Habari za Punde

Skuli ya Msingi Wingwi Mtemani yapongezwa


Na: Ali Othman Ali
 
Shule ya Msingi ya Wingwi Mtemani , Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, imepongezwa na  kuzawadiwa kwa kuweza kupasisha wanafunzi  8 kati ya 46 waliofanya mtihani katika awamu yao ya kwanza  ya mitihani ya darasa la saba mwaka 2013-2014 .
 
Tukio la kuwazawadia Wazazi, Walimu na Wanafunzi wa shule hiyo limefanyika katika hafla iliyoandaliwa na kudhaminiwa na Mwalimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha London, SOAS na Cambridge Bwana Yussuf Shoka katika viwanja vya shule hiyo siku ya Jumamosi ya tarehe 30 Agosti, 2014.
 
Hafla hiyo iliyosimamiwa na kuwakilishwa na mgeni mualikwa, Afisa wa Elimu Mkoa wa kaskazini Pemba  Bwana Muhammed Nassor  Salim ilihudhuriwa pia na Wazazi, Wanafunzi na Wanakijiji wa Shehia ya Mtemani ambapo Afisa huyo alimpongeza Bwana Yussuf Shoka kwa moyo wake wa kizalendo na wa kujitolea kwa hali na mali hususan katika nyanja ya Elimu hapa nchini.
 
Katika hafla hiyo, Mwalimu Yussuf Shoka aliwashauri walimu kusimamia suala zima la maadili na nidhamu kwa wanafunzi shuleni. Aidha, Bwana Shoka aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii wakiamini kwamba Elimu ndio mkombozi wa maisha yao na kwamba  Elimu ni chachu ya maendeleo ya taifa.
 
Wakati huo huo Bwana Shoka amewazadia wanafunzi nane waliofaulu mchepuo darasa la saba mwaka 2013,  kwa kuwapa vifaa mbali mbali vya kusomea na fedha taslimu za kujikimu.
 
Mwalimu huyo pia ametoa fedha taslimu kwa walimu wote wa shule ya Wingwi Mtemani na kamati nzima ya shule ya Msingi Mtemani  ili kuwapa motisha kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuendeleza maendeleo ya Elimu na ustawi wa shule hiyo na Taifa kwa ujumla.
 
Akizungumza katika hafla hiyo, Bwana Shoka aliahidi kuipatia ofisi ya Mwalimu Mkuu kompyuta moja, printer na mashine ndogo ya fotokopi kama zawadi kwa ajili ya shule hiyo. Pia aliahidi kuanzisha maktaba ya kisasa katika shule hiyo ili kujenga na kuendeleza utamaduni wa kusoma na kaundika ili kunyanyua kiwango cha Elimu na ufaulu shuleni hapo.
 
Akihitimisha hutuba yake kwa walengwa wa hafla hiyo, Bwana Shoka ameahidi kuendeleza utamaduni wa kuwazawadia wanafunzi wote watakaofaulu katika ngazi ya mchepuo kutoka katika shule zote  nne za msingi za Wingwi kuanzia mwaka 2015.
 
Aidha, Bwana Shoka alibainisha sababu zilizompelekea kuandaa hafla hiyo kwa kusema; ‘Mimi si mwanasiasa, nabakia kuwa Mwalimu. Naomba nieleweke kuwa sitoi kwa ajili ya kujijenga kisiasa na wala sitoi kwa sababu nina fedha nyingi. Natoa kwa ajili ya Mungu, na kwa ajili ya ndugu zangu kwa kiasi ya uwezo niliojaaliwa nikiamini kwamba kutoa ni moyo na wala si utajiri’.
 
Wakati huo huo, Mgeni rasmi katika hafla hiyo Bwana Muhammed Nassor aliwaasa wanafunzi kujiepusha na matumizi mabaya ya teknolojia ya kisasa ya internet na Kompyuta  kwa kuwataka wanafunzi wa shule hiyo kuitumia teknolojia hiyo kwa ajili ya kujiendeleza na kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
                   

1 comment:

  1. Ni mfano Mzuri wa Kuigwa ili Kuwatia mortisha watoto na Walimu waweze kufanya kazi kwa pamoja na kudumisha nidhamu. na kukaza kamba yakusoma... Kinachosikitisha nikwamba Wanafunzi wa Kiislamu hasa Wenye Majina ya Kizanzibari huanza vizuri huku Chini hata Wakifika Form 4 na Form 6 Wakafelishwa na kupata FFFFFFFF tupu..

    Kwasababu Wazanzibari bado Tunatawaliwa na Mkoloni Mweusi Tanganyika ambae anamiliki hata Baraza la Mitihani... Na Ikiwa SMZ itaendelea Kushikiliwa na Ngedere Wasiokua na Vission isipokua Kujaza Matumbo yao tu na Fitna.. Basi Juhudi za wanafunzi hawa na walimu wao Zitaishia Ukingoni.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.