Mwanrafia
Kombo,MCC na Zuleikha Abdalla
MAMLAKA ya
Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar, imesikitishwa na hujuma
zinazofanywa na baadhi ya taasisi na watu binafsi ndani ya mji huo.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya ghafla katika maeneo katika
maeneo yaliyohujumiwa,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Issa Sariboko Makarani,
alisema mamlaka yake imesikitishwa na hujuma hizo zilizofanywa na taasisi
binafsi kwa kushirikiana na taasisi za serikali.
Alisema
katika kipindi hiki cha karibuni kumekua na matukio ya uharibifu wa viguzo
vilivyowekwa maalum kwa ajili ya kuzuia gari zisifike maeneo ya ndani kwa lengo
la kuzuia uharibifu wa nyumba katika eneo la mji huo.
“Tumekua tukiona uharibifu ukifanywa katika maeneo
mbali mbali ya mji wetu ambapo sehemu nyengine hufanywa na watu binafsi na
nyengine hufanywa na taasisi za serikali ambazo hufanya hivyo kwa lengo la
kupata pesa bila ya kujali kuwa wanaweza kuhatarisha mji wetu kutolewa katika
urithi wa kimataifa,” alisema.
Alisema
uharibifu huo ni pamoja na ukataji wa miti ndani ya mji huo,kuharibu taa na
viguzo vya vizuizi ambao umefanyika katika eneo la Shangani mbele ya hoteli ya
Africa House, uharibifu wa taa katika eneo la Forodhani na ukataji wa miti
uliofanywa eneo la Darajani.
Alisema
walioharibu viguzo mbele ya hoteli ya Africa House ni dhahiri wameshirikiana na
taasisi za serikali kwa vile walikwenda Mamlaka kutaka kibali cha kuviondoa na
wakakataliwa.
Alisema
baada ya mamlaka kukataa kutoa kibali ndipo wamiliki wa hoteli hiyo
walipokwenda katika taasisi nyengine ya serikali kuchukua kibali vya kuviondoa
viguzo hivyo, na bila kujali taasisi hiyo ilikubali kwa sababu tu itapata
mapato.
Alishauri wafanyabiashara
kuweka utaratibu wa kutumia maeneo mengine yalio nje ya mji huo kwa lengo la
kuhakikisha msongamano unapungua.
No comments:
Post a Comment