Habari za Punde

Mfungwa abaka mwanafunzi

Na Fatina Mathias, Dodoma
MFUNGWA Julius Tito (48) maarufu Madilu ameshtakiwa kwa kosa la kubaka mtoto mwenye umri wa miaka 10 (jina limehifadhiwa) katika eneo la kambi ya polisi mjini Dodoma na kesi yake inatarajiwa kutajwa  tena Julai 8 mwaka huu.

Akitoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo bungeni jana, Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe, alisema mfungwa huyo alikuwa akitumikia kifungo katika gereza la Isanga kwa kosa la kulawiti alilolifanya mkoani Singida.

Alisema akiwa katika gereza hilo alionesha nidhamu ya hali ya juu na hatimaye kupewa cheo cha unyampala.

“Kwa hiyo akaaminiwa na kupewa cheo cha unyampala mle ndani siku moja wakuchukuliwa yeye na wenzake wawili kwenda kufanya kazi kwenye kambi ya polisi iliyopo mjini Dodoma hapo ndipo alipotenda tendo hilo la kumbaka mtoto wa miaka 10 mwanafunzi wa skuli ya msingi iliyopo mjini Dodoma,” alisema Chikawe.


Alisema mfungwa huyo amekamatwa na kwa sababu alikuwa bado anatumikia kifungo cha kosa lake la kwanza  gerezani hapo kilichotokea alipelekwa mahakamani na kushitakiwa kwa kosa hilo la kubaka.

“Kesi yake ni kesi ya jinai namba 106 ya mwaka huu na itatajwa tena tarehe nane ya mwezi ujao,” alisema.

Aidha alisema kumekuwepo na watu wakidhani kwamba labda magereza imezuia mtu huyo asishitakiwe .

Hata hivyo, alisema askari ambao walikuwa wamewachukua kuwapeleka katika kazi hiyo nao pia wamechukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria ya jeshi la polisi ikiwa ni pamoja na kufunguliwa mashtaka ya kijeshi.

Alisema sio kweli kuwa Wizara haifanyi lolote kuhusu jambo hilo kwani tayari hatua zimechukuliwa.

Mfungwa huyo alianza kutumikia kifungo mwaka 1998 akiwa na miaka 31 na alitarajiwa kumaliza kifungo chake tarehe 14/6/2018 hivyo alikuwa amebakiza miaka minne.

Alipewa cheo cha unyampala mwaka 2000 baada ya kuonesha nidhamu ya hali ya juu na pia alikuwa akishiriki katika shughuli za ujenzi.

Madilu alikuwa ni miongoni mwa genge la mafundi ujenzi ambao walikuwa wakiruhusiwa wakiwa katika ulinzi kusaidia shughuli mbali mbali za ujenzi.


Siku ya tukio mfungwa huyo alikuwa akijenga chumba cha kuhifadhia silaha katika kambi ya polisi.      

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.