Na.Ameir Khalid na Mwanrafia Kombo
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Omar Yussuf Mzee,
amesema watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) upande wa Tanzania
Bara,wanasababisha mgogoro wa makusudi kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya Mwakilishi wa
Kikwajuni, Mhe. Mahmoud Mohammed Mussa, kuhusu makontena ya Zanzibar yaliyozuiliwa
bandarini Dar es Salaam na kitendo cha kuletwa wafanyakazi saba wa TRA
kufuatilia makontena hayo wakati akichangia bajeti ya wizara ya Biashara, Viwanda
na Masoko, Waziri huyo alisema TRA Tanzania Bara wana tatizo lakini hawalisemi,
hali inayosababisha mgogoro mkubwa.
Hata hivyo, alisema wataendelea kutafuta
kiini cha tatizo hilo kwa mazungumzo na ikishindikana watatumia Kamati ya kero
za Muungano.
Aidha alisema wizara inasubiri majibu kutoka
TRA Zanzibar kuhusu wafanyakazi wa TRA Tanzania Bara kutumwa kuchunguza
makontena hayo, baada ya kupokea malalamiko kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara,
Wenyeviwanda na Wakulima (ZNCCIA) kuhusu kitendo hicho cha TRA.
Mapema Mbunge huyo wa Kikwajuni, alisema
wafanyakazi hao wa TRA walitumwa kufuatilia makontena hayo na kuyapekuwa kujua
kilichomo ndani na kuripoti makao makuu na kuhoji utaratibu huo utaendelea hadi
lini.
Alisema makontena hayo yalifika bandarini Dar
es Salaam tokea Juni 5, lakini yalikuwa yakizuiliwa na TRA kwa utashi wao tu na
kwa lengo la kudhoofisha biashara ya
Zanzibar.
Wakichagia bajeti hiyo,Wawakilishi walieleza
kusikitishwa kwao kufa kwa viwanda vya ndani, hali iliyosababisha ukosefu mkubwa
wa ajira kwa vijana.
Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Mhe. Saleh
Nassor Juma, alisema Zanzibar ilikuwa na viwanda vingi muda mfupi baada ya
mapinduzi, lakini vyote vimekufa na kudhoofisha mfumo wa ajira kwa vijana.
Aidha aliitaka wizara hiyo kutafuta ufumbuzi
wa moshi nzito unaotoka katika kiwanda cha makonyo Wawi, ambao unasababisha
athari za kiafya kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo Tumbe,
Mhe.Rufai Said Rufai, aliitaka serikali kuimarisha viwanda ili kukuza uchumi.
Akitoa majumuisho, Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe.
Thuwaiba Kisasi, aliwataka wafanyabiashara kuwa na moyo wa huruma kwa wananchi
katika kipindi hichi wakijiandaa na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema serikali ilitoa msamaha wa kodi kwa
wafanyabiashara wa chakula, kwa lengo la kuuza bidhaa zao kwa wananchi kwa bei
nafuu, lakini misamaha hiyo hawaisaidii walaji na kuendelea kununua bidhaa kwa
bei ya juu.
Kuhusu kodi mara mbili, Waziri wa wizara
hiyo, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alisema bado tatizo hilo linaendelea kwa wafanyabiashara
wa Zanzibar.
Alisema wapo baadhi ya wafanyakazi wa TRA
ambao kwa makusudi wanataka kudhoofisha Muungano na kufanya ubaguzi baina ya wafanyabiashara wa
Zanzibar na Tanzania Bara jambo ambalo halifai kwani linaweza kuleta athari
kubwa siku za baadae.
Kuhusu kufungwa kiwanda cha kuzalisha
vinywaji baridi cha Coca Cola Zanzibar, alisema kiwanda hicho kimesitisha
uzalishaji kutokana na mitambo yake kuchakaa na hofu waliyonayo wamiliki wa
kampuni hiyo kwamba kikiachiwa kuendelea kuzalisha kinaweza kuzalisha bidhaa
zisizo na ubora.
Hata hivyo, aliwatoa hofu Wawakilishi kwamba
serikali inaendelea kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho na kwamba mitambo
iliyopo ndani ya kiwanda hicho ni mali ya kampuni lakini majengo ni ya
serikali.
Hivyo, kama kampuni hiyo itashindwa kufanya
uzalishaji, serikali itatafuta mwekezaji mwengine.
Wajumbe wa baraza hilo walichangia bajeti ya
wizara hiyo baadae wakaipitisha.
No comments:
Post a Comment