Habari za Punde

Balozi Mdogo wa India Afika Ofisini kwa Balozi Seif Kujitambulisha.

 Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana  Satendar Kumar akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana  Satendar Kumar akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
 Balozi Seif akibadilishana mawazo na Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana Satendar Kumar Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akipokea zawadi kutoka kwa Balozi Mdogo Mpya wa India Hapa Zanzibar Bwana  Satendar Kumar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis. OMPR                                                                                 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  ameyashauri  Makampuni  na Taasisi za uwekezaji  kutoka Nchini India kuwekeza miradi yao katika Visiwa vya Unguja na Pemba  ili kuitikia wito wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kukaribisha wawekezaji  mbali mbali kuwekeza hapa Nchini .

Alisema India  bado ina nafasi pana  kwa Makampuni yake kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi hasa katika Sekta ya Viwanda kama ilivyowahi kutumia fursa hiyo hapa Zanzibar katika miaka ya 80.

Akizungumza na Balozi Mdogo  Mpya wa India hapa Zanzibar  Bwana  Satendar Kumar hapo Ofisini kwake Vuga  Mjini Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Sekta ya Viwanda  ni eneo muhimu katika kukuza uchumi na kupunguza Umaskini.


Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa na malengo la kuimarisha sekta hiyo kwa azma ya  kulisaidia kundi kubwa la Vijana wasio na ajira ambalo limekuwa likiongezeka kila mwaka baada ya kumaliza masomo yao.

“ Ipo haja kwa wawekezaji wa Sekta ya Viwanda kutoka Nchini India kurejea tena Zanzibar kuwekeza miradi yao ya viwanda ili kusaidia uchumi wa Taifa pamoja na kupnguza wimbi la vijana wasio na ajira “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza India kwa jitihada zake za kusaidia Maendeleo ya Wananchi ikiwa nchi ya kwanza iliyojikubalisha  kuiunga mkono Zanzibar katika ujenzi wa Viwanda vidogo vidogo.

Akizungumzia miradi mengine ya Kiuchumi na Maendeleo ya Kijamii Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliiomba Serikali ya India kupitia Balozi wake Mdogo  huyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati za Maendeleo kwenye sekta hizo.

Balozi  Seif alitolea mfano Sekta za Elimu, Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari na Mawasiliano pamoja na kilimo ni miradi ambayo inafaa kupewa msukumo na India katika kuisaidia  Zanzibar Kitaaluma.

Alisema Zanzibar inakusudia kuimarisha Kilimo cha mpunga kwa lengo la kupunguza uagizaji wa  bidhaa ya mchele  nje ya Nchi ambayo ni chakula kikuu kinachotumia fedha nyingi za kigeni.

Balozi Seif alifahamisha kwamba mpango huo utasaidia uzalishaji wa mpunga kwa kiwango inachokadiriwa kufikia Asilimia 50% ambapo mahitaji ya mchele kwa sasa ni asilimia 80%  inayoagizwa kutoka nje ya Nchi.

Mapema Balozi Mdogo Mpya wa India hapa Zanzibar Bwana Satendar Kumar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba uhusiano wa Kidiplomasia kati ya India na Tanzania ikiwemo Zanzibar utaendelea kuimarishwa siku hadi siku.

Balozi Satendar alisema uhusiano huo umejengwa katika mpango Maalum wa Maendeleo wa India – Afrika  uliojikita kwa Wataalamu wa Nchi hiyo kusaidia taaluma katika sekta za afya, elimu, miradi ya Kazi za amali pamoja na 
Teknolojia ya Mawasiliano na Habari.

Alifahamisha kwamba mpango huo utajenga nguvu za ajira kwa Vijana wanaomaliza masomo yao ya Sekondari na vyuo vikuu ambao kwa sasa wanashindwa kuendesha maisha yao kutokana na ukosefu wa ajira ya kukidhi mahitaji yao ya maisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.