Na Mwantanga Ame
SERIKALI imesema hakuna mgogoro
wa kisiasa na kisheria Tanzania na haiko tayari kuruhusu kundi lolote kuvunja
sheria za nchi.
Tamko hilo limetolewa mjini
Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Dk. Asha Rose Migiro, wakati
akiwasilisha tamko hilo kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Tamko hilo inakuja wakati
CHADEMA ikipanga kuitisha maandamano na migomo ya nchi nzima kupinga kuendelea
mchakato wa katiba.
Alisema wito unaotolewa na
baadhi ya viongozi wa kulazimisha kusitisha bunge hilo sio sahihi kwani taifa
halina mgogoro wa kisiasa na serikali itahakikisha hakuna mtu atakaevuruga
amani iliyopo.
“Hakuna sababu ya kuruhusu watu
kujazwa hofu, serikali ipo macho na itasimamia sheria na taratibu zilizowekwa ili
kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kutafuta riziki na mchakato
huu upo kisheria,” alisema.
Aidha alisema mahakama kuu
imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa kutaka bunge hilo lisitishwe.
Alisema uamuzi huo wa mahakama,
unathibitisha bunge hilo lipo kihalali.
Alisema hadi juzi usiku wakati
bunge hilo linafanyiwa uhakiki kulikuwa na wajumbe 500 sawa na asilimia 79 ya wajumbe
wote 630, wakati wabunge waliosusia kuingia ni 130.
Alisema kundi la 201 lina
wajumbe 189 wanaoshiriki bunge hilo jambo ambalo linaonesha wazi kuwa idadi
hiyo haina kikwazo kwa shughuli za bunge.
Alisema wajumbe 348 wanaotoka Tanzania Bara kati yao
125 wanatoka kundi la 201 na kwa wajumbe wanaotoka Zanzibar wapo 152 ambapo kati
yao 64 ni wa kundi la 201.
Alisema bunge hilo, lina wawakilishi
wanaotoka vyama 18 vya siasa wakati vyama vilivyosusia ni Chadema, CUF na NCCR
Mageuzi.
No comments:
Post a Comment