Habari za Punde

Tanzania yasisitiza Azimio Kuhusu Walemavu wa Ngozi Liwe na Tija.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akilizungumza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  hapo siku ya Alhamis kabla Baraza hilo halijapigia kura Azimio linalotaka kuwapo kwa siku ya Kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi.  Kulia kwa Balozi ni Bi. Ellen Maduhu Afisa wa Uwakilishi anayeshughulika Kamati ya Tatu  inayohusika na masuala ya Haki za Binadamu, Utamaduni na  Masuala ya Jamii na alishiriki  kikamilifu katika  majadiliano ya kwanza   kuhusu Azimio hilo ambapo alihakikisha  Azimio limetambua juhudi zinazofanywa na Serikali  katika  kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na  kuzikabili changamoto wanazokumbana nazo.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakiwa katika mkutano  ambao ulipitisha  maazimio mbalimbali yaliyowasilishwa mbele ya Baraza  hiyo  na Kamati ya Tatu.  Baadhi ya Maazimio yaliyopitishwa katika mkutano huo uliofanyika siku ya Alhamis  lilikuwapo  linalopendekeza kuwapo  wa  siku ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu wa ngozi ( Albino).


Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  imesisitiza kwamba haitoshi kuwa na siku ya kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi ( Albino) pasipo kuwa na mikakati madhubuti inayolenga katika kuwawezesha.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi alipokuwa akizungumza muda mfupi kabla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa halijapigia kura Azimio linalotaka kuwepo kwa Siku ya Kimataifa ya Kuwatambua watu wenye Ulemavu wa ngozi.

Leo (Alhamsi) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokea mapendekezo ya maazimio mbali mbali ya liyowasilishwa mbele ya Baraza hilo yakitokea Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, 



Kamati inayohusika na masuala ya Haki za Binadamu,  Utamaduni na Maendeleo ya Jamii.
Miongoni mwa Maazimio hayo lipo lililohusiana na Haki za Binadamu ambapo ndani ya maazimio ya eneo hilo kuna azimio linalopendekeza kuwa siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Balozi Manongi amelieleza Baraza hilo kuwa,kimsingi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haipingi kuwapo kwa siku ya kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi.  Lakini inapata shida pale azimio hilo linaposhindwa kuainisha mchango na mikakati ya kimataifa ya kuwezesha jamii hiyo kukabiliana na changamoto mbali mbali.

Akiongea kwa msisitizo, Balozi Tuvako Manongi ameeleza kuwa  Tanzania  ni nchi ambayo ina idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wa ngozi na pamoja na changamoto na matatizo wanayokumbana nayo.

Amezitaja baadi ya changamoto hizo na ambazo pia zimeainishwa katika Tume ya Haki za Binadamu kuwa ni pamoja na kutopata huduma kamilifu za kiafya,  elimu, kunyanyapaliwa na madhira mengine.
“Kuna changamoto mbali mbali zinazowakabili,  Changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi na kutafutiwa ufumbuzi.  Kama nchi yenye idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Ujumbe wangu ulijjitahidi katika kuhakikisha kuwa pendekezo la Azimio hili ambalo leo limeletwa mbele ya Baraza hili linakuwa lenye tija na manufaa zaidi kwa walengwa kuliko lilivyo hivi sasa” amesema Balozi Manongi

Amesema kuwa pamoja na kwamba pendekezo hilo la kuwa na siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu wa ngozi ni hatua muafaka, lakini halitoi mwelekeo wa namna ya kushughulikia matatizo  yao pamoja na uwezeshwaji wao.

Ni  kwa sababu hiyo na kutokana na mapungufu hayo ambayo yalikuwa hayatoi nafasi kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na Juhudi za  Tanzania katika kuzikabili changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu wa ngozi.Ndiyo maana Tanzania kwa nia njema kabisa iliomba azimio hilo lipigiwe kura si kwa maana ya kulipinga azimio lakini kupinga azimio hilo kutokuwa na maslahi mapana kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amekwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa  Tanzania  na kama ilivyo kuwa kwa wanachama wengine,  imekuwa ikiaamini kuwa Chombo hicho kwa maana ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Mataifa kwa ujumla wake vinapaswa kupitisha maamuzi na maazimio yenye tija zaidi.

Azimio hilo limepitishwa kwa kupigiwa kura ambapo licha ya mapungufu yake,  inatambua kuwa  June 16 ya kila mwaka itakuwa ni siku ya Kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.