Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipokea jarida la Grobal Peace Foundation kutoka kwa Rais wa taasisi hiyo James Flynn, ofisini kwake Migombani.
Na Khamis Haji OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na taasisi ya Kimataifa ya Global Peace Foundation katika kuhimiza amani na utulivu Duniani.
Maalim Seif amesema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka jumuiya hiyo, ulioongozwa na Rais wake, James Flynn huko ofisini kwake Migomnani mjini Zanzibar.
Amesema Dunia inakabiliwa na matukio mengi yanayo hatarisha amani na utulivu, hivyo mchango wa jumuiya hiyo ni muhimu katika kupatikana ufumbuzi wa migogoro hiyo na kuwezesha watu kuishi katika hali ya utulivu na kuvumiliana.
Maalim Seif amesema kwa upande wa Zanzibar kuna kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa watu wake kuishi kwa kuvumiliana, licha ya kuwepo watu wenye imani tafauti za kidini, na itikadi za kisiasa.
Hata hivyo, Maalim Seif alihimiza juhudi kubwa zichukuliwe kuimarishwa uchumi wa nchi na kuandaliwa mazingira yatakayowezesha kupatikana ajira za kutosha kwa vijana na kuwaletea matumaini mema katika maisha yao.
Amesema hatua hizo zitawaepushia kuchukua maamuzi yasiyokuwa ya busara yanayosababishwa na vijana kupoteza mweleko wa kimaisha ambapo matokeo yake ni amani na utulivu wa nchi kuvurugika.
Naye Rais wa Jumuiya hiyo, James Flynn amesema nguvu kubwa wanazielekeza kusaidia ujenzi wa familia zinazozingatia maadili mema, pamoja na kushirikiana na Serikali za nchi tafauti kusimamia utawala bora ambao una umuhimu wa kipekee katika kudumishwa amani na utulivu.
No comments:
Post a Comment