HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM TAIFA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE, KATIKA SHEREHE ZA KUTIMIZA MIAKA 38 YA CCM, KWENYE UWANJA WA MAJIMAJI,
SONGEA - RUVUMA,
TAREHE 01 FEBRUARI, 2015
Ndugu
Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mheshimiwa
Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu na mjumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa
Anne Makinda, Spika wa Bunge na Mjumbe wa Kamati Kuu;
Ndugu
Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu
Mike Mukula, Makamu Mwenyekiti wa NRM ya Uganda na ujumbe wake;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa Oddo Mwisho,
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma;
Waheshimiwa Wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa;
Wajumbe
wa Sekretarieti ya CCM;
Ndugu Verena Shumbusho, Katibu wa
CCM Mkoa wa Ruvuma;
Wenyeviti
wa Jumuiya za CCM;
Viongozi,
wananchama na wapenzi wa CCM;
CCM
Oyee!
Naomba nianze kwa kuwashukuru na
kuwapongeza wenyeji wetu kwa mapokezi
mazuri, hususan napenda kuwatambua wananchi, viongozi na wana-CCM wa
Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mwenyekiti wao ndugu Oddo Mwisho, Katibu wa Mkoa
Mama Verena Shumbusho, Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Ndugu Said
Mwambungu. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizi. Hakika zimefana
sana. Hii ni mara ya pili sherehe hizi kuadhimishwa
mkoani hapa. Mara ya kwanza ilikuwa
mwaka 1991 wakati wa kuazimisha miaka 14 ya CCM.
Tunatambua
kuwa mmefanya kazi kubwa ya maandalizi mpaka mmeweza kufanikisha shughuli ya leo kwa
kiwango cha juu. Waswahili wanasema “Usione vinaelea Vimeundwa”. Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kwa
uongozi wake makini uliowezesha mambo kuwa mazuri kiasi hiki. Hongera sana kwa hili na kwa kazi nyingi
nzuri unazofanya kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Leo
ni siku ya furaha kwangu na kwa viongozi na wanachama wenzangu wa CCM kote
nchini ya kusherehekea na kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa Chama cha
Mapinduzi. Tunastahili kuisherehekea siku hii kwa nderemo na vifijo kwa sababu
ya mafanikio makubwa ambayo Chama chetu kimeendelea kupata ndani ya Chama na
katika kuliongoza taifa letu. Katika miaka 38 ya uhai wake Chama chetu kimezidi
kuimarika na kimeendelea kuliongoza vyema taifa letu: kuna amani, utulivu na
maendeleo yanayoonekana.
Tumeeendelea
kuaminiwa na kutumainiwa na Watanzania. Kama ilivyothibitika na ushindi wa
kishindo katika chaguzi zote tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1995 mpaka
sasa. Hata mwaka huu itakuwa hivyo hivyo.
Dalili ya mvua ni mawingu: ushindi mnono tulioupata kwenye Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa ni dalili tosha kwamba Oktoba, 2015 watani zetu hawana chao.
Ninaposema
hivyo nawaomba wana CCM wenzangu tusibweteke tukadhani kwamba ndiyo
tumekwishafika. Bado safari ndiyo kwanza tumeianza na inaweza kuwa na
changamoto zake. Lazima tufanye kazi
tena kazi kubwa sana ndipo tutakapojihakikishia ushindi. Nguvu ya ushindi inaanzia kwenye Chama. Huu ni mwaka ambao kazi ya Chama ndani ya
Chama na kazi ya Chama ndani ya umma inatakiwa ifanyike kwa nguvu zaidi na kwa
ari kubwa zaidi. Lazima tuhakikishe tunao
umoja wa dhati na kwamba wanachama wetu
wanakuwa na mwamko wa hali ya juu wa kukipigania Chama katika kutafuta na kupata
ushindi kwa Udiwani, Ubunge, Uwakilishi, Urais wa Zanzibar na Urais wa
Muungano.
Huu
ni mwaka ambao wanachama na viongozi wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanakutana
mara kwa mara kwa mujibu wa Katiba na hata zaidi kuzungumzia mikakati ya kupata
ushindi na kuitekeleza. Huu ni mwaka
ambao lazima tuhakikishe kuwa tunazo rasilimali na nyenzo za kutuwezesha
kufanya kazi ya Chama ndani ya umma na kuwapatia ushindi wagombea wa Chama
chetu.
Huu
ni mwaka ambao kazi ya Jumuiya za Chama ya kukiwezesha Chama kuungwa mkono na
jamii pana ya Watanzania walio vijana, wanawake na wazazi inafanyika kwa
umahiri na ufanisi wa hali ya juu.
Bila
ya shaka, ndugu zangu mtayakumbuka maneno niliyoyasema kwa kuyarudia kuwa “Mwisho
wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwingine”. Najua baadhi yenu
mmezingatia na kuchukua hatua za kufanya maandalizi mapema ya uchaguzi wa mwaka
huu mara baada ya kumaliza uchaguzi wa mwaka 2010. Hao
nawapongeza. Lakini wapo viongozi na
wanachama ambao hawajafanya chochote.
Hawa, wananisikitisha kwa athari mbaya na hatari ya kupoteza ushindi
wanayokiletea Chama chetu.
Naomba
kila mmoja wetu ajipime yupo fungu gani. Kama upo kwenye kundi la kwanza
lililokwishaanza maandalizi natoa pongezi nyingi. Nawaomba muendelee kukamilisha ipasavyo. Kwa
wale ambao wapo kundi la wale ambao maandalizi yao ni ya kiwango kidogo au hawajaanza
kabisa lazima waanze na wakati ni huu.
Usikawie, unatakiwa kufanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi
kama ilivyo kauli mbiu ya CCM. Yapo mambo kadhaa ya kufanya ambayo tulikwishaambiana
tufanye. Miongoni mwao ni lile agizo la
kutaka kila ngazi ya Chama na hasa Wilaya na Mikoa kuwa na Mfuko wa Uchaguzi.
Wakati wake ndio huu sasa wa mfuko huo kufanya kazi iliyokusudiwa. Naomba tujiulize wangapi wanayo mifuko hiyo
na wangapi hawana. Kwa wale walionayo
wahakikishe ina rasilimali za kutosha.
Kama hazitoshi waweke mikakati ya kuitunisha mifuko hiyo. Kwa wale ambao hawajaanzisha wachune bongo
kuhusu namna ya kupata fedha za kuendeshea shughuli za uchaguzi. Sina budi
kuwatahadharisha kuwa msichukue fedha ambazo zitazua matatizo.
Ndugu
viongozi na ndugu wanachama;
Huu
ni mwaka wa kutambua ahadi zipi tulizotoa zimetimizwa na zipi bado. Kwa zile ambazo hazijakamilika wajibu wetu ni
kuweka mikakati ya kuzikamilisha. Kwa
zile ambazo hazitakamilika tutafute maelezo sahihi ya kutoa kwa wadau wa huduma
hiyo. Naamini hazitakuwa nyingi za
kuchosha. Mwaka huu siyo mzuri kwenda na madeni lukuki ya ahadi. Yanaweza kutupunguzia ushindi wetu.
Huu
ni mwaka wa kuongeza ukubwa wa jeshi letu la ushindi kwa kuongeza wananchama
wapya. Natambua tatizo la upungufu wa kadi lakini najua mipango thabiti iliyopo
ya kuleta kadi nyingi za kutosha wale waliopo nje. Tujiepushe na kuingiza
mamluki hivyo taratibu za kuingiza wanachama zizingatiwe ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Jambo
lingine kubwa na muhimu sana kufanya mwaka huu ni kuwatembelea wanachama na
wananchi na kuzungumza nao. Hatujaifanya vizuri sana kazi hii lakini
hatujachelewa. Sina budi kutoa pongezi
maalum kwa Katibu Mkuu wa CCM kwa ufanisi mkubwa aliopata kwa jambo hili. Sote hatuna budi kuiga mfano wake mzuri. Tuache kukaa maofisini tutoke kuzungumza na
watu kuwashawishi waunge mkono na kuipigia kura CCM katika uchaguzi ujao. Kila
Ofisi ya Mkoa na kila Ofisi ya Wilaya inalo gari la kuwawezesha kufanya kazi
hiyo. Tafadhali fanyeni hivyo, kwani bila ya kufanya hivyo hakuna uhakika wa
kupata ushindi. Kilichobakia kwa upande
wetu ni kutafuta vipando kwa Ofisi za Kata na Matawi. Tusaidiane pale
inapowezekana.
Uandikishaji wa
Wapiga Kura
Ndugu
wana CCM na ndugu Wananchi;
Jambo lingine muhimu katika kutafuta
ushindi ni kupatikana kwa wapiga kura.
Chama chetu kama vilivyo vyama vingine, hatuna budi kuwahimiza wanachama
wetu, wapenzi wetu na wananchi wengine wajitokeze kwa wingi kujiandikisha
kupiga kura. Mwaka huu wenye kadi mpya
za mpiga kura ndiyo watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu na katika
kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Asiyejiandikisha
hatapata fursa ya kushiriki kura ya maoni na uchaguzi mkuu. Kwa sababu hiyo nawaomba viongozi na wanachama
wa CCM wawe ndiyo wa kwanza kujitokeza kujiandisha. Pia wawe mstari wa mbele kuwahimiza wananchi
wengine kujiandikisha. Nawaomba jambo hili
mlipe uzito mkubwa kwani safari ya kutafuta na kupata ushindi inaanzie kwenye
kupata wapiga kura hususani wapiga kura wanaounga mkono Chama chetu na wagombea
wetu.
Kura ya Maoni
Ndugu
wananchi;
Kama mjuavyo, jambo kubwa lililo mbele
yetu ni kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendezwa itakayofanyika tarehe 30
Aprili, 2015. Maandalizi yote husika yanaendelea kufanyika ili kuwezesha kura
hiyo kutekelezwa kama ilivyopangwa. Kama nilivyokwishaeleza hivi punde
uandikishaji wa wapiga kura ni miongoni ma maandalizi hayo. Mengine ni
uchapishaji na usambazaji wa Katiba Inayopendekezwa.
Yapo
mambo kadhaa ambayo nawasihi viongozi na wanachama wenzangu mfuatilie kwa
karibu ili yasiwapite. Yale tunayoyajua tuwaambie. Miongoni mwa mambo muhimu
sana ambayo Chama hakina budi kujipanga vizuri ni kuhusu kutoa elimu kwa umma
kuhusu Katiba Inayopendekezwa na kampeni ya Kura ya Maoni. Watani zetu watatoa
elimu hasi kuhusu Katiba Inayopendekezwa,
sisi tutoe elimu chanya. Wenzetu watataka Katiba Inayopendekezwa isipite. Sisi tupige kampeni ikubalike. Nilisema siku ile Dodoma
wakati wa kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa na narudia tena leo kwamba Katiba Inayopendekezwa imebeba maslahi mapana ya
taifa letu. Hatujawahi kuwa na Katiba kama hii Inayopendekezwa. Misingi ya historia ya nchi yetu yaani kule
tulikotoka, tulipo sasa na tuendako imezingatiwa vizuri. Katiba hiyo inatambua maslahi
ya makundi yote nchini na kuyawekea utaratibu mzuri wa kutekelezwa. Wakulima,
wafugaji, wavuvi, wanawake, vijana, wasanii, wafanyakazi, wazee na watoto wametambuliwa
kwa kina na upana zaidi kuliko Katiba ya sasa.
Katiba
Inayopendekezwa imeshughulikia kero za Muungano na kujenga mazingira bora zaidi
kwa Muungano wetu kuimarika. Yale mambo yaliyokuwa yanaikwaza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na kuukwaza Muungano yamepatiwa ufumbuzi mwafaka. Sasa
Zanzibar itaendesha na kushughulikia mambo yake kwa uhuru mkubwa zaidi.
Ndugu
wananchi;
Kwa maoni
yangu sioni sababu ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa. Hatuna budi kutambua
kuwa tukiikataa Katiba Inayopendekezwa, Katiba ya sasa itaendelea kutumika
mpaka hapo mchakato mwingine utakapomalizika miaka mingi ijayo. Viongozi wa
vyama vinne vya siasa wamesikika wakisema watasusia kushiriki katika kura ya
maoni na kuwataka wanachama wao wasishiriki. Kauli hiyo imenisikitisha sana
ingawaje haikunishangaza hasa tukikumbuka waliyoyafanya wakati wa Bunge la
Katiba. Mimi nawaomba washiriki.
Nawasihi
wananchi wasiwasikilize. Wao wakitaka kususia waacheni wasusie lakini nyie
jitokezeni kupiga kura. Nawasihi msikubali
kupoteza mema mengi yaliyo katika Katiba Inayopendekezwa ati kwa sababu tu hakuna
Serikali Tatu walizokuwa wanazitaka. Kama kweli wananchi wa Tanzania wanakereketwa
na Serikali Tatu watathibitisha hiyo kwenye kura ya maoni.
Naomba
msibabaishwe wala kudanganywa na watu wanaotaka kuturudisha nyuma kutoka katika
hatua kubwa muhimu tutakazopiga kwa kuikubali Katiba Inayopendekezwa. Tusikubali
kubaki nyuma.
Uchaguzi Mkuu
Ndugu wananchi;
Kama mjuavyo mwezi Oktoba, 2015 nchi
yetu itafanya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge, Wawakilishi, Rais wa Zanzibar
na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa nchi
yetu kwani tunachagua Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mimi nataka Rais huyo awe mwana CCM.
Sisi sote katika CCM tunataka Rais atoke katika Chama chetu kwa sababu kama alivyousia Baba Wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere “Rais wa nchi yetu anaweza kutoka Chama chochote lakini Rais bora
atatoka CCM”.
Huu
ni usia mzito wenye maono ya mbali.
Tusiupuuze wosia huu bali tuuenzi.
Sisi katika Chama cha Mapinduzi tuwe mstari wa mbele katika kuuenzi wosia
huu kwa kupata mgombea aliye bora wa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi ujao. Mgombea ambaye wananchi
wakisikia jina lake likitajwa watasema naam, hapo sawa, hapo barabara. Lakini tukiteua mgombea ambaye watu wataguna
na kusema hata huyu? Tutakuwa tumemuangusha Muasisi wa Chama chetu na taifa letu katika wosia
wake. Bila shaka laana yake tutaipata. Na hilo likitokea itakuwa hasara kubwa
kwa taifa letu na msiba kwa CCM. Nchi
itayumba.
Lazima
tuhakikishe kuwa hatutafika huko. Watu
wazuri wapo wa kutosha katika CCM na naamini tunawajua. Kama hawajajitokeza tuwashawishi
wafanye hivyo. Ndugu zangu, tusifanye ajizi katika jambo hili kubwa na la
msingi kwa Chama chetu. Kushinda chaguzi
za dola katika sehemu zetu mbili za Muungano ndiyo madhumuni makuu ya kuundwa
na kuwepo kwa CCM.
Napenda kuwahakikishia wanachama wa
CCM na wananchi kuwa, Chama cha Mapinduzi ni Chama kilichokomaa, kilicho makini
na imara. Tunao utaratibu unaoeleweka na
kutabirika wa kuwapata wagombea. Inazo kanuni na vigezo vya wazi vya kuwapata
viongozi walio bora, na tunavyo vikao rasmi vya kuchuja na kuteua wagombea kwa
kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya Chama chetu. Hivyo basi, hapataharibika
jambo.
Naomba
niwahakikishie kwamba CCM itawapatia Watanzania wagombea bora ambao hawatawapa
wananchi mashaka wala kigugumizi cha kuwachagua. Tutafanya hivyo kwa nafasi ya Rais wa
Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Nawaomba wagombea
wazingatie na kuheshimu masharti ya Katiba ya Chama, Kanuni na Madili ya uteuzi
kwa wanaotaka kuteuliwa kugombea nafasi katika chaguzi za dola. Asiyezingatia
hayo asije akakilaumu Chama bali ajilaumu mwenyewe kwa makosa aliyoyafanya.
Utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi wa CCM
Ndugu wananchi;
Miezi minne iliyopita nilifanya ziara
ya mkoa huu wa Ruvuma kukagua shughuli za maendeleo. Nimefurahishwa sana na jitihada za kujiletea
maendeleo zinazofanywa na wananchi wa mkoa huu na mafanikio mnayoendelea
kuyapata. Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mipango mbalimbali ya
serikali unakwenda vizuri, kiasi cha kuwastajabisha hata wale waliokuwa na
mashaka na wasio tutakia mema.
Yako
mambo mengi tuliyoahidi kufanya ambayo tumeyakamilisha na mengine utekelezaji
wake unaendelea vizuri. Kilio cha miaka mingi cha wananchi wa mkoa huu kuhusu
barabara kimefanyiwa kazi vya kutosha. Ujenzi wa barabara ya Namtumbo – Songea na Peramiho - Mbinga kwa kiwango cha lami
umekamilika. Tunaendelea na ujenzi wa barabara ya Namtumbo – Tunduru na Tunduru
– Mangaka ili kuunganisha mkoa wa Mtwara na Ruvuma kwa barabara za lami.
Aidha, mipango ya kujenga barabara ya Mbinga
– Mbambabay kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika imefikia mahali
pazuri. Kwa upande wa usafiri katika
Ziwa Nyasa hivi sasa mchakato wa ujenzi wa chelezo cha kujengea meli ya ziwa
hilo kule kwenye bandari ya Itungi, Kyela unaendelea vizuri. Ujenzi wa chelezo
ukishakamilika ujenzi wa meli utaanza.
Kwa
upande wa umeme tunaendelea na ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa Kv 220
kutoka Makambako kuja Songea na hadi Mbinga na Namtumbo. Ujenzi wa njia hii ya umeme utakapokamilika
utawahakikishia wakazi wa mji wa Songea na mkoa wa Ruvuma umeme wa uhakika. Tumechelewa
kidogo kwa sababu ya kubadilisha ukubwa wa njia kutoka msongo wa Kv 132
tuliyotaka kujenga awali hadi Kv 220. Aidha, usambazaji wa umeme vijijini
unaendelea kwa kasi katika maeneo yote nchini. Tunataka ifikapo June, 2015 zaidi
ya vijiji 5,336 viwe vimepatiwa
umeme. Kati ya vijiji hivyo zaidi ya vijiji 300 ni vya mkoa wa Ruvuma. Haya ni mafanikio makubwa na ya kutia
moyo.
Kuhusu
sekta ya Afya nako pia tumepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma ya
afya kwa Watanzania. Kwa hapa Songea nimekwishatoa maelekezo kwa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii kuanza mchakato wa ujenzi wa hospitali mpya ya Mkoa wa
Ruvuma na hii iliyopo sasa iwe ni hospitali ya Manispaa ya Mji wa Songea.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea iharakishe kutenga eneo la kutosha kwa ajili
ya ujenzi wa hospitali hiyo ya mkoa ambayo itakuwa ni ya rufaa kwa yale ambayo
hospitali za Wilaya zitashindwa kumudu.
Haya
ni maeneo machache tu ambayo yanaonyesha hatua kubwa tuliyopiga katika
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na maendeleo ya mkoa huu. Ukweli ni kwamba
Ruvuma ya miaka 10 iliyopita siyo Ruvuma ya leo. Ninyi nyote ni mashahidi wa
mambo haya. Mwenye macho haambiwi tazama.
Ndugu
wananchi;
Jambo
la mwisho ambalo napenda kulizungumzia ambalo nilishalizungumzia kwenye hotuba
yangu ya mwaka mpya inahusu ununuzi wa mazao ya wakulima. Nilieleza siku ile
kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilikuwa bado haijalipa shilingi bilioni 89 kwa wakulima kwa
mazao yao iliyonunua. Nilielezea kutokufurahishwa kwangu na hali hiyo na kuagiza Wakala kulipa
deni hilo.
Nimeambiwa
kuwa tayari shilingi bilioni 15
zimeshatolewa na hapa Ruvuma mmepata shilingi
bilioni 8. Hivi karibuni shilingi bilioni 36 zitatolewa na
kubaki shilingi bilioni 38 ambazo
zitalipwa mwezi Machi.
Jambo
lingine ambalo tunaendelea nalo kulishughuikia katika Serikali ni kupata masoko
mengine kwa mazao ya wakulima. Kama
nilivyosema NFRA haiwezi kununua mazao yote ya wakulima nchini. Uwezo wake ni
kuhifadhi tani 240,000 wakati
uzalishaji wa mahindi hapa Ruvuma ni tani
993,350. Hata kama NFRA ingeamua
kununua mahindi yote kutoka mkoa wa Ruvuma peke yake isingeweza kuyamaliza.
Nimewaagiza
viongozi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa yote
nchini washirikiane na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya
Viwanda na Biashara kutafuta masoko mengi kwa ajili ya mahindi, mpunga na mtama
wa wakulima ndani na nje ya nchi.
Tunakokwenda
Ndugu wana CCM;
Mafanikio ya
miaka 38 ya Chama chetu yasitufanye tubweteke. Bado tunayo kazi kubwa mbele
yetu. Ili tuendelee kuongoza dola hatuna
budi tuendelee kuwa tumaini na kimbilio la wananchi wetu. Inatupasa kuwa
waaminifu kwa ahadi zetu na watiifu kwa matakwa yao. Kubwa sana, tunatakiwa tuwe tayari wakati
wote kubadilika na kwenda na wakati. Tunaweza kufanya hivyo ikiwa tutaendelea
kukuza demokrasia ndani ya Chama chetu na kuruhusu na kuvumilia tofauti za
mitazamo. Hiyo ndiyo siri ya uhai wa CCM
ambayo hatuna budi kuendeleza.
Tunapoanza safari ya kuelekea mwaka wa
39, hatuna budi sasa kuelekeza nguvu zetu kwenye kuondoa utegemezi wa kifedha
kutoka kwenye ruzuku na michango ya wafanyabiashara. Kutegemea misaada na michango si mambo endelevu
na huo hauwezi kuwa ni mkakati wa kutumainiwa wa kuimarisha Chama chetu. Wakati mwingine michango hii imetugharimu
ndani ya Chama chetu. Lazima tuwe
wabunifu katika kutafuta vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na rasilimali zetu nyingi
tulizonazo ili kuwezesha Chama kujitegemea. Tayari yako mawazo yaliyoibuliwa
kutokana na kazi nzuri ya Kamati iliyoongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Mweka
Hazina wetu Mheshimiwa Zakhia Meghji tumeagiza yatekelezwe. Naomba mtimize
ipasavyo wajibu wenu.
Hitimisho
Ndugu
wana CCM;
Leo ni siku ya furaha kwetu sote.
Wakati tukisherehekea mafanikio yetu tuwakumbuke pia waasisi wetu Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Mwenyeti wa TANU na Ndugu Sheikh Aboud
Jumbe aliyekuwa Mwenyekiti wa ASP kwa busara, hekima na uamuzi wao uliotukuka
uliowezesha kuzaliwa kwa CCM.
Tunawakumbuka pia wale wote waliotangulia mbele ya haki ambao walijitoa
maisha yao kujenga CCM. Hatuna budi
kuwaenzi kwa kutoa mchango mkubwa zaidi
mwaka ujao na miaka mingi ijayo. Tuhakikishe kuwa tunaimarisha Chama chetu na kutenda
mema kwa ajili ya nchi yetu na watu wake. Hili linawezekana ikiwa kila mtu
atatimiza wajibu wake. Kidumu Chama cha Mapinduzi!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment