Habari za Punde

Polisi mbaroni kwa mauaji

Na Mwanajuma Mmanga
MTU mmoja mkaazi wa Migombani alietambuliwa kwa jina la Said Mohammed Said (45), ameuawa kwa kuchomwa kisu cha ubavu.

Mauaji hayo yametokea mtaa wa Kaburi Kikombe wilaya ya magharibi Unguja Agosti tano mwaka huu.
Mtuhumiwa wa mauaji hayo ametajwa kuwa ni Haji Maliki (40) ambae ni askari polisi anaefanya kazi kituo cha polisi Fuoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema mauaji hayo yalitokea saa 8:00 mchana wakati askari huyo alipofika nyumbani kwao marehemu kwa lengo la kuonana na mpenzi wake.

Alisema baada ya familia ya marehemu kumzuia mtuhumiwa kumuona mpenzi wake na kumtaka asiende nyumbani hapo kutokana na tabia zake mbaya, ndipo alipoamua kufanya mauaji hayo.

Alieuliwa ni shemeji wa mpenzi wa askari huyo ambae alifika nyumbani hapo kwa lengo la kumuona mama mkwe wake.


“Baada ya kuzuiwa mtuhumiwa alitoa kisu kidogo kilichokuwemo mfukoni kwake na kuanza kumchinja marehemu mikononi na baadae kumchoma kisu cha kifua upande wa kushoto na kusababisha kifo chake,” alisema.

Alisema baada ya mauaji hayo mtuhumiwa alikimbilia kituo cha polisi Mwanakwerekwe kwa kujisalimisha.


Alisema mtuhumiwa atafikifishwa mahakamani baada ya ushahidi kukamilika kujibu shitaka la mauaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.