Na Khamis Amani
Baada ya kuhukumiwa kutumikia
gerezani kwa muda wa siku 15 kila mmoja kwa
watoto sita wa muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Khamis Daruweshi,
askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana walifika Mahakama Kuu Vuga,
kuomba mmoja ya wafungwa hao ambae ni mtumishi wa jeshi, aruhusiwe akatumikie
adhabu mahabusu ya jeshi.
Zanzibar Leo iliwashuhudia
askari wa jeshi hilo zaidi ya 10, wakiingia mahakamani na kufanya mazungumzo na
Mrajisi wa mahakama, George Kazi, ambae ndie alietoa adhabu hiyo.
Mtumishi huyo wa jeshi aliehukumiwa
kifungo kwa kosa la kudharau amri ya mahakama pamoja na wenzake watano ni
Darwesh Khamish Darwesh.
Juzi Mrajisi huyo ambae pia ni
Hakimu wa mahakama ya Mkoa, aliwatia hatiani watoto hao sita wa familia moja
kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa siku 15 kila mmoja kwa kosa la kudharau
amri halali ya mahakama.
Wadaiwa wengine katika shauri
hilo ni Shaabani, Said, Asia, Atinji pamoja na Atika ambao wote hao ni watoto
wa marehemu Khamis Darwesh, ambao inadaiwa walikataa amri halali ya mahakama ya kutakiwa
kuhama katika nyumba yao inayobishaniwa baada ya mahakama kutoa maamuzi ya
kuuzwa.
Hata hivyo, Mrajisi huyo
aliwakatalia wanajeshi hao kumchukua mwanajeshi mwenzao kwenda kutumikia adhabu
jeshini, akisema uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa sheria.
Aidha aliwambia wanajeshi hao kuwa wana nafasi ya kuwasilisha
ombi la mapitio ya shauri hilo mahakama kuu ili liweze kusikilizwa.
Baada ya kauli hiyo, wanajeshi
hao waliondoka katika maeneo ya mahakama.
Habari za uhakika
zilizopatikana baadae jana zinasema baada ya zoezi la kumuomba Mrajisi
kumuachia mwanajeshi huyo, askari wengine wawili wa JWTZ walifika ofisini kwa
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, kwa kile kilichoelezwa kutafuta
njia ya kumnasua mwanajeshi mwenzao.
Mwanajeshi huyo na wenzake
walikumbwa na mkasa huo baada ya kushindwa kuielezea mahakama sababu
iliyowafanya washindwe kuhama ndani ya nyumba iliyoachwa na marehemu baba yao
Khamis Darwesh iliyouzwa kwa amri ya mahakama.
Nyumba hiyo iliyopo Kilimani
Kiungani plot namba 15, 17 na 18 iliuzwa na kampuni ya mnada ya Kumekucha kwa
idhini ya mahakama baada ya kufunguliwa kesi ya madai iliyohusisha familia ya
marehemu.
Mara baada ya nyumba hiyo
kuuzwa, kampuni ya Kumekucha iliwaandikia barua wakaazi wa nyumba hiyo kuhama
ili akabidhiwe mmiliki halali aliyeinunua
lakini familia hiyo ilikataa wakidai nyumba hiyo marehemu baba yao ambao
aliiweka wakfu.
No comments:
Post a Comment