Habari za Punde

balozi Seif Aipongeza Timu ya Ujamaa kwa Kupanda Daraja.

 Rais wa Klabu ya Ujamaa ya Rahaleo Othman Mussa akielezea mikakati ya Timu yake kushiriki mashindano ya 12 bora daraja la Pili Unguja mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.kushoto ya Othman Mussa ni mwenyekiti wa Klabu ya Ujamaa Ameir Makungu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiipongeza timu ya soka ya Ujamaa baada ya kupanda daraja ligi daraja la Pili Wilaya ya Mjini.
 Balozi Seif akiwa na Kombe la Ubingwa Daraja la Pili Wilaya ya Mjini, akifurahia baada ya kukabidhiwa Ofisini kwake na Uongozi wa timu ya Ujamaa baada ya kulitowa Kombe hilo la Ubingwa lililonyakuliwa na wakongwe wa Soka Unguja Timu ya Ujamaa daraja la pili Wilaya ya Mjini.wa mwanzo kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar { BTMZ } Sharifa Khamis na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi akiwa pia muasisi wa Timu pinzani dhidi ya Ujamaa Timu ya Muembeladu { Kubwa Lijalo } Mh. Abdulla Mwinyi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiipongeza timu ya soka ya Ujamaa baada ya kupanda daraja ligi daraja la Pili Wilaya ya Mjini.
Balozi Seif, akisalimiana na Viongozi wa Timu ya Ujama walipofika Ofisini kwake kumkabidhi Kombe la Ubingwa wa Wilaya ya Mjini kwa kuwa Mabingwa wa Ligi Hiyo kwa Mwaka 2014.

Othman Khamis Ame
Timu Kongwe ya Mchezo wa Soka hapa Zanzibar Ujamaa Sports Club imejizatiti kurejea tena kwenye ligi kuu ya Zanzibar Daraja la Kwanza baada ya kuteremka kiwango chake na kufikia hadi Daraja la Tatu mwaka 2013.

Rais wa Klabu ya Ujamaa yenye mastakimu yake Mtaa wa Rahaleo Mkabala na Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC – Redio } Othman Mussa alieleza hayo Wakati Uongozi pamoja na baadhi ya wachezaji wa Timu hiyo ulipofika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kumsalimia baada ya kutawadhwa rasmi kuwa mabingwa wa Soka Daraja la Pili Wilaya ya Mjini.

Othman Mussa  alimueleza Balozi Seif ambae pia ni Mchezaji wa Zamani wa Klabu hiyo kwamba ipo dalili kubwa kwa timu hiyo kongwe kupanda daraja na kufikia malengo kutokana na ari na mashirikiano makubwa yaliyopo kati ya wachezaji na Viongozi wa Klabu hiyo.

Hata hivyo Rais huyo wa Klabu ya Ujamaa alieleza kwamba zipo baadhi ya changa moto zinazoikabili timu hiyo kwa hivi sasa ikiwa ni pamoja na gharama za huduma kwa vile wako katika maandalizi ya kujenga kambi kwa ajili ya kukabiliana na fainali ya mashindano ya  timu 12 Bora za soka Wilaya za Unguja.

Naye Katibu Mkuu wa Klabu ya Ujamaa Juma Khalfan alieleza kwamba Timu hiyo ilifikia hatua ya ubingwa baada kazi kubwa ya mashindano ya ligi ya soka ya Daraja la Tatu iliyozikutanisha takriban Timu 22 zilizomo ndani ya Wilaya ya Mjini.

Juma Khalfan alifahamisha kwamba klabu ya Ujamaa ambayo ina historia ndefu ya mchezo wa soka  hapa Nchini iliwahi kuchukuwa ubingwa wa Zanzibar wa mchezo huo katika miaka ya nyuma.

Akitoa shukrani zake kufuatia ubingwa huo walioupata Klabu ya Ujamaa wa Soka Wilaya ya Mjini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Uongozi na Wachezaji wa Timu hiyo bado wana kazi kubwa ya kuhakikisha hadhi ya timu hiyo kisoka inarejea tena.

Balozi Seif alisema aliwasisitiza wachezaji wa timu hiyo kudumisha nidhamu wakati wanapokuwa michezoni kwa kutii uamuzi wa wachezeshaji soka ili lengo la kuimarisha uanamichezo lifanikiwe vyema.

“ Itapendeza na kufurahisha iwapo itafikia wakati timu yetu inatoa wachezaji wa Kitaifa na Kimataifa. Kwa nini wachezaji wetu wasifikie kiwango cha akina drogba, Eto, Song na wengineo wanaotoka ndani ya Bara la Afrika ? “. Aliuliza Balozi Seif.

Alisema kwa vile wachezaji wa Timu hiyo wameshaamua kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya 12 bora Daraja la Pili Kanda ya Unguja ataangalia uwezekano wa kuongeza nguvu zake ili wafikie lengo walilojiwekea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.