Habari za Punde

JK: Kura ya Maoni Katiba Aprili mwakani



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa endapo mipango yote itakwenda kama inavyoandaliwa, Watanzania watapata nafasi ya kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa, ili kukamilisha mchakato wa Tanzania kusaka Katiba Mpya.
Rais Kikwete amesema hayo asubuhi ya leo, Jumatano, Oktoba 22, 2014, wakati alipokutana na kuzungumza na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China.
Mkutano huo na mabalozi wa Afrika uliofanyika kwenye Nyumba ya Kufika Wageni ya Serikali ya Diaoyutai mjini Beijing ambako Rais amefikia, ilikuwa shughuli ya kwanza ya Rais Kikwete katika ziara yake rasmi ya Kiserikali ya siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping. Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete aliwasili China usiku wa jana, Jumanne, Oktoba 21, 2014.
Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo ya kukutana na mabalozi kuwaelezea hali ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi katika Afrika ikiwamo maendeleo ya mchakato wa Tanzania kusaka Katiba Mpya.
Kuhusu mchakato huo wa Katiba, Rais Kikwete amesema kuwa mchakato huo unakwenda kama ilivyofikiriwa tokea mwanzo kuwa wakati ulikuwa umefika wa Tanzania kuipitia upya Katiba ya sasa kwa nia ya kutunga Katiba Mpya “ambayo itaiongoza nchi yetu kwa miaka mingine 50 kama ilivyofanya Katiba ya sasa.”
Rais Kikwete amesema kuwa mpaka sasa mchakato huo unakwenda vizuri baada ya kupitia hatua zote ikiwamo ile ya Kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kuundwa kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi, Kuundwa na Bunge Maalum ya Katiba na hatimaye Bunge hilo kuipigia kura ya kuipitisha Katiba Inayopendekezwa.
“Lilikobakia sasa ni Kura ya Maoni ya Wananchi. Tunadhani kuwa kama itakwenda kama tulivyopanga, Kura hiyo itapigwa wakati wowote mwezi Aprili mwakani. Bado tunaangalia tarehe mwafaka kwa ajili ya shughuli hiyo muhimu,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katiba hiyo ikipita, sote tutashangilia na kushereheka lakini matokeo ya Kura ya Wananchi ikiwa tofauti basi tutaendelea kuongozwa na Katiba ya sasa mpaka huko mbele wakati nchi yetu na wananchi watakapoamua tena kujaribu kupata Katiba Mpya.”

Baadaye leo, Rais Kikwete amekutana kwa mazungumzo na wakuu wa taasisi kubwa za fedha katika China za Benki ya Maendeleo ya China ya China Development Bank (CDB) na Mfuko wa Maendeleo wa China na Afrika wa China-Afrika Development Fund (CADF) kuzungumzia miradi mbali mbali ya Tanzania .
Mazungumzo hayo yalilenga kuona jinsi gani taasisi hizo zinavyoweza kuzisaidia benki za Tanzania za Tanzania Investment Bank (TIB) na Tanzania Agricultural Bank kuongeza mitaji yake ili kuweza kutoa mikopo zaidi ya shughuli za maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi ya China Poly Group na China Poly Technologies ambayo imekuwa inatoa mikopo kwa shughuli za maendeleo nchini katika sekta za umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO na ujenzi wa nyumba kupitia Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
22 Oktoba,2014

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.