Habari za Punde

Wajawazito walala ‘mzungu wanne’ Shinyanga


Na Kadama Malunde,Shinyanga

UKOSEFU wa wodi za kutosha katika kituo cha afya cha Kambarage manispaa ya Shinyanga, umesababisha wanawake wajawazito na waliojifungua kulala wawili katika kitanda kimoja.

Aidha wengine wanalazimika kuweka magodoro sakafuni hali ambayo inahatarisha afya zao na watoto wachanga.

Hayo yalielezwa jana na daktari anayesimamia kituo hicho, Costantine Hubby, wakati akisoma risala kwa Katibu Mkuu  wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT),  Amina  Nassoro Makilagi,baada ya kutembelea kituo hicho na kujionea jinsi wanawake wanavyoteseka kutokana na ufinyu wa wodi.

Alisema kituo hicho hakina chumba cha upasuaji wa dharura kwa wajawazito wanaoshindwa kuzaa kwa njia ya kawaida pamoja na kutokuwa na gari la wagonjwa.

 “Kwa sasa tunawachanganya sehemu moja wagonjwa kwani tuna upungufu wa wodi ya wajawazito na ambao wamejifungua, inabidi walale chumba kimoja na watoto wao wachanga,”alisema.

Aliiomba serikali kuboresha mazingira ya vituo vya kutolea huduma kwa kuongeza majengo na vifaa tiba kwenye zahanati  na vituo vya afya ili kufikia malengo ya millenia.

Akizungumza na wafanyakazi wa kituo hicho, Katibu Mkuu wa UWT,Amina Makilagi,aliwataka kuendelea kuwa na moyo wa upendo na uvumilivu wakati wakuhudumia wagonjwa licha ya kuwepo kwa changamoto  nyingi.

Hata hivyo, aliahidi kufikisha suala hilo kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii ili kuona namna ya kuziondoa changamoto hizo.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Taifa, Zainab Shomari, aliwataka wanaCCM kuvunja makundi baada ya uchaguzi kwani ndiyo yanayochangia  wananchi wachague viongozi wa upinzani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.