Na Said Ameir, Comoro
TANZANIA imempongeza Rais wa
Muungano wa Comoro, Mhe. Dk. Ikililou Dhoinine, kwa kuimarisha umoja na
mshikamo miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo ambapo hivi sasa Comoro imekuwa na
utulivu na amani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, alisema ni jambo la kujivunia kuona wananchi wa visiwa
huvyo wako katika utulivu, amani na wamekuwa bega kwa bega na serikali yao
chini ya uongozi wa Rais Dhoinine.
Akizungumza katika hafla ya
chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshma yake na mwenyeji wake, Rais wa
Muungano wa Comoro, Dk. Shein alisema ziara yake nchini humo ina lengo la
kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo baina ya wananchi wa Tanzania na Comoro.
Alimueleza Rais Dhoinine na
wageni waliohudhuria hafla hiyo kuwa amefurahishwa na namna serikali na
wananchi wa Comoro wanavyothamini uhusiano wao na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na ushirikiano na ndugu zao wa Zanzibar.
“Najisikia niko nyumbani kwa
sababu uhusiano wetu umeimarishwa zaidi na mahusiano ya wananchi wake kwa karne
nyingi, mahusiano ambayo yamekuwa katika masuala ya kijamii, utamaduni,
biashara na mambo mengine mengi,” alibainisha Dk. Shein.
Aliongeza kuwa Zanzibar na
Comoro zina mazingira yanayofanana na hata changamoto zinazokabiliana nazo,
hivyo ushirikiano katika kukabiliana nazo ni jambo jema linaloweza kuleta
mafanikio kwa faida ya ustawi wa watu wa Zanzibar na Comoro.
Alimueleza Rais Dhoinine kuwa
Zanzibar na Comoro zina malengo mamoja ya kuleta maendeleo na ustawi kwa
wananchi wao kwa hivyo hiyo ni fursa kwa Zanzibar na Comoro kushirikiana kwa
pamoja kutimiza lengo hilo.
Alimshukuru Rais wa Comoro kwa
kumualika kutembelea nchini mwake ambapo viongozi hao wawili walipata fursa ya
kufanya mazungumzo ambayo yamefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa karibu kati
ya Tanzania na Comoro.
Kwa upande Rais wa Comoro, Mhe.
Dk. Ikililou Dhoinine, alieleza ziara ya Dk. Shein nchini humo kuwa imegusa
hisia za wananchi wa Comoro kwa kuwa wananchi wa Comoro na Zanzibar wana
uhusiano wa damu na kuifananisha hafla hiyo kuwa ni muungano wa kifamilia.
“Tunafahamu fika uhusiano wa
mioyo na damu inayowaunganisha watu wetu, uhusiano unatokana na historia,
lugha, mila na utamaduni, kutembeleana mara kwa mara na wananchi wengi wa
visiwa kubadilishana makazi katika visiwa hivi,”alisema.
Alimshukuru Rais wa Zanzibar
kwa kukubali mwaliko wake wa kutembelea Comoro.
Mapema marais hao walifanya
mazungumzo rasmi ikulu ambayo yalikuwa juu ya namna ya kukuza ushirikiano kati
ya Zanzibar na Comoro ikiwemo kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa
ya pande mbili hizo.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara
hiyo, Dk. Shein anatarajiwa kutembelea kiwanda cha samaki na baadae kwenda mji
wa Mitsamihouli ambako wakaazi wake wengi wana mafungamano na wananchi wa
Zanzibar.
Akiwa huko atashiriki sala ya
adhuhuri na baadae kupata chakula cha mchana kilichoandaliwa na wananchi wa
Mitsamihouli kwa heshma yake na ujumbe wake.
Baadae atatembelea ubalozi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro ambako atapata fursa ya
kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchini humo na pia kuzindua tovuti ya ubalozi.
No comments:
Post a Comment