Habari za Punde

Semina ya kuwajengea Uwezo Wanahabari kuhusu Uandishi bora kwa Watu wenye Ulemavu wa Akili

 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Ally Uki akitoa mada katika Semina ya kuwajengea Uwezo Wanahabari kuhusu Uandishi bora kwa Watu wenye Ulemavu wa Akili Iliyoandaliwa na Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar (ZAPDD) kwa kushirikiana na Mwenvuli wa Asasi za Kiraia.
 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Ally Uki katikati akitoa mada katika Semina ya kuwajengea Uwezo Wanah`++-``abari. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar (ZAPDD) Juma Salim Juma na kulia ni Mdau kutoka ZAPDD Khalid A Omar.  Semina hiyo ilidhaminiwa na Mwenvuli wa Asasi za Kiraia.
Baadhi ya Washiriki kutoka Vyombo mbali mbali vya habari wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea Uwezo yaliyokuwa yakitolewa na Mhadhir wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Ally Uki katika Semina ya kuwajengea Uwezo Wanahabari juu ya kuandika habari za Watu wenye Ulemavu wa Akili. 

Picha na Faki Mjaka- Maelezo Zanzibar.

Na Faki Mjaka-Maelezo 

Waandishi wa habari nchini wameazimia kuboresha Fani ya Uandishi na Utayarishaji wa Vipindi Vinavyohusu Watu wenye Ulemavu wa Akili ili kuzidi kutetea Maslahi na Haki za Watu hao.

Maazimio hayo wameyatoa katika Semina ya Siku mbili ya kuwajengea Uwezo waandishi hao iliyoandaliwa na Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar (ZAPDD) kwa Msaada wa Mwenvuli wa Asasi za Kiraia.

Wamesema kuna kila haja ya kuboresha Habari na Vipindi wanavyotoa kutokana na Jamii ya Watu wenye Ulemavu wa akili kukumbwa na Changamoto nyingi na hivyo kukoseshwa haki zao za Msingi.

Aidha wameazimia kuongeza Ushirikiano wa karibu baina yao na Jumuiya ya ZAPDD ili kuona Jamii hiyo inawezeshwa kama zilivyokuwa jamii nyingine nchini.


Awali akitoa mada katika Semina hiyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu Ally Uki aliwataka Wanahabari hao kuwasaidia Walemavu hao wa Akili kwa kufichua maovu wanaotendewa ili Jamii ipate uelewa na kulinda haki zao.

“Ndugu zangu hawa Walemavu wa Akili Hawapewi haki ya Kutoa Ushahidi Mahakamani, Hawawezi kupiga kura, Wananyanyaswa na Kubakwa hivyo jitihada zenu ndio zitakazochangia kupata haki zao” Alisema Uki.

Kwa Upande wake Mdau wa Jumuiya ya ZAPDD Khalid A. Omar ameziomba Taasisi za Kiraia na Kijamii kuendelea kuihimiza Serikali kuongeza kasi ya kuzifanyia mapitia Sheria ambazo zinawakandamiza Watu wenye Ulemavu wa Akili.

Ameongeza kuwa ni vyema Taasisi hizo pia zisaidie 
kuishawishi Serikali kutenga Bajeti ya Angalau Asilimia 5%  ya gharama ya Sekta ya Afya ziende kwa Watu wenye Ulemavu.

Akifunga Mafunzo hayo Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya ZAPDD Tamrin Ali Said amesema wamelazimika kufanya kazi na Wanahabari wakiamini kuwa Mchango wao ni mkubwa katika kusaidia MApambano dhidi ya haki za Watu wenye Ulemavu wa Akili.

Tunajua Umuhimu wenu Waandishi ndio tukawaita hapa ingawa kuna Makundi mengine kama Viongozi wa Dini na Wasanii ambao nao tutafanya kazi kwa pamoja katika kusaidia kuwapatia haki zao Watu wenye Ulemavu wa Akili.

“Tunakuombeni sana Mujitolee katika kuandika na kutayarisha Vipindi vyenu ambavyo kwa hakika Mungu atakulipeni pale mnapofichua Ukandamizwaji wa haki za Watu wenye Ulemavu wa Akili” Aliomba Makamu Mwenyekiti.

Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar ZAPDD kwa sasa ina wanachama zaidi ya 2,600 ambapo imejikita zaidi katika kutetea haki na fursa Watu wenye Ulemavu wa Akili nchini.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.