STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 25 Machi, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wananchi wametahadharishwa juu ya vitendo vya makusudi vya kujenga katika maeneo ya barabara kwa matarajio kuwa Serikali itawalipa fidia wakati ujenzi au upanuzi wa barabara unapofanyika.
Tahadhari hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mbuyutende wilaya ya Kaskazini ‘A’ mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara za Kiashange-Kijini-Mbuyutende na Matemwe-Muyuni.
Aliwataka wananchi kuacha kujenga katika maeneo ya barabara na kuwakumbusha kuwa maeneo ya hifadhi ya barabara kuwa yanapaswa kuheshimiwa na kamwe watakaojenga watakuwa wanavunja sheria.
Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa wapo baadhi yao wanaanzisha na kuendelea na ujenzi katika maeneo ya barabara hiyo wakitaraji kupewa fidia na Serikali na kueleza kuwa watakaofidiwa ni wale tu waliojenga kabla ujenzi wa Barabara hiyo haujaanza.
Aliwakumbusha wananchi kuwa ardhi ni mali ya serikali na pale serikali inapoamua kuitumia ardhi hiyo kwa manufaa ya taifa wananchi wanaotumia ardhi hiyo watafidiwa mali zao na kusisitiza kuwa serikali wakati wote itafanya hivyo kwa kuzingatia sheria zilipo.
Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi mwaka 2010 na kuwa utekelezaji wake umechelewa kidogo kutokana na ukosefu wa nyezo ikiwemo fedha, vifaa na utalaamu.
Aliwaeleza wananchi hao kuwa ujenzi wa barabara hiyo unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inajengwa kwa kiwango cha kifusi kwa msaada wa kampuni ya Uwekezaji ya Pennyroyal Zanzibar Limited na Serikali itajenga awamu ya pili kwa kuitia lami kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza.
Dk. Shein alifafanua kuwa barabara hiyo ambayo itakuwa ya njia mbili itakuwa ya kisasa na kulifungua eneo hilo kwa kuwezesha miradi mikubwa ya kitalii kutekelezwa ukiwemo mradi mkubwa wa hoteli na nyumba za kitalii utakaojengwa na Kampuni ya Pennyroyal.
Alisema mradi huo na miradi mingine kama hiyo katika eneo la fukwe ya Matemwe Muyuni itabadili kiwango cha maisha cha wananchi hao na kuwa bora zaidi kwa kuwa watafaidika na huduma mbalimbali ikiwemo ajira.
Akiwa katika eneo hilo Dk. Shein alitembelea pia sehemu ya eneo litakalojengwa mradi mkubwa wa kitalii wa Amber Golf and Beach Resort unaaoendeshwa na Kampuni hiyo ya Pennyroyal.
Mradi huo utakaojumuisha hoteli na nyumba za kitalii katika pwani hiyo pamoja na kiwanja kidogo cha ndege unatarajiwa kuwa mradi wa aina ya pekee katika pwani ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu Dk. Juma Malik Akil barabara za Kiashange– Kijini- Mbuyutende na Matemwe - Muyuni zinaunganisha vijiji vya Kijini, Mbuyutende na Muyuni kutokea barabara kuu ya Mkwajuni-Matemwe.
Dk. Juma alisema barabara ya Kiashange-Kijini-Mbuyutende ina kilomita 9.4 wakati barabara ya Matemwe- Mbuyutende- Muyuni ina kilomita 7.6. Alibainisha kuwa kazi ya michoro na usanifu wa barabara hizo umefanywa na Kampuni ya Intercontinetal Cosultants and Technocrats kutoka India.
Wakati huo huo Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdallah Shaaban aliwaeleza wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani kuwa tatizo la maji katika vijiji hivyo litamalizika hivi karibuni baada ya mafundi kurekebisha tatizo lililojitokeza katika pampu za kusukuma maji za mradi wa kusambaza maji katika vijiji hivyo.
Alitoa maelezo kuhusu mradi huo baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Mheshimiwa Rais, Waziri huyo alieleza kuwa kazi ya kuchimba visima imekalimika pamoja na tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni tatu lakini tatizo la pampu limekwamisha utoaji huduma kikamilifu ambapo sasa tanki hilo limeweza kuhifadhi maji nusu ya uwezo wake.
Kwa hivyo alibainisha kuwa tayari mafundi waliofunga pampu hizo wameitwa kurekebisha tatizo hilo na kuwa zikitengemaa tu maji yatakuwa yanapatikana kwa wingi na kwa wakati wote.
Katika ziara hiyo fupi alikuwepo pia Waziri wa Mindombinu Juma Duni Haji, maafisa kutoka mfuko wa barabara pamoja na viongozi wa Kampuni ya Pennyroyal wakiongozwa na Mkurugenzi wake Bwana Brian Thomson ambaye pia ni mmliki wa kampuni hiyo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment