Habari za Punde

Dk Shein ahimiza ufanisi katika ulipaji na ukusanyaji kodi

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                            21 Disemba, 2014
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito wa kuongeza ufanisi katika ulipaji na ukusanyaji wa kodi nchini kwa kuwa ndio utakaowezesha serikali kukabiliana na changamoto za maendeleo inazokabiliana nazo hivi sasa.
 
“Lazima tuwe wastaarabu wa kulipa kodi...wako wafanyabiashara wanaofanya vizuri kwa kulipa kodi inayostahiki na kwa wakati lakini pia wako wengine wasiotimiza wajibu wao kikamilifu”alieleza Dk. Shein.
 
Dk Shein alitoa wito huo jana wakati alipokuwa akizungumza katika Mahafali ya Kumi ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar-SUZA yaliyofanyika katika Kampasi ya Tunguu nje kidogo ya mji wa Zanzibar.  
 
“Mapato makubwa ndio yatakayowezesha serikali kutoa huduma zaidi na za kutosha kwa wananchi ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya utoaji elimu nchini” alisema Dk. Shein.
 
Aliiambia jumuiya ya wanachuo na wageni waliohudhuria mahafali hayo kuwa serikali ingependa kutoa kila huduma kwa wanavyuo ikiwemo mikopo ya kutosha kwa kila mwanafunzi pamoja na huduma nyingine kama dakhalia(hsteli) na usafiri lakini dhamira hiyo haiwezi kutimizwa bila ya kuwa na mapato ya kutosha.
 
Kwa hivyo alisema ni wajibu wa kila mlipa kodi kulipa kodi inayostahiki na vyombo vya ukusanyaji kodi kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ili Serikali ipate mapato zaidi yatakayowezesha kutimiza mahitaji ya taifa.
 
Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Chuo hicho alisisitiza kuwa kodi ndio msingi wa mapato ya kila nchi huku akitolea mfano kuwa hata mataifa makubwa yaliyoendelea ambayo ni miongomi mwa wafadhili wetu wanaweza kufanya hivyo kwa kukusanya kodi vizuri.
 
Kwa hivyo katika hali ya sasa, Dk. Shein aliwaambia wahitimu hao kuwa haoni namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyoweza kutoa mikopo kwa kila mwanafunzi halikadhalika kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
“Katika hali ya sasa si Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wala Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye uwezo wa kumpatia mkopo kila mwanafunzi anayehitaji kwa kuwa hatuna uchumi unaotuwezesha kufanya hivyo” Dk. Shein alifafanua.
 
Katika risala yao kwa mgeni rasmi, wahitimu wa katika mahafali hayo pamoja na kuishukuru serikali kwa kuimarisha mazingira ya chuo lakini walieleza pia changamoto mbali mbali zinazowakabili ambazo zimekuwa kikwazo kwa wanafunzi kufanya vizuri.
 
Wanafunzi hao walieleza kuwa kutokuwepo hosteli kunawalazimu kuishi mbali na chuo na wengine kupanga katika nyumba za watu binafsi ambapo wamekuwa wakikabiliana na kero nyingi.
 
“wanafunzi wanaopanga wanakabiliwa na changamoto mbalibali ikiwemo kunyanyaswa na wenye nyumba kwa kupandishiwa kodi mara kwa mara, kukosa ulinzi na usumbufu mwingine kutokana na mazingira yasiyolingana na mahitaji yao” ilibainisha risala hiyo.
 
Matatizo mengine ni usafiri ambapo husababisha kuchelewa kufika kwa wakati na usumbufu katika kuwania usafiri huo na wananchi wengine.
 
Risala hiyo ilieleza pia kuwa mikopo ya wanafunzi wa vyuo bado haitoshelezi na kufafanua kuwa kati ya wanafunzi 4,020 wanaohitaji  mikopo ni wanafunzi 1,500 tu ndio waliopatiwa.
 
“Hata kwa wale wanaobahatika kupata mikopo hiyo, hucheleshwa na kuwafanya wanafunzi kuwa na madeni kwa muda mrefu”iliongeza risala hiyo.
 
Wanafunzi hao waliiomba Serikali kufikiria pia kuwapa mikopo wanafunzi wanaochukua mafunzo ya stashahada badala ya mikopo kutolewa kwa wanaochukua shahada pekee.
 
Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.