Habari za Punde

Tanzania mwenyeji mkutano mabunge Madola



Na Joseph Ngilisho,Arusha

TANZANIA itakuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa 45 wa Umoja wa Wabunge wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola,kanda ya Afrika (CPA), utakaofanyika Julai 24 hadi 26 mwaka huu,jiji Arusha.

Aidha mkutano huo utatanguliwa na vikao mbali mbali kikiwemo cha kamati tendaji,mkutano wa umoja wa wanawake wa jumuia hiyo,mkutano wa Makatibu wa Mabunge na vikao vya kanda za mashariki,magharibi,kusini na Afrika ya kati,vitakavyoanza leo.

 

Akizungumza na vyombo vya habari Rais wa CPA ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anne Makinda,alisema bunge la Tanzania limepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaofunguliwa na Rais Jakaya Kikwete na kwamba nchi 18 wanachana zinatarajia kuhudhuriwa,huku washiriki wapatao 500 wakitarajiwa kushiriki.

Alisema washiriki wa mkutano huo watatoka katika nchi za Botswana, Cameroon, Ghana, Kenya, Mauritius, Msumbiji, Lesotho, Nigeria, Shelisheli, Namibia, Rwanda, Uganda, Sierra Leone, Afrika Kusini,Swaziland,Zambia na wenyeji Tanzania.

Alisema kwamba lengo la mkutano huo ni kupitisha mpango mkakati wa umoja huo kwa kanda ya Afrika, ambapo moja ya vipengele vyake muhimu ni kubariki ujenzi wa jengo la kisasa la ofisi

za kitega uchumi cha umoja huo,kinachotarajiwa kujengwa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa wabunge hao watakuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu,kujadili changamoto na mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao ya kikatiba ya kutunga sheria,uwakilishi na usimamizi wa shughuli za serikali pamoja na kutazama masuala ya uchaguzi katika nchi hizo.

Alisema mkutano huo utaangazia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia, jinsia katika nyanja za uchaguzi na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazozikabili nchini wanachama.

Katika mkutano huo rais wa sasa wa umoja huo,Anne Makinda, atakabidhi rasmi wadhifa huo kwa Spika wa Lesotho,Sephiri Motanyane.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.