Habari za Punde

Dk Shein awataka waganga wa tiba Asili kuzingatia maadili

Na Khamis Haji, OMKR
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein ametoa wito kwa Waganga wa Tiba Asili nchini kuzingatia maadili na taratibu za kazi zao na kuepusha madhara yanayoweza kuwakumba wananchi wanaowapa huduma.

 Rais Shein ameyasema hayo leo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Waganga wa Asili Barani Afrika, yaliyofanyika katika bustani ya Victoria, Mnazi mmoja mjini Zanzibar.

 Amesema Tiba Asili na Tiba Mbadala inategemewa na wananchi wengi  Barani Afrika na Duniani kote, ambapo kwa Tanzania asilimia 60 ya wananchi wake imethibitishwa kuwa hupata tiba hiyo.

 Mhe. Rais amesema kutokana na haja iliyopo, Waganga wa Tiba Asili hawana budi kufuata taratibu zilizowekwa na Baraza la Tiba Asilia katika kuhakikisha hawasababishi athari kwa wateja wanaofika kupata huduma wanazozitoa.

 Dk. Shein ameeleza kuwa fani ya Tiba Asili itaweza kupata mafanikio na kunufaisha wananchi ipasavyo, iwapo waganga hao watashirikiana na Waganga wa Kisasa katika kuhakikisha matibabu yao yanathibitishwa kitaalamu na yana ubora unaohitajika.


 Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inathamini mchango unaotolewa na Waganga hao na itahakikisha Mamlaka zinazohusika na matibabu wanayoyatoa zinapewa msukumo na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

 Katika hafla hiyo, Rais wa Taasisi ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya Afrika Mashariki, Kamuntu Matoke ameahidi kuwa wataendelea kusimamia maadili na kuhimiza utunzaji wa miti asili ambayo imekuwa ikitegemewa na wananchi wengi kwa matibabu.

 Hata hivyo amesema ili waweze kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi na kufikia matarajio ya wateja wao, nchi za Afrika Mshariki zikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda zinazounda umoja huo hazina budi kuwa na Sera na Sheria za tiba asili zenye lengo moja.

 Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili Zanzibar, Dk. Mayasa Salum amesema wanachukua juhudi kubwa kuhakikisha watu wote wanaofanya kazi za Tiba Asili na Mbadala wanasajiliwa na kupewa mafunzo ya kazi hizo.

 Amesema hadi sasa Zanzibar kuna Waganga Asili 193 waliosajiliwa rasmi na wamekuwa wakinufaika na mafunzo mbali mbali yanayohusu utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.