Habari za Punde

Dk. Shein akaribisha wawekezaji wa Israeli



Na Said Ameir

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Zanzibar na Israeli zina kila sababu za kuimarisha ushirikiano wao ambao wakati wote umeonesha mafanikio kwa kila upande.

Akizungumza na Balozi wa Israeli nchini Tanzania anayemaliza muda wake,Gill Haskel, Dk. Shein alisema ushirikiano kati ya Zanzibar na Israeli umeshuhudia matokeo mazuri hususan katika sekta za afya na kilimo.

Alisema chini ya ushirikiano huo Israeli imekuwa ikisaidia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya afya kupitia Mpango wa Huduma ya Afya kwa Watoto ambapo hadi sasa watoto zaidi 200 hasa wenye matatizo ya moyo wamefaidika na mpango huo. 

Alisema  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ingependa kuona ushiriki zaidi wa Israeli katika kuunga mkono mpango wa serikali kuimarisha kilimo hasa katika kuwajengea uwezo watafiti wa Zanzibar na kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo.

Alisema chini ya mpango huo wa serikali, moja ya lengo ni kujitosheleza kwa chakula kwa kuongeza uzalishaji kupitia uimarishaji wa kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo.

Aliongeza tangu kuanza kwa mpango huo uzalishaji katika kilimo cha mpunga umeongezeka mara tano hivyo lengo la kufikia angalau asilimia 50 ya mahitaji ya chakula ifikapo mwaka 2015/2016 linaelekea kufikiwa.

Sambamba na kilimo cha mpunga alisema  fursa pia zimeelekezwa katika kuwasiaidia wakulima katika mazao mengine ikiwemo kilimo cha mbogamboga zikiwemo tungule asili ambazo zinalimwa maeneo kame.

Alitumia fursa hiyo pia kuiomba serikali ya Israel kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maafa yakiwemo katika usafiri wa majini.

Alibanisha kuwa Zanzibar inahitaji kuwa na vifaa na utalaamu kujiandaa na kukabiliana na maafa ili kupunguza vifo na upotevu wa mali maafa yanapotokea.

Kwa upande mwingine Dk. Shein alimueleza Balozi huyo fursa zilizopo katika sekta ya utalii na kueleza matumaini yake kuwaBalozi huyo atatumia fursa ya kuwepo wake Tanzania kuzitangaza fursa hizo kwa wananchi wa Israeli kuwekeza na kuja Zanzibar wakiwa watalii.

Alisema serikali inafanya jitihada kuitangaza Zanzibar katika masoko ya utalii ya China na Bara Asia ambapo kwa sasa ni watalii wachache kutoka sehemu hizo za dunia hufika Zanzibar.

Alimueleza Balozi huyo kuwa mbali ya vivutio vilivyoko,sifa nyingine kubwa ya  Zanzibar ni ukarimu wa watu wake na wakati wote ni salama na tulivu.    

Kwa upande wake, Balozi Gill Haskel ambaye alikuwa amefuatana na mkewe, alimhakikishia  Dk. Shein  juu ya azma ya serikali ya nchi yake ya kuendeleza ushirikiano na misaada yake kwa Zanzibar.

Alisema anaondoka huku akiwa anaamini kuwa katika kipindi chote alipokuwa akiitumikia nchi yake ameweza kuimarisha uhusiano kati ya Israel na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliongeza kuwa anahakika kuwa Balozi ajaye sio tu ataendeleza na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya ushirikiano yaliyopo sasa bali pia ataangalia uwezekano wa kupanua maeneo mapya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.