Na Salim Said Salim
UTAWALA wa kifashisti na udikteta huwa na sura nyingi na nyingine huwa za kuvutia ili kuuhadaa umma (watawala huuona umma kama kundi la mabwege).
Madikteta huwa hawajali wala hawaheshimu haki za binadamu, sheria za kimataifa za utawala bora au utu wa mtu ,haki za mke au mume wala watoto, watu wenye ulemavu, vizuka au mayatima.
Kwao kusema uwongo, kutesa, kujeruhi au hata kuuwa ili kubaki madarakani ili wafurahi na waimbe “ Tunawatesa” ni mambo ya kawaida.
Hawa madikteka wanapozungumzia amani na utulivu basi ogopa kwani huwa ndio wapo jikoni wanalipika jungu la kukamata watu na kuwafungulia mashitaka bandia.
Wanapoamua kusisitiza umoja na mshikamano ndio huzusha kauli za kibaguzi kama za “Wapemba waende kwao” na kunyanyasa watu na kuwatangaza wale wanaowakosoa kuwa si raia wa nchi hii kama Tanzania ni mali yao wao peke yao kwa vile chama chao kipo madarakani iwe kwa kwa kura au kwa mbinde.
Ukweli ni kwamba utawala wa kiditeta ni wa kinyama zaidi kuliko wa wanyama wanaofugwa au waliopo kwenye mbuga za Jozani (Unguja), Manyarana na Serengeti (Bara).
Madikteta hutoa kauli za kutisha watu. Kwa mfano, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, aliwahi kusema katika mkutano wa hadhara mjini Unguja kwamba kuuwa hata watu 10 ili ubaki madarakani sio vibaya kwa sababu kiti cha Ikulu ni kitamu.
Ili kuonyesha yeye ni mwenye nguvu alikuwa akiuliza :” Mnaniona komandoo…?” waliokuwa wakimshabikia kwa kuvunja haki za binadamu hawakuacha kumshangilia komandoo..komandooo.
Masikini Salmin, alijisahau na hii leo watu wanajifanya hawamuoni na kujidai wamesahau kwamba alikuwepo Fulani aliyeitwa komandoo.
Katika nchi yenye utawala wa kidikteta watu husombwa na kupigwa na askari hata majumbani mwao na usiku na hupelekwa sehemu zisizojulikana kwa familia zao.
Hali kama hii ya kinyama nilielezea mara nyingi kuwa ilikuwa ya kawaida Zanzibar kwa zaidi ya miongo miwili baada ya Mapinduzi ya 1964 na kusababisha watu wengi kupotea na mpaka leo hapajaelezwa kilichowakuta.
Waliobahatika kuachiwa waliathirika kiafya kwa mateso waliyoyapata mafichoni kulikojulikana kwa kwa jina la “ Ba Mkwe” na hadithi zake mpaka leo zikisimuliwa husikitisha na kutisha.
Hapajatolewa taarifa mpaka leo ya kilichowakuta watu waliopelekwa kwa “ Ba-mkwe” na kupotea, lakini upo uthibitisho kuwa wameshaiaga dunia, lakini vipi walikufa (inaaminika waliuliwa) haijaelezwa.
Hata makaburi yao hayajulikani yalipo. Hii ni dhulma ambayo haitasahaulika na itabakia kuwa sehemu chafu ya historia ya Zanzibar.
Hofu ya watu kukamatwa ovyo ndio iliopelekea maelfu ya Wazanzibari kukimbilia Bara, nchi za jirani, Arabuni, Aisa, Ulaya, Asia, Marekani, Canada na hata Australia kutafuta maisha ya salama.
Kinachosikitisha ni kuona dalili za hali hii kujirudia Visiwani na kutanda wingu la hofu juu ya wa watu kukamatwa majumbani na kupotea. Watu wameanza kuulizana kama kinachoendelea Visiwani ni historia kujirudia?
Matokeo ya karibuni ya watu kukamatwa na kupelekwa mafichoni yanashuhudiwa wakati Zanzibar ikijanasibu kuwa na utawala bota, lakini kinachoonekana ni udikteta na ujahili.
Kama Serikali imeamua kuirejesha sheria ya kidikteta ya kuweka watu kizuizini ieleleze ili umma ujue kuwa udikteta umerejea rasmi Visiwani.
Sio vibaya pia yakaandaliwa maandamano kuunga mkono uamuzi huu wa “ busara” wa serikali wa kurudia siasa za vitisho zinazosababisha watu kupotea.
Vinginevyo wanaohusika na kuweka watu kizuizini wawajibishwe kwani wanapandikiza mbegu za utawala wa kifashisti.
Katika baadhi ya nchi siku hizi, viongozi wa polisi na usalama wa taifa huwekwa gerezani na kuteswa kwa wiki mbili au tatu ili waone machungu ya mtu kuwekwa mafichoni na kuteswa.
Mfumo huu pia huwasaidia kuelewa namna familia zao zilivyopata tabu wakati walipokuwa hawajulikani walipo. Ni vizuri Zanzibar ikawa na mtindo huu ili kuwapa mafunzo ya vitendo wakuu wa vikosi vya ulinzi wanaopenda kuweka watu mafichoni.
Kuwanyamazia wanaoweka watu kizuizini na kutesa familia zao hakutoi tafsiri yoyote ile isipokuwa ya kwamba viongozi wa serikali wanaruhusu vitendo hivi.
Sheria zinataka mtu anayeshutumiwa na kosa la jinai akishakamatwa afikishwe mahakamani haraka na sio kuvumbikwa mafichoni kama embe mbichi inayongojea kuwiva ndio ipelekwe sokoni.
Ni muhimu umma kuelezwa watu waliokamatwa walipelekwa wapi na kosa lao ni lipi. Hili halifanyiki na wakubwa wa nchi wanajigamba ati wanaongoza kwa misingi ya uwazi. Hapana uwazi bali ni ujambazi.
Watu wanapokamatwa ovyo na kuwekwa kizuizini huzuka hofu na hili likifumbiwa macho litawafanya wanaotafuta mwanya wa kurejesha maovu Visiwani kuendelea na udhalimu wao.
Kama tahadhari isipochukuliwa mapema Zanzibar inaweza kujikuta na wimbi jingine la watu kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola .
Hapo tena panaweza kuzuka uvumi wa kila aina na watu kuishi kwa hofu na wengine kukimbia Zanzibar kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Wale wasioitakia mema Zanzibar nao hawatokuwa nyuma kuimba nyimbo za visiwa hivi havikaliki hivyo kukimbiza watalii wanaotegemewa kuingia fedha za kigeni.
Kulea uovu wa ina hii kutasababisha athari za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwani usalama wa watu unapokuwa shakani maendeleo nayo husuasua.
Ni vizuri viongozi wa nchi wakawa makini kupima hatari na athari za kuweka watu kizuizini zilizoanza kuiharibia sifa Zanzibar iliyonza kuonekana tena kuwa nchi inayojali haki za binadamu.
Siku hizi usalama wa nchi ni miongoni mwa vigezo vya uhusiano wa kimataifa. Nchi zinazoelezwa kuwa haziheshimu haki za binadamu hutengwa na kunyimwa misaada na hili lilifanyika kwa Zanzibar miaka ya nyuma.
Ni vizuri tukazuia mazingira yanayotoa taswira mbaya kwani nchi inayotengwa na Jumuiya ya kimatifa huathirika katika maendeleo.
Zanzibar lazima ijifunze kutokana na makosa iliyofanya miaka ya nyuma, kama ikirejea itapswa ijilaumu yenyewe badala ya kuelekeza lawama zake kwa washirika wa maendeleo wameiwekea ngumu wakati ni yenyewe ndio iliyoosabaisha kususwa.
Hapo tena kunung’unika na kutafuta mchawi hakutasaidia kwani wenyewe ndio wachawi.
Njia pekee ya salama kwa Zanzibar ni kuheshimu katiba na haki binaadamu na wanaoivunja katiba au kudhalilisha watu, wawe watoto wa Ba mkwe au wa Ba- Mjomba wasipewe nafasi ya kutamba.
Viongozi wa Zanzibar wakiruhusu watu wachache kutumia vibaya madaraka yao wataujuta kwa namna historia itavowazungumza baya kama inavyofanya kwa komandoo Salmin hivi sasa.
Udikteta na ufashisti, hata ukipewa visingizio gani vya kuuhalalisha, hauisaidii nchi yoyote ile kujenga demokrasia.
Nchi haiongozwi kwa mabavu na ukomandoo, bali kwa katiba na sheria. Mungu inusuru Zanzibar na wanaotaka kuvirejesha visiwa hivi katika utawala wa kinyama kama ulioshuhudiwa miaka ya nyuma.
Chanzo : Tanzania Daima
Article ya fitna kinafiki na uzushi. Hakika wamefilisika siku ya hukumu wale wanaotumia ndimi zao kufarakanisha wenzao. Ukiangalia kwa undani mwandishi wa makala haya ni dikteta zaidi ya hao anaowahukumu kuwa madikteta. Mola akuzindue Inshaa Allah na uepekane na mawazo ya kurudisha nyuma jamii. Jitahidi kuangalia na kuzungumzia mambo ambayo yatajenga na kuinganisha jamii kwa maslahi yao na vizazi vyao.Hapa hujengi isipokuwa unabomoa.
ReplyDeletealiyeshiba hamjui mwenye njaa , subiri ndugu mchangiaji hapo juu siku watu wako wakikumbwa na mkasa huu ndipo utajua ukwelli wa SMZ
ReplyDeleteKinaya ni shibe tosha. Hata ushibe vp Kama hujakinai hutoona tafauti ya shibe na njaa. Hakuna nchi yoyote duniani ambapo hakuna Mamlaka na inayowataka RAIA zake watii Sheria na taratibu. Inaonekana ww hujafanya uchunguzi wa kutosha ukaona jinsi ambavyo nchi mbali mbali duniani zinavyoendeshwa. Mimi pahala popote pale duniani ninapoishi hufuata Sheria na taratibu zilizowekwa hata Kama sizipendi. Kwa hiyo hayo unayosema Mimi hayatonifika.Yatawafika wasiofuata sheria. Watakaondeleza ubabe na fitna. Mimi hayanikuti hayo kwa sababu dini yangu inanifunza utii na unyenyekevu ili kulinda na kudumisha amani utulivu na Upendo. Na Kama pamekushinda Zanzibar basi itakuwa vigumu kwako kuishi kwa amani kokote uwendako. Waswahili wanasema ukitaka kumtupa paka mpe jina baya kwanza. Lakini dini yetu inatukataza kuhukumiana na kupeana majina mabaya. Hao unawaona ww sio wenzio wanawapenda kupita kiasi. Chunga ndimi yako na itumie kalamu yako vyema kwa ajili ya Mola wako. Usitie watu taharuki kwa mapenzi yako binafsi. Sio kweli hiyo taswira unayoiweka kuhusu Viongozi wa Zanzibar. Kama Una mtazamo wako basi ubakie uwe wako usitake watu wawe na msimamo huo wako. Mkamilifu ni Allah peke yake. Madikteta wanashtakiwa The Hague. Kinachofanyika ni uchonganishi na kuna dhima kwa Mola Mtukufu.
ReplyDeletemchangiaji hapo juu naona una maneno makali na unatumia jina la mungu kuhalalisha dhuluma wanazofanyiwa raia kwa sababu tu mtazamo wao ni tofauti na wa serikali tawala , hio sio demokrasia , naam kama kuna dhima basi hio wataijibu viongozi wetu wenye kudhulumu haki zetu , tusubiri kwani makaburi hayako mbali na sisi , na viongozi wetu wengi kiumri wako karibu kurudi kwa udongo. Ushauri wangu kwako usitumie jina la mungu mtukufu kwa kuhalalisha mambo usiyoyajua
ReplyDeleteNdugu blogger si kila kinachoandikwa ukipost itakushinda hii blog jaribu ku zihariri post kabla kujaweka hapa huo ni ushauri tu
ReplyDeleteKudadadeki
ReplyDeleteManeno makali maana yake ni nini ndugu mchangiaji wa NNE hapo juu. Kama ni kuwa na mawazo tofauti na mtoa mada ndio maneno makali basi naomba radhi kwa hilo. Lakini niseme tu Demokrasia sio maana yake kufanya kile tu mtu anachojisikia. China inaudhibiti Mkubwa kwa watu wanaotaka kuvuruga amani kwa kisingizio cha demokrasia. Ni taifa la utawala wa chama kimoja na inaongoza ulimwengu kwa maendeleo. Kuhusu kumtaja Mungu ni kwa sababu Quran tukufu haijabakisha kitu kukizungumzia. Nenda kwenye YouTube mawaidha ya Kishki uangalie katika anuwani isemayo 'UMUHIMU WA KUDUMISHA AMANI NA UTULIVU'. Wanasiasa na waandishi wa habari Rwanda walifanya makosa haya haya ya kuandika makala za kichochezi na matokeo yake watu millioni moja walifariki. Kama tunataka kubadilishana mawazo na kuelimishana basi haya ndo mawazo yangu ninayochangia. Ila Kama kinachoandikwa tu tukubaliane nacho basi na hii comment isiwe posted Kama ilivyotokea kwa comment ya mwanzo. Nawatakia kila la kheri katika kuelimiaha jamii.
ReplyDeleteNashukuru kuona comment yangu hapo juu. Nitoe rai tu kwa mchangiaji wa NNE. Kama kuna jambo nalisema silijui basi nielimisha kwa faida ya jamii nzima baada ya kudai kwamba nisizungumze mambo nisiyoyajua.
ReplyDeleteLakini tena Nenda YouTube mawaidha ya KISHKI yenye Anwani 'TUSIDHARAULIANE'.Utapata picha ya hili ninalolizungumzia. Allah anakataza kuwahukumu wenzetu na kuwaita majina mabaya. Haya yapo miongoni mwetu mashehe na viongozi wa serikali.
Mfano katika makala hii inatuhumiwa mahakama kutotenda haki. Cha kushangaza anahusishwa kiongozi wa nchi. Kwa mujbu wa KISHKI ni kumdhulumu. Kwanini asiwe Jaji au Hakimu.
Mfano mwengine kwa lipi kubwa alilofanya Salmin mpaka aitwe Dikteta. Si Kiongozi huyo aliyemtoa Makamo wa Rais wetu wa sasa Jela. Kama kuna kosa alilofanya Kama mwanadamu kwanini asisamehewe kama alivyosamehewa Makamo wa Rais ambaye alizunguka ulimwengu nzima kuisaliti nchi yake mwenyewe mbele ya jumuiya ya kimataifa hatimaye ikatengwa kwa kukoseshwa misaada.
Makala inazungumzia maauaji yaliyotokea Zanzibar. Ni kwa manufaa ya nani na kwa misingi IPI? Kwanini Wahindi Wekundu ( Red Indians) wenyeji wanaopatikana nchini Canada Brazil na Austrilia waliuwawa takribin million 40 wasilipize kisasi na kuendeleza uhasama katika nchi zao. Tuwasuse Western basi walotudhalilisha Waafrika kwa utumwa na zaidi ya watu million 800 walitoswa baharini katika zoezi hilo.
Watusi na Wahutu wanaishi pamoja. Huu uchungu upo Zanzibar tu.
Naomba hii comment iwe posted ili tuendelee kubadilishana mawazo kwa ustaraabu kwa nia ya kuelimishana.
Nashukuru.