Na Rose Chapewa, Mbeya
WATU watatu wamefariki dunia
mkoani Mbeya katika matukio tofauti akiwemo Mwinjilisti wa Kanisa la Baptist
kufariki baada ya kupigwa mchi wa kutwangia kichwani,wakati akimuombea mgonjwa
wa akili huku mwingine akifariki baada
ya kuchomwa mkuki na mtoto wake wa kambo, na mwingine akiuwawa kwa deni la
shilingi 500.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa huo, Ahmed Msangi, mwinjilisti huyo
alitambuliwa kwa jina la Ambumbulwise Mwasomola (35) mkazi wa kijiji cha
Lukasia tarafa ya Busokelo wilaya ya Rungwe.
Alisema tukio hilo
lilitolea Septemba 27 saa 5:30 usiku
ambapo alipigwa na mtu mmoja aliyefahamika
kwa jina la Swalapo Mwaisanila (56) mkazi wa kijiji cha Lwangwa anayedaiwa
kuwa ni mgonjwa wa akili.
Alisema chanzo cha tukio hilo
kilisababishwa na marehemu kutaka kumuombea mtuhumiwa huyo, baada ya
kusumbuliwa na ugonjwa wa akili muda mrefu na hivyo kuinuka na kumpiga na mchi
kichwani.
Akizungumzia tukio la pili,
alisema mtu mmoja aliyefehamika kwa jina moja na Kabote (41) mkazi wa kijiji
cha Mwanavala wilayani Mbalali, alifariki dunia baada ya kuchomwa mkuki sehemu
mbalimbali za mwili wake na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Nyamaniengo
Kinanga ambaye ni mmiliki wa klabu cha pombe za kienyeji.
Tukio hilo lilitokea Septemba
28 saa 5 usiku Mwanavala tarafa ya Rujewa ambapo inadaiwa mauaji hayo yalitokea
baada ya marehemu huyo kushindwa kulipa deni la shilingi 500 alilokuwa akidaiwa
mara baada ya kunywa pombe kilabuni hapo.
Kutokana na tukio hilo watu 13 waliokuwepo
eneo la tukio wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano.
Na mtu mmoja aliyefahmika kwa
jina la Richard Nelson Fwambo (50) mkazi
wa kijiji cha Utambalila wilaya ya Mbalali alifariki dunia baada ya kukatwa
katwa na kitu chenye ncha kali sehemu za
kikichwani na Khamis Mgala (32) mkazi wa Mlowo Mbozi ambaye ni mtoto wake wa kambo.
Tukio hilo lilitokea Septemba
28 mwaka huu saa 7 usiku katika kitongoji cha Magamba wilayani Mbozi, ambapo
inadaiwa mtuhumiwa kabla ya kutenda kosa hilo alivunja mlango kisha kuingia
ndani na kuanza kumshambulia marehemu.
Ilidaiwa mtuhumiwa alianza
kumshambulia marehemu ndani kwake akiwa amelala na mke wake aliyefahamikwa kwa
jina la Yustina Kashapamba (40) maarufu kwa jina la Nakamanga ambaye ni mama mzazi wa mtuhumiwa.
Alisema chanzo cha tukio hilo,mtuhumiwa
alikuwa hapendi mama yake aishi na marehemu ambaye ni baba yake wa kambo, baada
ya baba yake mzazi kufariki, na kwamba mtuhumiwa baada ya kufanya mauaji hayo
alikimbia na kutokomea kusikojulikana na anatafutwa na jeshi la polisi.
No comments:
Post a Comment