Habari za Punde

Dadi akerwa na uchafu Mtemani



Na Masanja Mabula,Pemba
SERIKALI ya mkoa wa kaskazini Pemba, imeelezea kusikitishwa na uchakavu wa makaro katika nyumba za maendeleo Mtemani wilaya ya Wete na kuagiza taasisi husika kuyafukia ili kuepusha uwezekano wa kutokea maradhi ya mripuko.

Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi, alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Majenzi, Baraza la mji Wete,Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Shirika la Umeme Pemba.

Alisema ni vyema taasisi hizo kushirikiana pamoja na kuyafukia makaro hayo ambayo yamekuwa yakitiririsha maji machafu yenye vinyesi vya binadamu.

"Hili ni tatizo na linatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka ili kunusuru afya za  wakaazi wa nyumba hizi kupata maradhi ya mripuko,”alisema.


Katika hatua nyingine Dadi aliagiza migomba iliyopo bloke namba nne na tano yang’olewe ili kudumisha hali ya usafi.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Ofisa Mdhamini  Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati  Pemba, Hemed Salim, alisema tatizo la nyumba hizo linakwamishwa na ufinyu wa bajeti.

Alisema tayari wizara imeomba fedha kwa ajili ya matengenezo ya nyumba hizo na kwamba wanatarajia kupatiwa fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

"Tatizo lipo na linasababishwa na ufinyu wa bajeti, lakini tunatarajia kwamba hali hiyo itaondoka katika kipindi hichi cha fedha kwani tumeomba fedha kwa ajili ya matengenezo ya nyumba hizi,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba, Fatma  Mohammed   Omar, alisema ofisi hiyo kupitia Idara ya Mazingira itahakikisha usafi katika nyumba hizo unadumishwa

1 comment:

  1. Serikali jengeni mji mwengine wa kisasa. Musikae hapo mpaka Leo kubwabwaja maendeleo ya mzew Karume. Nyie mumefanya lipi kubwa. Jengeni new town unguja na pemba.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.