Habari za Punde

Mkuya:Afrika inashikilia hatma ya dunia



Na Mahmoud Ahmad, Arusha
WAZIRI wa Fedha, Sada Mkuya,amezitaka nchi za Afrika kutambua kwamba bara lao ndilo linalotupiwa macho na dunia kuwa sehemu yenye uhakika wa maisha  yao ya siku za usoni.

Aidha alisema  Afrika ni kituo kikubwa cha shughuli zote za uchumi wa dunia kutokana na kuwepo kwa rasilimali ambazo bado hazijatumika.

Alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa kodi za ndani kwa nchi za Afrika, unaoendelea  jijini Arusha  lengo likiwa ni kubadilishana mawazo, uzoefu na namna ya ukusanyaji wa kodi kwa maendeleo ya nchi washirika.

Alitaja baadhi ya rasilimali zilizogundulika kuwa ni pamoja na gesi asilia na mafuta yanayotarajiwa kuanza kupatikana miaka michache ijayo.

Alisema kutokana na hali hiyo nchi za bara hilo zinapaswa kujitambua na kuweka miundombinu mizuri itakayowezesha kuvunwa rasilimali hizo kwa faida ili ziwanufaishe na kinua uchumi wa nchi zao.


Alitaja miundombinu hiyo kuwa  ni pamoja na usafiri wa aina zote na  elimu ya uvunaji wa rasilimali hizo ili kuepuka kutafuta wataalamu kutoka nje.

Alisema baada ya upande huo kuimarika,mikakati mizuri inapaswa kuandaliwa kudhibiti kodi za ndani ikiwa ni pamoja na kuzuia misamaha ya kodi ambayo imeonekana kuwa kikwazo katika ukuaji wa pato la nchi.

Alisema katika kuondoa misamaha ya kodi, nchi hizo zinapaswa kuweka kiwango maalumu cha misamaha ya kodi badala ya ilivyo sasa ambapo kila nchi inafanya itakavyo.

Aliagiza wanasiasa kushirikishwa zaidi katika mikutano kama hiyo kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya kodi pamoja na kuwasilisha maoni ya wananchi wao kwa kuwa yapo mambo yanayoigusa jamii.

Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Rished Bade, alisema nchi nyingi za Afrika zinakwama katika ukusanyaji wa kodi kutokana na kuwa na sera mbovu.

Alionya dhana ya misamaha ya kodi kama njia ya kuwavutia wawekezaji na kuzitaka nchi hizo kuwa makini akisema  misamaha hiyo ikizidi inaweza kuwa kikwazo na kusababisha nchi hizo kukusanya kodi zake chini ya viwango.

Hata hivyo, alisema Tanzania imefanya vizuri katika ukusanyaji wa kodi za ndani kutokana na mifumo mbalimbali inayotumika hali iliyosababisha kuwa kinara kwa nchi hizo hadi nchi zingine kuja kujifunza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.