Habari za Punde

Imani za kishirikina zakamwisha miradi ya maji Chemba



Na Fatina Mathias,Chemba

KATIKA hali isiyo ya kawaida, imani za kishirikiana katika baadhi ya maeneo ya halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, zimetajwa kuwa ni chanzo cha kukwamisha utekelezaji miradi ya maji na umeme kufuatia wakandarasi kukumbana na vioja mbali mbali ikiwemo nyoka kila wanapochimba.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, katika zoezi la kutia saini mikataba ya ujenzi wa mifumo ya usambazaji maji katika vijiji vitano vya wilaya hiyo.

Alisema wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wanakumbana na hali hiyo kila wanapofukua  mashimo ya kuweka nguzo za umeme kutoa nyoka badala ya mchanga na kwa upande wa maji  maji mabomba yanapasuka muda mfupi baada ya kufukiwa ardhini kwa madai kuwa wakandarasi hao hawajawashirikisha wazee wa kimila kabla ya miradi kuanza.

Aliwataka wakandarasi  kuhakikisha wanawaona wazee wa vijiji hivyo ili kuepuka matukio kama hayo kuendelea kujitokeza na hivyo kuchelewesha maendeleo kwa wananachi.

“Mambo ya kimila jamani ni muhimu naomba tuyafuate ili tuondokane na hali hii, wewe mkandarasi ukawakusanye wazee wa eneo husika unawanunulia mbuzi na pombe ili wafanye tambiko uweze kufanikiwa
katika utekelezaji wako,”alisema.


Aidha aliishukuru serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.187 ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) katika  vijiji vitano.
“Wakazi hawa wenye shida ya maji watawapa ushirikiano ili kuondokana na vikwazo vya aina yoyoe na miradi izingatie thamani ya fedha,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu mhandisi wa maji wa wilaya hiyo, Robert Mganga,alikiri kuwepo kwa matukio ya aina hiyo na kudai yamekuwa yakikwamisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Naye Mhandisi wa wakala wa umeme vijijini (REA) Onesmo Kilamuhama, alisema wamekuwa wakilazimika kufanya matambiko mara kwa mara na wazee wa kimila ili kupata ridhaa ya kutekeleza mradi huo.
Akizungumza katika zoezi hilo,Mkuu wa wilaya hiyo, Francis Isaac,alisema wilaya hiyo inakabiliwa na uhaba wa maji ambapo asilimia 66 ya wananchi hawapati maji kabisa  hali inayochangia kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,William Mafwere, alisema vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni  pamoja na Waida,Chase,Lihonde na Kisande.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.