Na
Abdulla ali-maelezo.
Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imeanza kuwapatia nyenzo za kufanyia kazi Askari wa Jeshi
la Kujenga Uchumi (JKU) ili liweze kujiendesha na kujiinua kiuchumi.
Hayo
yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,. Tawala za Mikoa na Idara Maalum za
SMZ Mhe. Haji Omar Kheri wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Wawi
Mhe. Saleh Nassor Juma katika ukumbi wa Baraza
la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja.
Amesema
vijana wengi wanaoajiriwa kupitia Jeshi hilo ni
kwa ajili ya kuwapa mafunzo ya kizalendo na kujifunza mbinu za utendaji kazi
ikiwemo Ufundi, Kilimo, na Ujasiriamali na katika kufanikisha hilo Serikali imekuwa ikiwapatia nyenzo za
kufanyia kazi kwa kadri hali ya uchumi inavyoruhusu.
Amefahamisha
kuwa kwa sasa Serikali imeshawapatia vifaa vya kilimo ikiwemo Matrekta, vifaa vya
Ufundi, vifaa vya shughuli za Mifugo na kwa sasa Serikali inaendelea kutoa
mafunzo ya uvuvi kwa Jeshi hilo na kuiomba serikali kuwaongezea posho vijana
wanaojiunga na Jeshi la JKU kwa kujitolea ili waweze kukidhi mahitaji yao.
Ametanabahisha
kuwa Baraza la Wawakilishi limeshapitisha Sheria ya Wakala wa Ulinzi hatua
ambayo itapelekea kuimarika kwa Jeshi hilo kiuchumi kama ilivyo kwa wenzao wa Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) ambapo wameweza kumiliki Shirika la Biashara la SUMA JKT
pamoja na kampuni za ujenzi wa nyumba vinavyowasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua
uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Wakati
huohuo akijibu swali la pili la mwakilishi wa jimbo la wawi amesema Wizara yake
inaangalia uwezekano wa kupata fedha kutoka Wizara ya Fedha ya Zanzibar
kwa ajili ya ununuzi wa matrekta na vifaa vyengine vya kilimo ambapo hadi sasa
matrekta 2 aina ya FORD yameshapatikana ambayo yamegaiwa katika Kambi ya Kinumoshi
Unguja na Kangagani kwa Pemba .
Vilevile
amesema kwa upande wa miundombinu ya umwagiliaji maji Wizara yake imeshafanya
mawasiliano na Wizara ya Kilimo na Maliasili na kukubaliana kupatiwa mashamba
ya mpunga yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na mashamba hayo kuingizwa
katika mradi mkubwa wa umwagiliaji Kitaifa ambao unafadhiliwa na Korea na Nchi nyengine
wahisani.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment