Habari za Punde

Z-NCDA Kuzindua Kampeni ya Uchunguzi wa Kansa Zanzibar

Na Faki Mjaka Maelezo.
Jumuiya ya Maradhi yasiyo Ambukiza Zanzibar (Z-NCDA) inatarajia kuzindua Kampeni ya Uchunguzi wa Maradhi ya Kansa ya Shingo ya Kizazi Agosti 30-31 mwaka huu.

Uzinduzi huo utafanyika katika Kituo cha Afya Mpendae mjini Zanzibar ambapo Wanawake wenye dalili za Maradhi hayo watafanyiwa uchunguzi bure kituoni hapo.

Akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwao Mpendae, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Ali Mansour Vuai amesema lengo la uchunguzi huo ni kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya Ugonjwa huo hatari ambao ni vigumu kujua dalili zake.

Amezitaja dalili za Saratani ya Shingo ya Kizazi kuwa ni pamoja na Maumivu makali sehemu ya kiuno hadi mapajani pamoja na kutokuwa na mpangilio maalum wa Hedhi.

Dalili zingine ni kutokwa na Damu wakati wa tendo la ndoa, kutokwa na maji maji Ukeni yanayowasha kwa muda mrefu na kujiskia maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.

Mwenyekiti Ali amewaomba Wanawake ambao watakuwa na moja kati ya dalili hizo waweze kufika Mpendae ili kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Amesema Jumuiya yao itakapogundua Muathirika wa Tatizo la Kansa ya Shingo ya Kizazi watamsaidia kwa kumkutanisha na Madaktari wa Mnazi mmoja au Muhimbili ili kusaidiwa matibabu ya Afya yake.


“Zanzibar kumefanyika uchunguzi wa magonjwa mengi ikiwemo Kansa lakini hakujawahi kufanyika Uchunguzi wa Kansa ya Shingo ya Kizazi kwa Wanawake..hili ni tatizo ambalo linawamaliza wanawake wengi ndio maana Jumuiya ikaamua kufanya kazi hiyo”Alisema Mwenyekiti Ali.

Kwa upande wake Katibu wa Z-NCDA Ali Zubeir amesema ni Vyema watu wakajenga mazingira ya kupima afya zao mara kwa mara hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya Magonjwa ikiwemo Saratani ya Shingo ya Kizazi huchukua muda mrefu kabla ya kumuathiri mgonjwa.

Amesema kwa vile maradhi hayo huathiri sana sehemu za siri wameandaa mazingira mazuri ambayo mgonjwa atafanyiwa uchunguzi wake na Wataalamu Wanawake ili kulifanya zoezi hilo kuwa rahisi kwao.

Katibu huyo amesema malengo yao ni kufanya uchunguzi wa Kansa ya Shingo ya kizazi katika kila Jimbo Zanzibar, lakini kwa sasa hawana pesa za kugharamia Uchunguzi huo na kwamba wanaishukuru Asasi ya Kiraia ya nchini Denmark kwa kuchangia jumla ya Shilingi Milion 7 na nusu kwa ajili ya zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.