Na Husna Mohammed
WAKULIMA wa mpunga mkoa wa kaskazini
Unguja, wamesema msimu wa mavuno ya mpunga kwa mwaka huu ni mabaya ikilinganishwa
na miaka iliyopita.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
gazeti hili, wakulima hao walisema sababu kubwa ya mavuno ya zao hilo kuwa mabaya ni mashamba yao kuvamiwa na viwavi jeshi pamoja na
kunguni mgumba.
Pandu Mtumwa na Mwajuma Kombo wa kijiji
cha Kinyasini, ambao wanalima katika bonde la Kibokwa, walisema pamoja na
uvamizi wa wadudu hao, pia Idara husika ilichelewa kuwapa dawa za kuuliwa
wadudu.
“Mabwana na mabibi shamba walikuja lakini
walisema kuwa kama watapeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi watachelewa lakini
pia walisema wadudu hao ni wagumu wa kufa,” walisema.
Hata hivyo, walisema wako baadhi ya
wakulima walipata kunyunyuziwa dawa huku tayari viwavi hivyo vilikwishaleta
athari kubwa ya zao hilo .
Aidha Mwandiwe Makame Ali, mkaazi wa
Chaani kubwa, alisema mpunga karibu
ekari moja aliyolima umevamiwa na viwavi jeshi.
“Mpunga wangu ulikuwa mzuri sana lakini ulipovamiwa
na viwavi jeshi ulikufa mwingi na mchache uliochipua hakuzaa vyema,” alisema.
Nae Mwandiwe Makame Ali wa kijiji cha
Chaani kubwa, alisema yeye ni miongoni mwa wakulima wa mpunga walioathiriwa
viwavi jeshi katika konde yake.
“Kwa kawaida nalima nusu ekari na kuvuna
vipolo hadi 15 lakini kwa mwaka huu naona mavuno yatakuwa mabaya sana kwani
hata nikipata basi itakuwa polo nne hadi
tano,” alisema.
Akizungumzia kuhusu dawa za kuulia
wadudu, alisema licha ya kufika bibi shamba lakini hakuna huduma iliyotolewa ya
kuua wadudu hao.
“Bibi shamba ni hodari kwani
anatutembelea mara kwa mara lakini hakuna msaada tuliopata kwa ajili ya kuulia
wadudu hawa na ndio maana wakatuathiri sana,” alisema.
Kwa upande wake, mkaazi wa kijiji cha
Mkokotoni, Hadia Makame, anaelima bonde la
Fungu refu, alisema eneo hilo halikuathiriwa na viwavi jeshi lakini
aliomba Idara husika kuwapatia mbegu na mapema na dawa ya kuulia wadudu na
magugu wakati muafaka.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ ,Riziki
Simai, akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Gamba, alikiri wakulima kuvamiwa
kwa viwavi jeshi na kunguni mgumba .
“Kwa kweli msaada wa serikali kwa mwaka
huu haukuwa mzuri kwani wakulima wengi mpunga wao uliathiriwa na wadudu na kwa
wakati uliobaki hawakuwa na mbegu wala mbolea na kusababisha wengine hawakupanda tena mpunga,”
alisema.
Aliyataja mabonde yaliyoahiriwa na wadudu
hao kuwa ni pamoja na bonde la Mvivu, Kilombero, Kibokwa, Upenja , Pangeni na
mto wa maji.
Mapema Naibu Waziri wa Kilimo na
Maliasili Zanzibar, Mtumwa Kheir Mbarak, aliliambia baraza la wawakilishi kwamba
viwavi jeshi vilivamia mashamba mengi ya mpunga hasa Unguja.
Alisema karibu eka ri 400 za mpunga
wilaya ya Kati na Kaskazini ‘A’ zimevamiwa na wadudu hao.
No comments:
Post a Comment