Habari za Punde

Dk. Karume ahimiza walimu, wazazi kushirikiana



Na Bakar Mussa, Pemba
RAIS mstaafu wa awamu ya sita, Alhaj Dk. Aman Abeid Karume, amewataka wazazi kuongeza ushirikiano na walimu wa madrasa ili kuwaendeleza watoto katika kuhifadhi na kusoma Quran.

Alisema bila ya ushirikiano lengo la kuendeleza mbele juhudi zinazochukuliwa na waalimu wa madrasa za kuendeleza dini hiyo hazitazaa matunda.

Aliyasema hayo katika msikiti wa Ijumaa wa Miembeni Chake Chake kisiwani Pemba,wakati akizungumza na walimu, wazazi na wanafunzi, walioshiriki mashindano ya kuhifadhi Quran ambapo alikuwa mgeni rasmi.


Aliwapongeza walimu waliofanya kazi ya kuwaandaa watoto katika suala zima la kuhifadhi Quran, kwa vile kazi walioifanya ni kubwa na inataka ujasiri na ustahamilivu.

Alisema wanachokifanya walimu hao ni muendelezo wa historia ya Zanzibar kuwa itovu cha elimu ya dini na dunia.

Aliwataka walimu kuwa kitu kimoja kuliendeleza hilo na kuwataka wengine kuisoma historia ya Zanzibar ili waone jinsi Wazanzibari  walivyoanza kuwa  chem chem ya elimu.

Aliwataka viongozi kumaliza changamoto zinazowakabili kwani matatizo ni sehemu ya maisha ya jamii.

Aliwasihi wanafunzi kuwa tayari kujiendeleza na kwa wale ambao walishindwa basi wasivunjike moyo wajitahidi kwa mara nyengine kwani wanapoisoma dini yao matunda yake watayaona.

Mapema akisoma risala ya jumuiya hiyo, kiongozi wa jumuiya hiyo, Nassor Abdalla Nasor, alisema jumuiya inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa ofisi  na vitendea kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.