Na Fatina Mathias, Dodoma
JAMII nchini imetakiwa kutambua kuwa
wakimbizi na wahamiaji wasio rasmi, wana haki ya kuhudumiwa, kusikilizwa na
kusimamiwa kama walivyo binadamu wengine.
Mbali na hilo pia wanatakiwa kuelimishwa juu ya
umuhimu wa kuwa na vibali vya kuingia nchi nyingine.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Mafunzo kwa
Vitendo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), anayehusika
na Usalama , Nicholas Gichubiri ,wakati akitoa semina kwa waandishi wa habari mkoa
wa Dodoma iliyohusu masuala ya wakimbizi na wahamiaji iliyoandaliwa na shirika
hilo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Wahamiaji(IOM).
Alisema jamii inapaswa kupewa elimu juu
ya sheria za mipaka ya nchi ili kuzuia mkanganyiko unaoweza kujitokeza baina ya
nchi na nchi ama wananchi husika ikiwa ni pamoja na kutafuta njia nzuri
itakayosaidia kutohalalisha kundi hilo
kuingia nchini.
Kwa upande wake , Ofisa miradi taifa, Charles
Mkude, aliwaasa waandishi wa habari kufanya uchunguzi wa kina juu ya habari
wanazozitoa kuhusiana na masuala ya wakimbizi na wahamiaji wasio rasmi ili
kuepuka kuwa midomo ya kusemea watu.
Alisema ni vyema wanahabari wakajiuliza
maswali ya ziada kwa kile wanachoambiwa juu ya wakimbizi ama wahamiaji
wanaoingia nchini ikiwa ni pamoja na kujua sababu za wao kuingia nchini kabla
ya kuandika habari zao ili kuleta maana kamili ya habari hiyo.
Aidha aliwataka kuwa na uelewa wa kutosha
wa lugha za kimataifa hasa kiingereza ili kuleta urahisi katika utendaji wa kazi
zao.
No comments:
Post a Comment