Na Khamis Haji, Istanbul
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim
Seif Sharif Hamad amesema hali ya amani na utulivu katika eneo la Afrika
Mashariki ni ya kuridhisha na wawekezaji vitegauchumi pamoja na wafanyabiashara
wanaotaka kutumia fursa zilizopo katika eneo hilo waje na waondowe hofu.
Maalim Seif ameyasema hayo katika mkutano wa Uchumi
wa Dunia (WEF) unaoendelea katika jiji la Istanbul nchini Uturuki alipotakiwa
kutoa maoni yake juu ya hali ya usalama katika eneo hilo la Afrika Mashariki.
Amesema iliwahi kujitokeza hali ya kukithiri vitendo
vya kiharamia vilivyo sababishwa na kukosekana utulivu katika nchi ya Somalia,
lakini matukio hayo hivi sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mashirikiano
ya pamoja kati ya nchi zilizopo jirani pamoja na Jumuiya ya Kimataifa.
Amesema nguvu hizo za jumuiya ya kimataifa zinapaswa
kuendelezwa, ikiwemo kuzijengea uwezo nchi za Afrika katika kukuza upatikanaji
wa ajira kwa vijana, ili kuwaepusha na uwezekano wa kushawishiwa na makundi ya
watu waovu ambayo yamekuwa chanzo cha kuongezeka matendo maovu.
“Hali katika eneo la Afrika Mashariki ni salama sana
kuna vivutio vya kila aina, wawekezaji
tumieni fursa hii kuja kufungua miradi yenu”, amesema Maalim Seif.
Amesema ni jukumu la Jumuiya ya Kimataifa kuzipa
msukumo nchi zenye matatizo ya uchumi, likiwemo tatizo kubwa la uhaba wa ajira
miongoni mwa vijana, ambalo litawaepusha vijana na tabia ya kurubuniwa kuingia katika matendo
yasiofaa.
Waziri Mkuu wa Mali, Moussa Mara akizungumza wakati
wa ufunguzi wa mkutano huo, amesema mataifa yakiungana kupiga vita matendo ya
ugaidi yanayojitokeza katika maeneo tafauti Duniani yanaweza kudhibitiwa.
“Mataifa yana wajibu wa kuungana na kukusanya nguvu
kupiga vita matendo ya kigaidi ambayo hayajui mipaka”, amesema.
Amesema mkutano huo wa Dunia wa masuala ya Uchumi uwe
ni hatua ya kufungua ukurasa mpya katika kukabiliana na matendo ya ugaidi
ambayo licha ya kutoa mchango mkubwa katika kurejesha nyuma maendeleo ya
kiuchumi, lakini pia husababisha maafa makubwa kwa jamii zote.
“Ugaidi Duniani hivi sasa ni kama maradhi ya
Saratani, njia pekee ya kuweza kuyatibu ni mataifa kushirikiana katika kuandaa
mikakati ya pamoja kuyakomesha”alishauri.
Baadhi ya wajumbe katika mkutano huo wamesema changamoto
zilizopo katika eneo la Afrika chini ya Jangwa la Sahara zimekuwa zikichangiwa
kwa kiasi kikubwa na hali ya mapigano, kukiukwa kwa haki za bianaadamu na
kukosekana utawala wa kisheria katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, walisema kumekuwa na mafanikio makubwa
katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo kutokana na
juhudi kubwa zinazoendeela kuchukuliwa na mataifa ya eneo hilo.
Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip
Erdogan, ukibeba ajenda kuu ya kuwepo matumizi mazuri ya rasilimali kwa
maendeleo ya mataifa na kuweka hali ya usalama.
Katika hotuba hiyoya Rais Erdogan, ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa
kushirikiana na nchi yake katika kuleta demokrasia, Utawala Bora na amani ya
kudumu katika nchi zilizopo jirani na Uturuki, zikiwemo Irak na Syria.
Amesema migogoro inayojitokeza katika nchi hizo imekuwa
chanzo kikuu cha matendo ya kigaidi, pamoja na kuibua madhara makubwa kwa nchi
yake yanayotokana na wimbi la wakimbizi wanaokimbia machafuko katika nchi
zilizopo jirani na Uturuki.
Amesema hadi sasa kuna wakimbizi wapatao milioni 1.5
wanaohifadhiwa katika nchi yake na kuilazimisha nchi hiyo kuwa na mikakati
mikubwa ya kuweka ulinzi katika mpaka wake na nchi jirani zenye mizozo.
No comments:
Post a Comment