadhalika, ushirikishwaji na uhamasishaji wa jamii juu ya utoaji wa huduma
za afya za mama na mtoto kwa wasambazaji wa dawa za mpangilio majumbani, wakunga
wa kienyeji, masheha pamoja na utoaji wa elimu ya afya mashuleni kuhusu afya
ya kinywa na meno umefanyika.
13.10.6Mheshimiwa Spika,
moja ya mkakati unaotumiwa na wizara katika kufikisha huduma za afya kwa jamii
ni kuendesha siku za afya vijijini. Katika siku hizi huduma mchanganyiko zilitolewa
ikiwemo elimu ya afya, uchunguzi wa macho, afya ya kinywa na meno, masikio, koo
na pua, Kifua Kikuu na Ukoma, upimaji wa hiari wa VVU (VCT), Shindikizo la damu,
kutoa matibabu na rufaa kwa wale ambao
wana matatizo zaidi. Huduma hizi zimetolewa katika shehia tofauti katika wilaya
zote kumi.
13.10.7 Mheshimiwa Spika, kama
nilivyoeleza hapo awali kuwa kila wilaya husika hupanga mpango kazi kulingana
na mahitaji yake. Katika mwaka 2013/14 wilaya ya Micheweni, Chakechake na Wete
zilipanga kuongeza idadi ya vyoo katika jamii. Kwa kufanikisha suala hilo
wilaya hizo zilinunua vifaa na kuzipatia familia zote zilizoamua kuchimba vyoo.
Jumla ya mashimo ya vyoo 150
yalichimbwa katika wilaya ya Micheweni, 130
Wete, na jumla ya vyoo 75 vilichimbwa
kwa Wilaya ya Chake.
14.0 CHANGAMOTO
14.1 Mheshimiwa Spika, wizara
katika utekelezaji wa majukumu na malengo yake imekuwa ikikabiliwa na
changamoto za aina mbali mbali. Baadhi ya changamoto hizo zinahitaji
mashirikiano yetu sote kuzipatia ufumbuzi.
14.2 Mheshimiwa Spika, moja
ya changamoto inayoikabili sekta ni ongezeko la maradhi yasiyoambukiza yakiwemo
maradhi ya kisukari, saratani, shindikizo la damu na athari zinazotokana na ajali
za barabarani. Ukuaji wa maradhi haya yenye gharama kubwa ya matibabu umeathiri
uwezo wa sekta kuwahudumia wanaopatwa na maradhi haya. Aidha, mapambano dhidi
ya magonjwa yasiyoambukiza kuendelea kuonekana kama jukumu la sekta ya afya
pekee na ugumu wa wananchi kutobadili mfumo wa maisha ikiwemo kuacha kufanya
mazoezi, utumiaji wa vyakula visivyo mlo kamili (Balance Diet) na kutopima afya
zetu mara kwa mara.
14.3 Mheshimiwa Spika, changamoto
nyengine inayotukabili ni kuibuka kwa wauzaji wasio rasmi wa dawa za asili mitaani
na katika sehemu za ibada jambo ambalo linaathiri juhudi za wizara katika kuimarisha
na kustawisha huduma za tiba asili hapa nchini. Aidha, kuwepo kwa waganga
wanaojitangaza katika vyombo vya habari kinyume na taratibu za afya kuwa wanatibu
maradhi fulani kunakwamisha juhudi hizi.
14.4 Mheshimiwa Spika,
zipo changamoto ambazo hujitokeza kila mwaka kwa mfano, kukosekana au kuchelewa
kupata fedha kumeendela kuathiri upatikanaji wa vitendea kazi kunakopelekea
kuzorota au kukosekana kabisa baadhi ya huduma zetu kwa jamii. Vitendea kazi hivyo ni pamoja na usafiri,
mafuta, dawa, vifaa vya tiba na kinga.
Aidha, hali hii imeathiri matengenezo na upanuzi wa majengo hasa vituo
vya afya, kutokana na kujengwa zamani na udogo wake kulingana na kutanuka kwa
huduma zinazotolewa.
14.5 Mheshimiwa Spika, pamoja
na jitihada za serikali kuajiri na kupeleka masomoni wafanyakazi wake, wizara
bado inakabiliwa na tatizo la uhaba wa wataalamu hali inayoathiri utoaji wa
huduma kwenye hospitali na vituo vya afya.
14.6 Mheshimiwa Spika,
hali ya lishe kwa wananchi wa Zanzibar bado si ya kuridhisha hususan kwa mama
wajawazito na watoto. Hali hii inachangiwa na kuwepo kwa upungufu wa matumizi
ya vyakula vyenye virutubishi wakati wa kipindi cha ujauzito, unyonyeshaji,
ulishaji usio sahihi kwa watoto na matunzo hafifu ambayo hupelekea lishe duni.
15.0 MALENGO MAKUU YA WIZARA YA AFYA KWA MWAKA WA
FEDHA 2014/2015
15.1 Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2014/2015 kazi kuu zilizopangwa kutekelezwa na Wizara ya Afya ni
pamoja na:-
1.
Kuendelea
na mchakato wa kuanzisha vyanzo mbadala vya upatikanaji wa rasilimali fedha ikiwemo
Bima ya Afya.
2.
Kuongeza
upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa hospitali na vituo vya afya
vya Serikali.
3. Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na
tathmini katika sekta ya afya.
4. Kuimarisha miundombinu ya afya
ikiwemo:-
a.
Ujenzi wa
jengo la watoto lenye sehemu ya matibabu ya maradhi ya figo (Dialysis), katika
hospitali ya Mnazi Mmoja
b.
Kuanza
ujenzi wa jengo la kliniki za maradhi maalumu, wodi ya kina mama ya
kujifungulia na baada ya kujifungua na chumba cha huduma za dharura (Emergency
Units/casuality) katika hospitali ya Mnazi Mmoja
c.
Kulifanyia matengenezo jengo la macho katika
Hospitali ya Mnazi Mmoja
d.
Kujenga jengo la kutolea huduma kwa waathirika wa
madawa ya kulevya (Detoxification Centre) katika hospitali ya Kidongo Chekundu.
e.
Kuendelea na ukarabati wa majengo na vituo vyote vya
afya.
5.
Kuimarisha
huduma za afya kwa jamii ili kupunguza maradhi ya kuambukiza na yasiyo ya
kuambukiza.
6. Kutayarisha
na kupitia miongozo mbali mbali kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za afya.
7. Kuanzisha
mfumo wa kupima utendaji wa wafanyakazi (Performance Appraisal System).
16.0 HITIMISHO
16.1 Mheshmiwa Spika, mafanikio
yaliyopatikana hayatokani na juhudi za wizara ya afya na sekta ya watu binafsi
tu, bali pia kwa mashirikiano, ushauri na misaada ya hali na mali kutoka
mashirika ya kitaifa na kimataifa pamoja na nchi marafiki, taasisi za serikali
na siziso za serikali, wananchi wa ndani na nje ya nchi. Wizara inawashukuru kwa dhati kubwa na
inawaomba wasichoke kwani misaada yao ina thamani kubwa kwetu. Shukrani makhsusi
ziende kwa Serikali ya Denmark, Cuba, Marekani, India, China, Korea, Hispania, Uingereza,
Urusi, Omani, Israili, Uholanzi, Norway na Uturuki.
Aidha,
shukurani zetu pia ziende kwa mashirika mbali mbali yakiwemo ADB, CDC, CLINTON
FOUNDATION, DANIDA, WHO, PEPFAR, USAID, GLOBAL FUND, ITALIAN COOPERATION, SAVE THE
CHILDREN, IVODE CARENER FOUNDATION, JHIEPIGO, UNICEF, UNFPA, WDF, UNDP, SIGHT
SAVERS, PATH FINDER, ICAP, SCORE/ZEST, HIPZ, PROJECT HOPE, KOICA na wale wote ambao sikuweza kuwaorodhesha kwenye
hotuba hii.
16.2 Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 wizara imepangiwa kuchangia Tsh 124,000,000 na kwa Hospitali ya Mnazi Mmoja
imepangiwa kuchangia Tsh 550,000,000
na kuingiza katika mfuko mkuu wa serikali.
Kiambatisho namba 11 kinatoa ufafanuzi. Pia wizara kupitia SMZ imepangiwa
kutumia Tsh 7,253,200,000 kwa kazi
za kawaida, Tsh 1,219,200,000 ruzuku
na Tsh 14,274,800,000 kwa mishahara
na maposho. Kiambatisho namba 12 kinatoa
ufafanuzi. Kwa upande wa kazi za maendeleo wizara imepangiwa kutumia Tsh 3,850,000,000 kutoka Serikalini na Tshs
24,356,897,000 ambazo ni misaada
kutoka washirika wa maendeleo. Kiambatisho
namba 13 kinatoa ufafanuzi.
16.3 Mheshimiwa Spika, naomba
Baraza hili liipokee na wajumbe waijadili hotuba yangu, kutoa ushauri na hatimae
kuipitisha ili wizara ipate uwezo wa kuwahudumia wananchi kupata huduma bora za
afya kwa wepesi. Baada ya maelezo hayo naomba Baraza hili liidhinishe jumla ya
Tsh 22,747,200,000 kwa kazi za
kawaida, ruzuku, mishahara na maposho, pia naomba Baraza lako liidhinishe jumla
ya Tsh 8,282,000,000 kwa ajili ya
hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matumizi ya kawaida mishahara na maposho. Kwa
upande wa kazi za maendeleo baraza liidhinishe jumla ya Tsh 3,850,000,000 kutoka mfuko mkuu wa
serikali na Tsh 24,356,897,000
kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Kwa
heshima kubwa na taadhima, kwa idhini yako NAOMBA
KUTOA HOJA.
MHESHIMIWA JUMA DUNI HAJI
WAZIRI WA AFYA,
ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment