Habari za Punde

Ombi la dhamana ya Mansoor Agosti 11

Na Khamis Amani
 
MAHAKAMA Kuu Zanzibar itasikilisha ombi la dhamana lililowasilishwa na mawakili wanaomtetea aliewahi kuwa Waziri katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid, anayekabiliwa na mashitaka ya kupatikana na silaha na risasi 407.

Ombi hilo litasikiliwa na Jaji Abraham Mwampashi  Agositi 11.

Juzi mahakama ya mkoa Vuga chini ya Hakimu Khamis Ramadhan ilimnyima dhamana Mansoor baada ya kufikishwa makamani hapo kujibu mashtaka matatu yanayomkabili.

Sababu zilizotolewa na hakimu huyo ni kwamba  shitaka la kupatikana na silaha ni miongoni mwa mashitaka yasiyokuwa na dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 150 (1) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.


Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kisheria ya kutoa dhamana kwa makosa yote yasiyokuwa na dhamana.

Ombi hilo ameliwasilisha chini ya kifungu cha 150 (4) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.

Mahakama Kuu tayari imeshatoa hati za wito pamoja na hati ya kiapo iliyowasilishwa na mshitakiwa huyo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ambae ndiye mpingaji wa dhamana.

Mansoor ambae aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kufukuzwa,anakabiliwa na mashitaka matatu ya kupatikana na silaha, risasi na marisau kinyume cha sheria.

Silaha anayodaiwa kupatikana ni bastola aina ya Bereta pamoja na mashitaka ya kumiliki risasi za moto 295 za bastola na kumiliki risasi aina ya marisau 112 za bunduki aina ya shortgun, badala ya marisau 50 alizoruhusiwa kisheria mashitaka ambayo yana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kesi dhidi yake inatarajiwa kufikishwa tena mahakama ya mkoa Vuga Agosti 18 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, kutokana na upelelezi wake kutokamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.