Habari za Punde

Fedha za TASAF si za anasa, kaya maskini zaambiwa



Na Haji Nassor, Pemba
FAMILIA maskini kisiwani Pemba, ambazo zinawezeshwa kifedha na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu, zimekumbushwa kuwa fedha wanazopatiwa sio kwa ajili ya kununulia madira na sare za harusini na badala yake wazitumie kwa kujikwamua na umaskini.

Kauli hiyo imetolewa na Muwezeshaji wakati wa ugawaji wa fedha hizo, shehia ya Ndagoni wila
ya ya Chake Chake, Salma Haji Khamis, kabla ya ugawaji wa fedha hizo kwa kaya maskini 351.

Alisema ni vyema wakajipanga ili kuhakikisha fedha hizo zinawaendeleza na kuwakomboa kutoka kwenye hali ngumu ya umaskini.

“Jamani fedha tunazaowapa nyinyi kutoka TASAF, mzitumie vyema ikiwa ni pamoja na kujikusanya pamoja kuanzisha miradi midogo midogo, ambayo inaweza kuwaendeleza hata baada ya TASAF kumaliza,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuachana na tabia iliozuka kwa baadhi ya shehia, kuzihonga kamati zenye kazi ya kuibua kaya maskini kwani kuafnya hivyo sio sahihi.

Nae Mratibu wa TASAF Pemba, Mussa Said Kisenge, alisema mfuko huo una lengo la kuwakomboa wananchi maskini, hivyo ni vyema wanapokabidhiwa fedha wazitumie kwa malengo yaliokusudiwa.

Alisema zoezi la kutoa fedha hizo kwa awamu hii, lilianza kwa shehia tano za wilaya ya Mkoani ikiwa ni pamoja na shehia ya Makoongwe, Jombwe, Shamiani, Shidi na Mtangani.

Kwa wilaya ya Chake Chake shehia ambazo zilikabidhiwa fedha hizo ni Ndagoni kaya 351,  ambazo zilikabidhiwa shilingi 9,405,563, Kiboni kaya 236 ilikabidhiwa shilingi 5,999,311, Mvumoni kaya 212, shilingi 6,511,769 na Wawi ambapo kuna kaya 251, ambapo zilikabidhiwa shilingi 7,431,060 milioni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.