Habari za Punde

Karafuu zakamatwa Pemba

Na Haji Nassor, Pemba                       
JESHI la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, limefanikiwa kukamata karafuu kavu zilizoroa maji ya chumvi, gunia 18, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10, ambazo zinaaminika zilitaka kusafirishwa au kuingia kisiwani Pemba kwa njia ya magendo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia simu, Kamanda wa Polisi mkoani humo Sheikhan Mohamed Sheikhan alisema karafuu hizo zilikamatwa na wapiganaji wake, kwenye bandari ya Mkiang’ombe wakati mmiliki wa karafuu hizo akitaka kuzipakia ili kuzipeleka kwake kwa nia ya kutaka kuzianika.
Alisema kijana huyo Mussa Khamis Jabu (26) mkaazi wa Konde, ambae alidai kuziokota karafuu hizo bahari ya Kigamboni Dar-es Salaam, alikamatwa na Polisi wa kituo cha Polisi Konde na alipohojiwa alidai kuwa awali alipokea simu kutoka kwa wavuvi walioko Kigamboni kumpa taarifa za kuona karafuu hizo.
Kamanda alisema baada ya kuhojiwa ameachiwa kwa dhamana na baada ya uchunguzi kukamilika, hatua ya kumfungulia mashitaka zitafuta dhidi yake, kwa vile alichokifanya kitendo cha kuhujumu uchumi.
“Ni kweli kuna kijana alikamatwa na karafuu polo mbili kubwa na ndogo 14, akidai kwamba ameziokota na anataka kuzikausha maji ili baadae aziuze kituo cha ZSTC’’,alieleza Kamanda huyo.
Mapema Afisa Mdhamini ZSTC Pemba Abdall Ali Ussi, alisema karafuu hizo zinaonesha ziliinga maji ya chumvi ingawa kwa sasa wanazishikilia na kuzianika ambapo baadae watangalia uwezokano wa kuzinunua.
Mdhamini huyo alifafanua kuwa, hata kama kijana huyo anadai ameziokota kwenye bahari ya Kigamboni, suala la kuingiza karafuu au kutuoa kwa kutumia bandari bubu ni kosa.
“Sisi tunazo na tunangalia uwezekano wa kuzianika na baadae hatua za kuziuza na fedha kuingia serikali litafuata hapo baadae”,alieleza Afisa Mdhamini huyo.
Kwa upande wake kijana huyo Mussa Khamis Jabu mkaazi wa Konde, alisema wiki iliopita alipigiwa simu na wavuvi wa kupiga mbizi wa Pemba, walioko bahari ya Kiangamboni kwamba wakati wakiwa kazini wameona karafuu chini ya bahari.
Alifafanua kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, aliamua kupanda boti hadi huko na alipofika aliwakutana nazo gunia tatu ingawa baadae walipopiga tena mbizi wakafanikia kupata karafuu kwenye vipolo zenye ujazo wa gunia 18.
“Mimi baada ya kufika nikakodi mashuwa hadi bandari ya kwetu Mkiang’ombe wilaya ya Micheweni Pemba, na nilipofika nikatafuta gari ili nizipeleke nyumbani ili nizianike na kuziuza ndipo nilipokamatwa na Polisi’’,alifafanua.
Hata hivyo alisema ameshatumia wastani wa shilingi milioni 2.5 kuanzia kwenda Dar-es Salaam na kuzisafirisha karafuu hizo hadi kuzifikisha Kisiwani Pemba, ambapo ameiomba ZSTC watakapozinunua kumpatia mgao.
“Mimi bado najua ni zangu karafuu hizi nilizoziokota, na kama ZSTC wakiamua kuzinunua wao wenyewe baada ya kukauka basi nna tamaa ya mgao mkubwa’’,alizidi kufafanua.
Taarifa zilizopatika kutoka miji ya Konde na Wete, zinaeleza kuwa kijana huyo huwenda alitaka kuzisafirisha karafuu hizo kwa njia ya magendo na kutokana na kupigwa na dhoruba aliokumbana nayo hakufanikiwa zoezi hilo.
Baadhi ya wananchi walisema jeshi la Polisi ni vyema likafanya uchunguzi wa kina juu ya kadhia hiyo, na hasa kwa vile karafuu zinaonekana kuanza kuoza kwa kukaa baharini kwa muda mrefu.
Hili ni tukio la kwanza la aina yake kuwahi kutokea katika miaka zaidi ya 30 ya mtu kukamatwa akiingiza karafuu kisiwani Pemba, ambapo karafuu zaidi ya gunia 113 zilizokamatwa kwa kipindi cha miaka minne iliopita ni kutaka kupekelekwa nje ya Pemba na sio kuingizwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.