Na Joseph Ngilisho, Arusha
OFISI za Chama Cha Mabadiliko
na Uwazi (ACT) mkoani Arusha,zimevamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana na kuzuvunja, kisha
kuiba fedha taslimu shilingi 280,000 na nyaraka muhimu za chama hicho.
Akizungumza na vyombo vya
habari ofisi kwake, Katibu wa ACT mkoa wa Arusha, Matokeo Simba, alisema tukio
hilo limefanyika majira ya usiku na wanahisi watu hao ni wafuasi wa Chadema.
Alisema katika nyaraka
zilizoibwa ni pamoja na kadi 10 zilizokuwa za wanachama wa chama hicho.
Alisema iwapo isingekuwa watu
hao kuwa ni wafuasi wa Chadema wasingeiba kadi hizo, kwakua zilikua na mzozo
kutoka kwa viongozi wa Chadema baada ya wanachama hao pamoja na Mwenyekiti huyo
kutangaza kukihama Chadema ambapo waliwataka warejeshe kadi hizo.
“Hivi kama sio wao
inawezekanaje watu wavunje ofisi yetu halafu waibe pia kadi hizo zilizokuwa za
wanachama wao, si wangeiba tu nyaraka nyingine,” alihoji.
Alitaja nyaraka nyingine
zilizoibwa kuwa ni hati ya uhakiki wa wanachama kutoka kwa Msajili wa vyama vya
siasa,jambo ambalo linaonesha lina lengo la kupoteza ushahidi wa uhakiki huo.
Alisema mbali na hati hiyo pia
watu hao waliiba kadi tupu za uanachama pamoja na bendera jambo ambalo pia
alilielezea kuwa lina lengo la kufanya hujuma katika mikutano ya hadhara, kwa
kuwapandikiza watu ili waoneshe wanarejesha kadi na kujiunga na vyama vingine.
Alisema fedha hizo shilingi
280,000 zilizoibwa zilikua ni za michango kutoka kwa wanachama, ada za
uanachama na mauzo ya kadi za chama
ambazo zilikua ofisini hapo kwa ajili ya shughuli za chama.
Alisema waligundua tukio hilo
saa 2:00 asubuhi wakati walipokua wakifungua ofisi ambapo walikuta mlango wa
mbao na wa chuma uko wazi na ndipo walipotoa taarifa polisi ambapo walipatiwa
namba AR/RB/12473/2014 na kuahidiwa kufanyika upelelezi.
Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti
wa Chadema mkoa wa Arusha, Aman Golugwa, alisema kamwe viongozi na wafuasi wa
chama chake hawawezi kufanya kitendo hicho kwa kuwa viongozi waliokihama chama
chao hawana shida nao.
Alisema chama chake kwa sasa
hakina muda wa kuhangaika kutafuta wanachama bali kinachofanya ni kutafuta
wapiga kura kwa ajili ya chaguzi zijazo.
No comments:
Post a Comment